Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutoka askari wa msituni DRC hadi mwajiriwa wa UN Goma 

Fabien Mwingwa akiwa ofisi kwake. Yeye ni mpiganaji wa zamani wa msituni na sasa ameajiriwa na MONUSCO, Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC kama askari wa zimamoto.
UN/Eskinder Debebe
Fabien Mwingwa akiwa ofisi kwake. Yeye ni mpiganaji wa zamani wa msituni na sasa ameajiriwa na MONUSCO, Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC kama askari wa zimamoto.

Kutoka askari wa msituni DRC hadi mwajiriwa wa UN Goma 

Amani na Usalama

Machungu niliyopata nikipigana msituni, chawa waliozingira nguo zangu pamoja na majonzi yaliyokuwa yanampata mama yangu ndio chanzo cha mimi kuamua kusalimisha silaha na kurejea uraiani. 

 

Huyu si mwingine bali ni Fabien Mwingwa, akizungumza na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa mjini Goma jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. 

Akiwa amevalia sare  yake ya kazi ya kitengo cha Zimamoto cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, Bwana Mwingwa anasema ametoka mbali na hana budi kushukuru MONUSCO na zaidi ya yote Umoja wa Mataifa.

Tweet URL

MONUSCO imemtoa wapi? 

Nikiwa na umri wa kati ya miaka 16 na 17 mwaka 1998, nilijiunga na kikundi cha wanajeshi hapa Goma tukiambiwa tunakwenda kufanya kazi ya kukomboa nchi kwani viongozi walikuwa wanaongoza kikabila waongoze nchi nzima. Tuliitwa kisiri na kuahidiwa kuwa tukikomboa nchi tutakuwa na maisha mazuri.  
Bwana Mwingwa walipitishwa katika mafunzo ya kijeshi kuanzia Goma hadi baadaye wakahamishiwa Bunia jimboni Ituri kwa kuwa viongozi wao waliona kuwa wazazi wanaanza kutafuta watoto wao. 

“Walituhamishia Bunia na baadaye tukapelekwa Rwampara huko tulijenga kambi na kuanza kupatiwa mafunzo ya kijeshi kwa lugha ya kiswahili na kiingereza,” anasema Bwana Mwingwa. 

"Mama alisema 'mtoto wangu kijana ni vema ubakie hapa Goma kwa maana jamaa tuna kilio sana tangu umeenda na tumesikia uliteseka kule ulikoenda,' na kweli tuliteseka kwani chawa zilituingia kwenye sare zetu basi nikaamua kubaki hapa Goma."- Fabien Mwingwa

Kwa mafunzo zaidi walihamishiwa Kisangani katika kambi ya Kapalata huko walikutana na askari wengine wa msituni kutoka kikundi cha Mai Mai. “Mafunzo  yaliendelea na baada ya hapo tulipelekwa uwanja wa vita huko Manono,” anasimulia Bwana Mwingwa. 

Katika  uwanja wa vita anakumbuka vita ilikuwa ni kubwa mno, “kwa sisi ambao tulipona na wengine walipata hata wazimu kwa sababu silaha zilikuwa ni zile nzito nzito kama vile RPG na mabomu makubwa makubwa na mimi ni mtoto. Mama yangu alikuwa ni mjane na angalipenda kuniona tena katika mji wa Goma na alikuwa analia kila wakati.” 

Fabien Mwingwa akiwa ofisi kwake. Yeye ni mpiganaji wa zamani wa msituni na sasa ameajiriwa na MONUSCO, Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC kama askari wa zimamoto.
UN/Eskinder Debebe
Fabien Mwingwa akiwa ofisi kwake. Yeye ni mpiganaji wa zamani wa msituni na sasa ameajiriwa na MONUSCO, Goma jimbo la Kivu Kaskazini nchini DRC kama askari wa zimamoto.

 

Ilikuwaje akarudi Goma? 

Alibahatika kupangwa kurejea Goma pamoja na askari wengine kwa kuwa alikuwa kwenye kikosi cha ulinzi wa kiongozi wao. 

Tulipofika uwanja wa ndege mama yangu mzazi akasikia hiyo habari akanishurutisha  tena na kunisihi ‘ni vema mtoto wangu kijana ni vema ubakie hapa Goma kwa maana jamaa tuna kilio sana tangu umeenda na tumesikia uliteseka kule ulikoenda, “na kweli tuliteseka kwani chawa zilituingia kwenye sare zetu basi nikaamua kubaki hapa Goma.” 

