Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake wa Afrika wako msitari wa mbele katika ulinzi wa amani UN

Maafisa wa kikosi cha polisi wanawake kutoka Rwanda wakitoa usaidizi kwa kuwatembelea maafisa wenzao waliokwenda kwenye kambi kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na watoto wanaoishi kwenye kituo cha ulinzi wa raia Juba , Sudan Kusini
Picha na UNMISS
Maafisa wa kikosi cha polisi wanawake kutoka Rwanda wakitoa usaidizi kwa kuwatembelea maafisa wenzao waliokwenda kwenye kambi kwa ajili ya kuwasaidia wanawake na watoto wanaoishi kwenye kituo cha ulinzi wa raia Juba , Sudan Kusini

Wanawake wa Afrika wako msitari wa mbele katika ulinzi wa amani UN

Amani na Usalama

Kuelekea mkutano wa ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa ngazi ya mawaziri utakaofanyika huko Accra Ghana tarehe 5 hadi 6 Desemba, tunaangazia jukumu la lazima la walinzi wa amani wanawake kutoka Afrika ambao wanakaidi kanuni za kijinsia ndani ya mifumo ya usalama ambayo kwa hulka imekuwa mfumo dume ili kuleta amani na usalama kwa jamii zinazojikwamua kutoka kwenye vita kuelekea katika amani. 

Kwa zaidi ya mwaka mmoja, kikundi cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Ghana wakiongozwa na Kapteni Esinam Baah mara kwa mara wamekuwa wakishika doria kwenye "blue line" au mstari wa kuweka mipaka kati ya Lebanon na Israeli, na kutembelea vitongoji katika eneo hilo, kuangalia familia za wenyeji na kuhakikisha kuwa walikuwa salama.

Mwaka 2022, Baah alikuwa mmoja wa walinda amani wanawake 173 wa Ghana waliohudumu katika operesheni ya muda ya Umoja wa Mataifa nchini Lebanon. Pia alikuwa mmoja wa walinzi wa amani wanawake 6,200 waliovalia sare za Umoja wa Mataifa wanajeshi na polisi wanaohudumu katika operesheni 12 za kulinda amani duniani ambazo nyingi ziko Afrika (6) na Mashariki ya Kati (3). Wanawake hawa wanaonekana kuwa kinara wa matumaini na ulinzi kwa mamilioni ya raia, wengi wao wakiwa wanawake na wasichana, ambao wanahangaika kujilinda huku wakisaidia kujenga upya maisha na jamii zao baada ya vita.

Kapteni Baah (kulia) akitembelea familia ya Walebanon Kusini mwa Lebanon.
UNIFIL
Kapteni Baah (kulia) akitembelea familia ya Walebanon Kusini mwa Lebanon.

Baah anasema “Kuna baadhi ya watu mjini hawaridhii hali ya mwanaume asiyejulikana kuongea na wanawake wao kwa hiyo, kwa sababu mimi ni mwanamke nina uwezo wa kumkaribia mwanamke yeyote katika mji wowote kwa sababu wananiona mimi ni mwanamke na mimi ni mwanamke mwenzao hivyo si tishio.”

Usawa wa kijinsia katika ulinzi wa amani, hasa miongoni mwa viongozi wake na wafanyakazi wanaovaa sare za Umoja wa Mataifa, umekuwa kipaumbele kwa Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu. 

Shirika hilo ambalo linategemea nchi wanachama wake kutoa vikosi vya kijeshi na polisi, limeanzisha mipango kadhaa kwa miaka mingi, ikiwa ni pamoja na kuzihimiza na kuzitia motisha nchi zinazochangia wanajeshi na polisi kupeleka askari wengi zaidi wanawake wa kulinda amani.

"Dunia itakuwa mahali pazuri na usawa wa kijinsia. Kwa hivyo, tunapaswa kuendelea kupinga dhana potofu za kijinsia, kutoa wito kutokomeza suala la ubaguzi, kutozingatia upendeleo na kutafuta ushirikishwaji,” anasema Faustina Anokye kutoka Ghana ambaye ni Naibu Kamanda wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kura ya Maoni katika Sahara Magharibi, kuhusu njia muhimu za kuondokana na vikwazo vya kijinsia.

Kwa miaka mingi, maendeleo kadhaa yamefanyika. Kati ya 1957 na 1989, kulikuwa na wanawake 20 tu waliovaa sare za Umoja wa Mataifa katika ulinzi wa amani. 

Kufikia Septemba 2023, kulikuwa na wanawake 6,200. Lakini maendeleo yamekuwa ya polepole na ya chini sana miongoni mwa vikosi vya kijeshi. 

Kati ya zaidi ya askari 70,000 wanaovalia sare za kulinda amani, wakiwemo zaidi ya wanajeshi 62,000, chini ya asilimia 10 ndio wanawake.

Zaidi ya nusu ya wanawake hawa walinda amani wanatoka Afrika. Miongoni mwa nchi zaidi ya 120 zinazochangia askari na polisi, Misri, Ethiopia, Ghana, Rwanda, Senegal, Afrika Kusini na Zambia ni baadhi ya wachangiaji wakubwa barani Afrika wa walinda amani wanawake wanaovaa sare za Umoja wa Mataifa leo hii.

Takwinu za wanawake katika ulinzi wa amani mwaka 2022. Wanawake 6.6% pekee wako katika kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani, 15.6% pekee wa polisi wa Umoja wa Mataifa (UNPOL) ni wanawake. Kadi ya kati ikionyesha nchi tano za juu zinazochangia we…
United Nations
Takwinu za wanawake katika ulinzi wa amani mwaka 2022. Wanawake 6.6% pekee wako katika kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani, 15.6% pekee wa polisi wa Umoja wa Mataifa (UNPOL) ni wanawake. Kadi ya kati ikionyesha nchi tano za juu zinazochangia wengi wa walinda amani wanawake.

