Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tamu-chungu ya wapiganaji wa zamani kurejea nyumbani Rwanda baada ya mapigano msituni DRC

Raia 11 wa Rwanda wakiwemo wapiganaji wa zamani 4 na wategemezi wao wakiwa wamepiga picha ya pamoja katika kituo cha mpito cha Munigi, Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kabla ya kuondoka kurejea nyumbani 24 February 2022.
UN/Eskinder Debebe
Raia 11 wa Rwanda wakiwemo wapiganaji wa zamani 4 na wategemezi wao wakiwa wamepiga picha ya pamoja katika kituo cha mpito cha Munigi, Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC kabla ya kuondoka kurejea nyumbani 24 February 2022.

Tamu-chungu ya wapiganaji wa zamani kurejea nyumbani Rwanda baada ya mapigano msituni DRC

Afya

“Mke wangu niliyempata wakati napigana porini, alijifungua mtoto, sasa nikaona maisha ya kukimbia huku na kule porini na familia hayawezekani tena bora nirudi nyumbani Rwanda nikalee familia yangu.” Ni Mukeshimana Jean-Nepo, mpiganaji wa zamani wa kikundi cha Raiya Mutomboki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC akizungumza kwa furaha siku ya kurejea nyumbani Rwanda tarehe 24 mwezi Februari mwaka 2022.
 

Akiwa kwenye kituo cha mpito cha Munigi kwenye mji wa Goma jimboni Kivu Kaskazini, nchini DRC, Jean-Nepo amevalia nguo mpya kabisa kuanzia shati, suruali, koti, na raba nyeupe, vifaa ambavyo wamepatiwa na mradi wa Kupokona silaha, kuvunja vikundi na kujumuisha wapiganaji wa zamani katika jamii, DDR,  mradi unaotekelezwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO. “Nimefurahi sana sijawahi kuvaa hivi, porini nguo zilikuwa na chawa,” anasema Jean-Nepo.

Mambo tayari! Mukeshimana Jean-Nepo akijitazama kwenye kioo, huku mkewe Uwezimana Mapenzi akiwa amembeba mtoto wao muda mfupi kabla ya kuondoka kituo cha mpito cha Munigi, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.
UN/Eskinder Debebe
Mambo tayari! Mukeshimana Jean-Nepo akijitazama kwenye kioo, huku mkewe Uwezimana Mapenzi akiwa amembeba mtoto wao muda mfupi kabla ya kuondoka kituo cha mpito cha Munigi, jimboni Kivu Kaskazini nchini DRC.

Si peke yake anayerejea nyumbani, la hasha, wako 11, miongoni mwao ni wapiganaji wa zamani wanaume 4, wanawake 2, na watoto 5, mmoja wa watoto hao ni Uwase Josiane mwenye umri wa mwezi 1, ambaye ni mtoto wa Jean-Nepo na mkewe Uwineza Mapenzi mwenye umri wa miaka 20.
Ilikuwaje akapigana msituni?

Maisha yalinivuruga nikaingia kupigana msituni. Sasa nafurahi naenda nyumbani nikifa nazikwa kwenye ardhi ya Rwanda, nafurahi sana! - Mukeshimana Jean-Nepo, Mpiganaji wa zamani wa msituni

Wazazi wa Jean-Nepo walikimbia mauaji ya kimbari Rwanda mwaka 1994, ndipo yeye akazaliwa DRC na akiwa na umri wa miaka 16 wazazi walirejea nyumbani, lakini yeye alikataa akabaki mwenyewe. Maisha yalikuwa magumu na ndipo akalaghaiwa akatumikishwa vitani kwa miaka 10. “Maisha porini yalikuwa magumu, huwezi kufanya mradi wowote, unakimbia kila siku na kuna wakati wanakupiga.”

Mapenzi ambaye ni mke wa Jean-Nepo akiwa amebeba mwanae anasema hakuweza kukataa kwenda porini kwa kuwa mumewe alimwambia twende, “siwezi kukataa” lakini maisha yalikuwa magumu ili mtu aweze kula ni lazima “waende wakaibe vyakula vya watu ndio mpike. Unakula vyakula vya wizi ndio furaha gani? Hata taulo za kike zilikuwa shida, maji tulikuwa tunateka mtoni. Pindi waume zetu wameenda kupigana, na sisi tulikuwa tunapigwa.”

Wawili hawa wapendanao baada ya siku ya kuondoka kufika walifungasha virago vyao na kuhakikisha hakuna wanachosahau kwenye makazi yao ya muda hapa Munigi.

Nyirabisamana Pelagie (kushoto) na mwanae wakichukua mlo kabla ya kuondoka kambini. Mlo ni wali na maharage.
UN/Eskinder Debebe
Nyirabisamana Pelagie (kushoto) na mwanae wakichukua mlo kabla ya kuondoka kambini. Mlo ni wali na maharage.

MONUSCO DDR inafanyaje kunusuru walio tayari kurejea?

MONUSCO-DDR ni kitengo kilicho chini ya Idara ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za ulinzi wa amani na jukumu lao ni kuleta amani kwa kufainikisha kuvunja vikundi na wale wapiganaji wanasaidia kujumuishwa uraiani iwe katika nchi wanamopigana au nchi walikotoka.