Harakati za kutaka kujisalimisha 

Mwaka 2004, yaani baada ya miaka 6 ya mapigano msituni, Bwana Mwingwa alianza kuona bora aitikie wito wa mama yake mzazi wa kurejea nyumbani. Akiwa Goma akajiunga na kikundi cha kijeshi kwa kuwa alisikia wanaanza kuachilia watu ili warudi uraiani. 

“Nami nikaangalia katika jeshi tuliteseka sana nikiangalia maisha yangu hayakuendelea, hata tunalala nje, fedha kidogo tunatumikia, tunapatia wakubwa viongozi,” anasema Bwana Mwingwa.  

Hatimaye mwezi Julai mwaka 2005 akasikia kuhusu MONUSCO wakati huo ikiitwa MONUC, kitengo cha kuvunja makundi, kupokonya silaha, na kujumuisha wapiganaji uraiani, DDRRR, akaenda kujisalimisha ambapo alipata urahisi wa kurejea uraiani. 

Pichani ni Fabien Mwingwa, yeye alikuwa mpiganaji wa zamani wa msituni nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC lakini alijisalimisha mwaka 2005 na sasa ni mwajiriwa wa ofisi ya MONUSCO mjini Goma.
UN Video
Pichani ni Fabien Mwingwa, yeye alikuwa mpiganaji wa zamani wa msituni nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC lakini alijisalimisha mwaka 2005 na sasa ni mwajiriwa wa ofisi ya MONUSCO mjini Goma.

 

MONUSCO-DDR ni kitengo kilicho chini ya Idara ya Umoja wa Mataifa ya operesheni za ulinzi wa amani na jukumu lao ni kuleta amani kwa kufainikisha kuvunja vikundi na wale wapiganaji wanasaidia kujumuishwa uraiani iwe katika nchi wanamopigana au nchi walikotoka.

Taratibu za kujisalimisha 

Ofisi zilikuwa uwanja wa ndege Goma na akapokelewa akakabidhi silaha pamoja na sare za kijeshi na kupatiwa nyaraka ya kuthibitisha kuwa amesalimisha vifaa hivyo. 
Alikaguliwa pia iwapo alifanya uhalifu nayo ikathibitishwa kuwa hakuwahi kufanya uhalifu wowote. Kisha ofisi nyingine ikathibitisha pia alikuwa mwanajeshi na alipata mafunzo ya kijeshi. 

Baada ya hapo MONUSCO DDRRR iliwapatia mafunzo ya kuweza kujikwamua kimaisha na baada ya mafunzo alipatiwa mtaji na madumu 6 ya mafuta ili afanye biashara ya mafuta. 
Biashara hiyo hakuipenda aliingia kwenye bodaboda ambayo alifanya kwa muda mfupi na ndipo akaajiriwa na ofisi ya ulinzi ya KK Security. 

Ofisi hii ilikuwa ndio mwanzo wa safari ya maisha yake ya ajira za vipindi vifupi ikiwemo MONUSCO iliniajiri kwenye uhandisi na pia udereva. 

Mwaka 2015 akapata taarifa kuwa MONUSCO inasaka mzimamoto msaidizi na kwa kuwa alishawahi kupata mafunzo na kupata cheti, alifanya mtihani na akaajiriwa hadi leo. 
Nashukuru MONUSCO na Umoja wa Mataifa 

Bwana Mwingwa sasa ni mwajiriwa wa MONUSCO Goma, na anatoa shukrani kwa kuwa ofisi hiyo ilisimama naye tangu alipoamua kujisalimisha hadi sasa. Anashukuru Umoja wa Mataifa kwa kumpatia mshahara mzuri na yeye ameweza kujenga nyumba, ameoa ana watoto na wanasoma vizuri. 

Vijana wanaoingia msituni anawaambia nini? 

Tafadhali msiende huko, hakuna faida! Mimi niliteseka, nilipoteza muda, rudini nyumbani, mje msome mfanye mafunzo mbalimbali ya maisha, mnaweza kupata kazi kama mimi na maisha ni mazuri.”