Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuondoka kwa MONUSCO DRC,wananchi wasema sharti kuu ni utulivu

Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa ziarani nchini DRC.
MONUSCO Video
Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa ziarani nchini DRC.

Kuondoka kwa MONUSCO DRC,wananchi wasema sharti kuu ni utulivu

Amani na Usalama

MONUSCO ambao ni ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,DRC uko kwenye mchakato wa kuondoka nchini humo na kukabidhi jukumu la ulinzi na usalama kwa serikali. Tayari imeshaondoka maeneo ya Kasai na jimbo la Tanganyika. 

Soundcloud

Hivi sasa imesalia majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri. Umoja wa Mataifa umeweka vigezo vya MONUSCO kuondoka nchini humo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024. Katika kukagua maendeleo ya mpango huo, kiongozi mwandamizi wa UN nchini DRC amezuru majimbo ya Kivu Kusini, Kivu Kaskazini na Ituri, 

Helikopta ya Umoja wa Matafa ikiwa kwenye anga la jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na ugeni. Ardhini ni kwenye kambi ya MONUSCO maandalizi ya mapokezi yaaendelea. 

Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa ziarani nchini DRC.
MONUSCO Video
Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa ziarani nchini DRC.

Kuwasili kwa Bi.Keita 

Mgeni ni Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC. Salamu za kijeshi kutoka walinda amani wa UN kutoka India wanaohudumu hapa Lubero Kivu Kaskazini. 

Bi, Keita akaingia eneo ambamo mkutano unafanyika, mkutano ambao lengo lake kujadili mpango wa mpito kwa hatua inayofuata ya MONUSCO kuondoka nchini DRC.  

Kikao na wawakilishi wa wanajamii Kivu Kaskazini 

Hivyo, Bi. Keita ambaye pia ni Mkuu wa MONUSCO alifika eneo hili kujionea hali halisi ya usalama na changamoto zinazokumba wakazi kwenye eneo hili ambamo bado MONUSCO ina kambi za kijeshi. 

Washiriki wa mkutano huu hapa lubero ni pamoja na wawakilishi wa vikundi mbalimbali, kama vile mashirika ya kiraia na vikundi vya wanawake.  

Mwanamke mmoja akatumia fursa hii kuonesha kazi za mikono za ufumaji wa nguo na kofia kwa kutumia nyuzi za sweta. Bi. Keita hakusita kuijaribu… ikamtosha na akaivaa na mkutano ukaendelea. Wanawake, wanaume wakijadili amani na usalama kwenye eneo lao. 

Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC akipokea zawadi kutoka kwa wanawake wajasiriamali wa ushonaji.
MONUSCO Video
Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini DRC akipokea zawadi kutoka kwa wanawake wajasiriamali wa ushonaji.

Yeye ni mwanamke kama sisi ametutia moyo - Françoise 

Huyo ni Françoise Kahindo mmoja wa wanawake walioshiriki mkutano huu na kando mwa kikao akasema“mkutano kwetu sisi ulikuwa mzuri kwa sababu tumemkaribisha mwanamke kama sisi, ametueleza madhumuni ya ziara yake. Amefika hapa kuzungumza nasi na kufahamu matatizo tunayokumbana nayo kama wanawake.” 

Bi. Kahindo akaendelea kufafanua kwa kina kile alichokiona kizuri zaidi kwenye mkutano ya kwamba “mazungumzo yalikuwa tulivu. Tulijadili kile ambacho tunapitia sisi wanawake. Tulimshukuru kwa kile anachotufanyia kwenye kitongoji na mji wa Lubero. Ni mwanamke ambaye anataka kuelewa shida zetu, anataka kutambua uwezo wetu na hilo ndilo jambo tumeshukuru.” 

Usalama na utulivu view msingi wa kuondoka kwa MONUSCO 

Katika ukumbi huu ama hakika wanawake walikuwa wasikivu, wakifuatilia kwa makini. Lakini si peke yao hata wanaume walikuwemo. Mathalani John Kambale, Mratibu wa Kikundi cha vijana, Lubero yeye akizungumzia hoja ya MONUSCO kuondoka. 

