Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama lapitisha azimio kuhusu Gaza

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijadili hali ya Gaza, kufuatia kupitishwa kwa azimio.
UN News
Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakijadili hali ya Gaza, kufuatia kupitishwa kwa azimio.

Baraza la Usalama lapitisha azimio kuhusu Gaza

Masuala ya UM

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo Novemba 15 limepitisha azimio kuhusu hali ya Gaza likitoa wito wa kufunguliwa kwa vituo vya dharura na vya muda mrefu vya kibinadamu.

Hati hiyo imepita kwa kura 12 za ndio lakini Urusi, Uingereza na Marekani hazikupiga kura. Pendekezo lililoletwa na Malta linataka kuundwa kwa njia za kufikia misaada ya kibinadamu na kutoa wito wa kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas. Pia linatetea ufikiaji kamili, wa haraka, salama na usiozuiliwa wa kibinadamu kwa maeneo ya Gaza.

Kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote

Azimio hilo linazungumzia suala la "kufuata sheria za kimataifa, yaani ulinzi wa raia, hasa watoto, na kuachiliwa mara moja na bila masharti mateka wote wanaozuiliwa na Hamas na makundi mengine, hasa watoto wadogo".

Kabla ya upigaji kura, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema "ana wasiwasi mkubwa" baada ya kupoteza mawasiliano na timu yake katika Hospitali ya Al-Shifa, huko Gaza, kufuatia hatua za jeshi la Israeli katika hospitali hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Dkt. Tedros, akizelezea kama ripoti “zinazoleta wasiwasi” za operesheni hiyo ambayo, kulingana na mashirika ya habari, ilianza Jumanne usiku, saa za Gaza.

Kura

Ili kupitishwa, azimio hili lilikuwa linahitaji kura tisa za kuunga mkono na bila kura ya turufu ya kupinga ambayo ni fursa kwa nchi 5 pekee duniani  kura ya turufu - fursa iliyohifadhiwa kwa wanachama wake wa (China, Marekani, Ufaransa, Uingereza na Urusi).

Marekani na Urusi, ambazo katika wiki zilizopita zilipinga maazimio yaliyokwamisha Baraza la Usalama, zimeamua kutoshiriki katika upigaji kura wa leo, na hivyo kuruhusu azimio hilo kupitishwa. 

Kutokuwepo maneno ya kulaani Hamas katika pendekezo la azimio lililokuwa limeletwa mezani na kutokuwepo kwa usitishaji vita endelevu ndio sababu ambazo Washington na Moscow wametoa zilizosababisha wasipige kura. 

Ufaransa, China, Malta, UAE, Albania, Brazil, Ecuador, Gabon, Ghana, Japan, Msumbiji na Uswizi zimepiga kura ya ndio.