Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 100 za mzozo: Hatuwezi kuruhusu yanayotokea Gaza kuendelea, wala kutokea Lebanon - Guterres

Watoto wakisubiri kugawiwa chakula huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.
© UNICEF/Abed Zagout
Watoto wakisubiri kugawiwa chakula huko Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Siku 100 za mzozo: Hatuwezi kuruhusu yanayotokea Gaza kuendelea, wala kutokea Lebanon - Guterres

Amani na Usalama

Siku 100 tangu kuanza kwa mzozo wa Israel na Palestina, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres leo Januari 15 akizungumza na wanahabari jijini New York Manreakni ametaka "kuachiliwa mara moja na bila masharti kwa mateka wote. "Pia akiongeza kusema mashambulizi dhidi ya Gaza yaliyotekelezwa na vikosi vya Israeli katika siku hizi 100 yamesababisha uharibifu mkubwa na viwango vya mauaji ya raia kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea katika miaka ya uongozi wake kama Katibu Mkuu."

Guterres amesema mateka "lazima watendewe ubinadamu na kuruhusiwa kupokea wageni na usaidizi kutoka kwa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu," na "matukio ya unyanyasaji wa kijinsia uliofanywa na Hamas na wengine mnamo Oktoba 7 lazima yachunguzwe kwa ukali na kufunguliwa mashtaka."

"Hakuna kitu kinachoweza kuhalalisha mauaji ya kimakusudi, kujeruhi na utekaji nyara wa raia - au kurusha roketi kuelkuwalenga raia."

Akibainisha kwamba "wengi" wa waliouawa huko Gaza ni wanawake na watoto, Guterres amesema, "hakuna chochote kinachoweza kuhalalisha adhabu ya pamoja ya watu wa Palestina."

Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu Mashariki ya Kati.
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu António Guterres akihutubia waandishi wa habari kuhusu Mashariki ya Kati.

Katibu Mkuu pia ameonya kuhusu athari za kikanda za mzozo huo akisema, "kiini cha mvutano katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa unazidi kupamba moto na kuongezeka kwa ghasia na kusababisha janga kubwa la kifedha kwa Mamlaka ya Palestina. Mvutano pia uko juu sana katika Bahari Nyekundu na kwingineko - na inaweza kuwa vigumu kuudhibiti hivi karibuni.

Guterres ameonesha "wasiwasi mkubwa" kuhusu kurushiana risasi kila siku katika eneo la mpaka ‘Blue Line’ katika ya Israel na Palestina, hali ambayo ni "hatari ya kuchochea kuongezeka kwa kiwango kikubwa kati ya Israeli na Lebanon na kuathiri pakubwa utulivu wa kikanda."

Ametoa wito kwa wahusika "kuacha kucheza na moto katika eneo la ‘Blue Line’, kupunguza makali, na kumaliza uhasama kwa mujibu wa Azimio 1701 la Baraza la Usalama.

Katibu Mkuu amesema, "hatuwezi kuona huko Lebanon kile tunachokiona huko Gaza. Na hatuwezi kuruhusu kile ambacho kimekuwa kikitokea Gaza kuendelea."

Guterres ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano ya kibinadamu pamoja na ufikiaji wa mahitaji ya kibinadamu wa haraka, salama, usiozuiliwa, uliopanuliwa na endelevu ndani na kote Gaza.