Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ibara nadra yatumiwa na Katibu Mkuu wa UN kutuma ujumbe mzito kwa Baraza la Usalama kuhusu Gaza

Watu wanatafuta mali zao kwenye vifusi katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko Gaza.
© UNRWA/Ashraf Amra
Watu wanatafuta mali zao kwenye vifusi katika kambi ya wakimbizi ya Nuseirat huko Gaza.

Ibara nadra yatumiwa na Katibu Mkuu wa UN kutuma ujumbe mzito kwa Baraza la Usalama kuhusu Gaza

Amani na Usalama

Akitumia ibara ya 99 kutoka katika Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ambayo ni nadra sana kutumia, Katibu Mkuu António Guterres leo Jumatano kwa njia ya barua ametoa wito kwa Baraza la Usalama "kushinikiza kuepusha janga la kibinadamu" huko Gaza na kuungana katika wito wa usitishaji kamili wa mapigano kati ya Israeli na wanamgambo wa Palestina, Hamas. 

Ibara hii ya 99 iliyoko katika Sura ya XV ya Makataba wa Umoja wa Mataifa inasema kwamba mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa "anaweza kulijulisha Baraza la Usalama jambo lolote ambalo kwa maoni yake, linaweza kutishia kudumisha amani na usalama wa kimataifa." 

Katika taarifa kwa waandishi wa habari pamoja, Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric amesema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Bwana Guterres kuhisi kulazimishwa kutumia Ibara ya 99, tangu aingie madarakani mwaka wa 2017. 

Mtoto akitembea katika mitaa ya Deir El-Balah katikati mwa Gaza.
© UNRWA
Mtoto akitembea katika mitaa ya Deir El-Balah katikati mwa Gaza.

'Mateso ya kutisha kwa wanadamu' 

Katika barua yake kwa Rais wa Baraza, Bwana Guterres amesema zaidi ya wiki nane za mapigano kwa ujumla "zimesababisha mateso ya kutisha kwa binadamu, uharibifu wa kimwili na kiwewe cha pamoja kote Israel na eneo la Palestina linalokaliwa kwa mabavu." 

Ameangazia zaidi ya watu 1,200 "waliouawa kikatili" na wanamgambo tarehe 7 Oktoba, ikiwa ni pamoja na watoto 33, na watu 130 bado wanazuiliwa. 

"Lazima waachiliwe mara moja na bila masharti. Idadi za unyanyasaji wa kijinsia wakati wa mashambulio haya ni za kutisha,” mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ameongeza. 

Wakati Israel ikiendelea kuwalenga wapiganaji wa Hamas, Guterres amesema raia katika eneo lote la Ukanda huo wanakabiliwa na hatari kubwa, huku zaidi ya watu 15,000 wakiripotiwa kuuawa, zaidi ya asilimia 40 wakiwa watoto. 

Takriban asilimia 80 ya wananchi wa Gaza wameyakimbia makazi yao, zaidi ya watu milioni 1.1 wakitafuta hifadhi katika makazi ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Palestina (UNRWA).