“Masharti kwa MONUSCO kuondoka si mawili, ni moja tu. Ni usalama. Lazima tuhakikishiwe kuna usalama DRC. Na ndio maana amesisitiza kuwa ujumbe huo bado upo hapa, ijapokuwa uko katika mchakato wa kasi wa kuondoka. Tumesema kuna changamoto tatu: Chaguzi zinazokuja, waasi wa ADF na M-23 ambao bado wako hapa. Halikadhalika kuna changamoto za shughuli za kiuchumi na kijamii kwa jamii ambazo zinataka kupata huduma za msingi zilizo bora.” 

Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa ziarani nchini DRC.
MONUSCO Video
Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa akiwa ziarani nchini DRC.

Kutoka Kivu Kaskazini hadi Ituri 

Mwisho wa kikao Kivu Kaskazini ikawa mwanzo wa safari nyingine kwa Bi. Keita na ujumbe wake kuelekea kambi ya wakimbizi wa ndani ya Lala iliyoko takribani kilometa 100 kutoka mji mkuu wa jimbo la Ituri, Bunia, mashariki mwa DRC, ukanda ambao bado waasi ni tishio kwa raia.  

Safari ilifanywa kwa helikopta ya Umoja wa Mataifa. Baada ya muda helikopta ikatua Bayo kwenye kambi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Bangladeshi, wanaohudumu MONUSCO. 

Kutoka Bayo hadi kijiji cha Lala ni takribani kilometa 11, hivyo msafara wa gari kuelekea Lala.  

Baada ya mapokezi kutoka kwa viongozi, moja kwa moja walielekea eneo lenye makaburi ambamo kuna kaburi la pamoja. 

Vilio vyatawala eneo la Lala jimboni Ituri 

Vilio vilisikika kutoka kwa wanawake waliofika hapa ambapo kiongozi wa kambi ya Lala alimweleza Bi. Keita ya kwamba tarehe 12 juni mwaka huu waasi wa CODECO walivamia kambi ya Lala na kuua watu 46 kati yao watoto 23. Na kwamba watu 44 walizikwa kwenye kaburi la pamoja lililoko lango la kuingilia kambini. 

Baada ya Bi. Keita kuweka shada la maua kwenye kaburi hili alipata fursa ya kuzungumza na wakimbizi wa ndani kusikiliza maoni yao hususan usalama. 

Tunalala kwa hofu na hatulali kambini- Julie 

Julie Malosi mkimbizi wa ndani hapa Lala anasema tangu kufanyika kwa mashambulizi, tunaishi kwa shida. Shambulizi lilifanyika usiku, tunaogopa kuishi kambini. Usiku tunaenda kulala eneo kubwa. Na zaidi ya yote hatuendi shambani kulima, wengi wanauawa huko. Tunategemea vibarua kutoka kwa watu hapa karibu na kambi ambapo tunapata faranga 1,000 kujikimu.” 

Julie Malosi mkimbizi wa ndani katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Lala nchini DRC.
MONUSCO Video
Julie Malosi mkimbizi wa ndani katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Lala nchini DRC.

Faranga 1,000 ni sawa na dola senti 50. Julie akimulika kipato na mlo, mkimbizi mwingine Deogratias Bura Lomo anasema shambulio hilo limepatia watu kiwewe na zaidi ya yote, “huu ni mfululizo wa mashambulio hapa Lala lililosababisha vifo vya watu 64 akiwemo mwanangu wa kiume Maki Rogacien aliyekuwa na umri wa miaka minane. Watu hawajui la kufanya, hakuna msaada wa kibinadamu, wana kiwewe, wanahitaji msaada wa kisaikolojia. Wakimbizi wanatoa wito kwa serikali na jamii ya kimataifa iwezesha kurejea kwenye jamii zetu.” 

Suala muhimu tuendelee kujengea uwezo FARDC na Polisi wa Taifa – Bi. Keita 

Tamati ya ziara yake hapa Ituri, ilimrejesha Bi, Keita kwenye mji mkuu wa DRC Kinshasa ambako akizungumza na waandishi wa habari Jumatano Julai pili amesema katika ziara zake aliokutana nao wameomba serikali iimarishe uwepo wa jeshi la serikali, FARDC na Polisi hasa kwa muktadha wa kuondoka kwa MONUSCO, ili kuepusha hatari ya kushuhudia mauaji kila siku. 

Amesema ni ombi pia la MONUSCO ndani ya mfumo wa kuondoka taratibu, kiwajibu na kiundelevu, kushirikiana na serikali kuweka mpango bora wa kuondoka kimkakati kwenye maeneo huku ikizingatia uimarishaji wa jeshi na polisi wa kitaifa.