John Bashali afisa kutoka MONUSCO-DDR Goma anasema wanyarwanda hawa 11 walipata taarifa kupitia ujumbe unaorushwa kwenye redio huko msituni na walitumia redio kwa kuwa wapiganaji hao huwa wana redio za mkononi. “. “wakati umefika unapaswa kusalimisha silaha na kurudi nyumbani, usiwe na hofu, kuna amnai nyumbani, na tutakuwezesha urejee nyumbani vizuri.” Na kwa wale wanaotikia wito wanaweza kupiga namba ya simu isiyo na utambulisho ili kuepusha wao kutambuliwa na kukumbwa na visasi kutoka kwa wenzao ambao bado wako msituni. Gharama za simu zinalipwa na MONUSCO.

Kituo cha mpito cha Munigi, Goma

Kilianzishwa mwaka 2014 na kinahifadhi wapiganaji wa zamani kutoka DRC na pia nchi za kigeni pamoja na wategemezi wao. Kutokana na janga la COVID-19, kanuni zote za kujikinga zinazingatiwa ikiwemo maji ya kunawa mikono na sabuni pamoja na uvaaji wa barakoa.

Wakiwa hapa wanapatiwa malazi, chakula, wanapata taarifa mbali mbali kupitia televisheni, wanacheza michezo kama vile mpira na ndio maana Jean-Nepo ndoto anacheza soka namba 11 na ndoto yake ni kucheza soka la kimataifa.

Bwana Bashali anasema “hapa tunawafundisha mambo ya amani na namna ya kuishi na kujigharamia, tunawapatia mavazi na kitu kidogo cha kuwasaidia wakifika kwao.” MONUSCO inaamini kuwa hatua hii ni muhimu kwa kuwa wapiganaji hawa wa zamani  wamechana vita inaendelea, sasa wameondoka huko. Pili walikuwa wanafanyia fujo wakazi sasa hiyo imeisha. Na tatu huku Mashariki ya DRC wananyanyapaliwa wanaelezwa hawapaswi kubakia huku, tumewahamasisha sasa wanarejea nyumbani.”

Ikumbukwe kuwa majukumu ya DDR yanatokana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2098 la tarehe 28 mwezi Machi mwaka 2013 ambalo lengo lake ni mosi, kufaniisha kuvunja vikundi na kurejesha makwao wapiganaji wote wa kigeni na wategemezi wao, pili; kukusanya na kutokomeza silaha zinazosalimishwa na tatu; kuchangia katika kufanikisha miradi ya kitaifa ya kupokonya silaha, kuvunja vikundi na kujumuisha wapiganaji wa zamani kwenye jamii.

Nizeyemukiza Anasthase (kushoto)  mwenye umri wa miaka 45 alikuwa mpiganaji na kundi la Nyatura, DRC. Mkewe aliuawa porini vitani na waasi. Sasa anarejea nyumbani kwa wazazi wake na watoto.
UN/Eskinder Debebe
Nizeyemukiza Anasthase (kushoto) mwenye umri wa miaka 45 alikuwa mpiganaji na kundi la Nyatura, DRC. Mkewe aliuawa porini vitani na waasi. Sasa anarejea nyumbani kwa wazazi wake na watoto.

Mchanganyiko wa furaha na huzuni kwa Anasthaze

Wakati Jean-Nepo anarejea nyumbani kwa furaha na mkewe pamoja na mtoto, hali ni tofauti kwa Nizeyemukiza Anasthase mwenye umri wa miaka 45 ambaye alijikuta DRC wakati akikimbia mauaji ya kimbari Rwanda mwaka 1994. Alitumikishwa katika kikundi cha Nyantura nchini DRC.

“Maisha porini hakuna nyumba, hakuna chakula, hakuna malazi,” alisema huku akiwa anaonekana kumbukumbu za porini zinamuumiza. “Narudi nyumbani baada ya kusikia kuwa wazazi wangu bado wangali hai, bora nirudi kwa wazazi na kwa watoto wangu.”

Alipoulizwa mke wake amemuacha wapi? Swali hilo lilitonesha kidonda kwani alijibu kwa huzuni, “mke wangu walimuua porini.” Na ujumbe wake kwa ambao wanapigana ni kwamba warejee nyumbani, “waache vita, kwa kuwa vita haijengi bali inabomoa. Tumeacha watu bado wanapigana huko. Mimi narudi nyumbani nitafanya kazi ya kulima nihudumie watoto.”

Mukeshimana Jean-Nepo akiwasili kwenye kituo cha mpaka wa Rwanda na DRC akiwa amembeba mtoto wao mwenye umri wa mwezi mmoja Uwinase Josiane.
UN/Eskinder Debebe
Mukeshimana Jean-Nepo akiwasili kwenye kituo cha mpaka wa Rwanda na DRC akiwa amembeba mtoto wao mwenye umri wa mwezi mmoja Uwinase Josiane.

Je wakifika Rwanda wanafanya nini?

Safari ya kutoka Munigi hadi mpakani mwa DRC na Rwanda ikianza, wapiganaji hawa wa zamani na wategemezi wao wana ndoto ya kubadilisha maisha yao wakifika nyumbani.
Bwana Bashali anasema hadi kufikia hatua hii, mazungumzo yalikwishafanyika na upande wa serikali ya Rwanda ambapo wakifika mpakani wanakabidhiwa upande wa pili na taratibu za nyaraka zinakamilika ikiwemo kupimwa virusi vya Corona au COVID-19.

“Wakishaingia Rwanda wanapelekwa kituo cha mpito cha Mutobo ambako wanapatiwa mafuzo ya kati ya miezi miwili hadi mitatu, mafunzo kama vile stadi za kazi ili waweze kujimudu kimaisha baada ya kurejea nyumbani,” amesema Bwana Bashali.