Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ofisi ya MONUSCO Lubero, Kivu Kaskazini yafungwa

Bendera ya Umoja wa Mataifa ikikabidhiwa kwa maafisa wa MONUSCO nchini DRC kuashiria kufungwa kwa ofisi ndogo za ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani kwenye eneo hilo lililoko kilometa takribani 140 kutoka mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini.
UN/George Musubao
Bendera ya Umoja wa Mataifa ikikabidhiwa kwa maafisa wa MONUSCO nchini DRC kuashiria kufungwa kwa ofisi ndogo za ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda amani kwenye eneo hilo lililoko kilometa takribani 140 kutoka mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini.

Ofisi ya MONUSCO Lubero, Kivu Kaskazini yafungwa

Amani na Usalama

DRC, MONUSCO umefunga kituo chake kilichoko Lubero jimboni Kivu Kaskazini baada ya kuweko huko kwa miaka 21.Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wake wa kujiondoa kwa utaratibu kutoka DRC, kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia ombi la serikali ya DRC.

Kituo hicho kilikuwa na vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka India, Afrika Kusini, Morocco na Nepal ambao walishiriki tukio hilo sambamba na wageni wengine. Shuhuda wetu alikuwa mwandishi wetu huko DRC, George Musubao kutoka kijijini Mulo, wilaya ya Lubero, kilometa 140 kutoka mji wa Beni jimboni Kivu Kaskazini.

Tukio lilifanyika saa saba mchana jumanne kwa saa za DRC ambapo bendera ya bluu ya Umoja wa Mataifa ilishushwa, ili kutoa nafasi kwa ile ya DRC. Katika uwanja wa kituo hiki cha kijeshi ambacho kilikuwa na walinda amani wengi, nyuso za wageni rasmi na wakazi wa eneo hilo katika sherehe ya kuwaaga zilionyesha furaha, lakini pia majuto, huzuni na wasiwasi kwa sababu ya kufungwa kwa kituo hiki cha MONUSCO.

MONUSCO msitusahau wanawake wa Lubero

Angel Kawalina Kavugho, Mratibu wa kikundi cha wanawake, lakini pia mkazi wa Lubero, akaelezea mafanikio makubwa ya MONUSCO kwa niaba yao akisema, “kile ambacho sitakisahau kuhusu uwepo wa MONUSCO ni ushirikiano. Walitufundisha kuhusiana na ukatili wa kijinsia. Tunasikitika kuondoka kwao, kwa sababu walitusaidia sana. Kujenga chumba cha mikutano kwa ajili ya wanawake na masoko ya starehe. Tunaomba MONUSCO isiwasahau wanawake wa Lubero."

Mwakilishi wa mashirika ya kiraia hapa Lubero, Hilaire Kamabu anasema “tunaishukuru MONUSCO kwa msaada kwani walituhimiza sana katika mafunzo mbalimbali ya jinsi ya utetezi, jinsi ya kulinda mazingira na mengine mengi, kozi hizi zimetufundisha kutekeleza majukumu yetu kikamilifu, mafanikio mengine MONUSCO imejenga madaraja, vilalo na hata aliahidi kujenga ofisi ya utawala ya wilaya letu".

Tumefunga Lubero lakini haimaanishi UN inaondoka

"MONUSCO inaondoka Lubero, lakini sio Umoja wa Mataifa," alisema Josiah Obat, mkuu wa Ofisi ya MONUSCO-Beni-Lubero, ambaye alifunga rasmi kituo cha Lubero.

Aliongeza kuwa "leo ni siku ya mwisho kwa hii ofisi ya MONUSCO hapa Lubero. Tumefanya kazi pamoja na viongozi wa eneo hili ofisi ifungwe. Nimechukua bendera ya Umoja Wa Mataifa ninarudia nayo mjini Beni. Lakini kufungwa kwa ofisi hii haimaanishi kwamba MONUSCO inakata uhusiano na watu wa Lubero.”

Badala yake amesema wao wako Beni na wataendelea kushirikiana na watu wa Lubero. “Kuna vitu vingi ambavyo tumefanya hapa pamoja tumejenga soko, ofisi ya shirika la kiraia pia tuna miradi mbalimbali ambayo bado hatujamaliza. Tunadhani kwamba tutaendeleza ushirikiano ili tumalize kufanya miradi yote. Tunaalika wananchi waendelee na kazi ambazo tumeanza ili amani idumu katika hii sehemu"

MONUSCO na urejeshaji wapiganaji waasi

Tangu mwaka 2002, kupitia Kitengo chake cha DDR cha kuvunja makundi ya waasi, kupokonya silaha na kujumuisha kwenye makundi wapiganaji,  MONUSCO imewarejesha nchini Rwanda waasi 25,000 wa kigeni wa FDLR. Kwa hesabu hii imeongezwa wapiganaji 11,000 wa zamani kutoka makundi yenye silaha, ambao tayari wameunganishwa tena, ambao wengi wao wanaingia katika jamii kwa msaada wa MONUSCO.

Baada ya kufunga ofisi Lubero, MONUSCO imekabidhi  samani na vifaa vya ofisi, jokofu, mahema,  majengo,  kompyuta, mapipa makubwa ya taka kwa washirika wake, ofisi ya ulinzi wa raia, vyama vya wanawake pia na utawala wa eneo la Lubero.