Waanzilishi na wafuatiliaji

"Pamoja na waanzilishi wengine wote wanawake, tuna jukumu la kubeba mwenge na kuondokana na dhana potofu za kijinsia, chuki na vikwazo dhidi ya wanawake katika uwanja wa urekebishaji na usalama," anasema Téné Maïmouna Zoungrana, afisa wa magereza kutoka Burkina Faso ambaye alihudumu katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA).

Zoungrana alitunukiwa Tuzo ya kwanza kabisa la Umoja wa Mataifa kwa maafisa wanawake wa Haki na Urekebishaji mwaka wa 2022. 

Akifanya kazi chini ya mamlaka ya MINUSCA kusaidia kujenga uwezo wa kitaifa wa kudumisha sheria na utulivu, alikuwa na mchango mkubwa katika kuunda timu ya uingiliaji kati wa haraka ya wanawake wote, kuajiri na kutoa mafunzo kwa maafisa wa magereza wa ndani katika gereza kuu la Ngaragba linalochukuliwa kuwa jela kubwa na yenye sifa mbaya zaidi huko Bangui.

Téné Maimouna Zoungrana ni Afisa wa marekebisho kutoka Burkina Faso anayehudumu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA).
MINUSCA/Hervé Serefio
Téné Maimouna Zoungrana ni Afisa wa marekebisho kutoka Burkina Faso anayehudumu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA).

"Katika mazingira yangu ya kitaaluma, nyanja ya usalama, wanawake mara nyingi huwekwa nafasi ya pili au hata kupuuzwa, kwa sababu ya mitazamo potofu kwamba wanaume wanafaa zaidi kwa kazi hiyo. Nilikuwa na ujasiri na nguvu, na wito, kuvunja vizuizi na kujikita kwa ujasiri katika uwanja huu, "anaongeza Zoungrana.

Fursa zenye vikwazo na upendeleo za kutumwa, mitazamo ya kijinsia kuhusu jukumu la wanawake, ukosefu wa sera zinazofaa familia, na ukosefu wa wanawake katika jeshi la kitaifa na vikosi vya polisi ni baadhi ya sababu za kukosekana kwa usawa wa kijinsia, kulingana na Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Usawa wa Kijinsia ambao ulizinduliwa mnamo 2018.

Walinda amani wa kike kama Zoungrana ni mfano wa kuigwa kwa wanawake na wasichana wengi. 

Kazi yake inasaidia kuvunja vizuizi vya kijadi vya jinsia, na kuwahamasisha na kuwawezesha wanawake wa eneo hilo kuchukua majukumu yasiyo ya kitamaduni yanayohodhiwa na wanaume katika sekta ya usalama kuboresha ufikiaji wao wa kazi za maana na mchango wao kwa jamii, na kusaidia kujenga imani yao.

Walinzi wa amani pia wana jukumu muhimu katika kuweka programu za uhamasishaji zinazozingatia jinsia zilizoundwa mahsusi kukidhi mahitaji ya kipekee ya wanawake na wasichana. 

Mshauri wa kinsia wa kijeshi Steplyne Nyaboga kutoka Kenya, ambaye alishinda tuzo ya Mtetezi Bora wa Jinsia wa Kijeshi wa Umoja wa Mataifa mwaka 2020, alikuwa mmoja wa walinda amani kama hao. 

Alitoa mafunzo kwa kikosi cha kijeshi cha zaidi ya wanajeshi 15,000, waliohudumu katika Misheni ya Umoja wa Mataifa huko Darfur (sasa imefungwa), kuhusu mienendo ya kijinsia na kuimarisha ushirikiano wa operesheni hiyo na wanawake wa Darfur.

"Ulinzi wa amani ni suala la kibinadamu, kuwaweka wanawake na wasichana kuwa kitovu cha juhudi na wasiwasi wetu kutatusaidia kulinda raia vyema na kujenga amani endelevu," anasema Nyaboga.

Kwa miongo kadhaa iliyopita, kanuni na mikataba ya kimataifa imepitishwa kuwajumuisha wanawake katika michakato ya amani ili kuhakikisha kuwa wanawake wanawakilishwa katika mazungumzo ya amani, kusaidia mashiŕika ya kiraia ya wanawake na kushughulikia usawa wa kijinsia miongoni mwa watoa maamuzi ambao unaendelea kuwepo leo.

Mwaka 1995, Mkutano wa Nne wa Dunia wa Wanawake huko Beijing, Uchina, ulirasimisha hitaji la dharura la kushughulikia uwezeshaji wa wanawake na ushirikishwaji katika utatuzi wa migogoro kati ya vipaumbele vingine, kuandaa njia ya kupitishwa kwa azimio la 1325 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Wanawake, Amani na Usalama mwaka 2000 ambalo lilikubali na kusisitiza umuhimu wa michango ya wanawake katika kuzuia na kutatua migogoro, kulinda amani na kujenga amani.

Hivi karibuni zaidi mwaka 2019, Mfuko wa Elise Initiative, ulioandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake UN Women, ulianzishwa ili kuzipa nchi motisha za kifedha na msaada ili kuongeza idadi ya walinzi wa amani wanawake wanaovalia sare za Umoja wa Mataifa.

Kufikia 2022, ulikuwa umewekeza dola milioni 17 kusaidia taasisi 21 za usalama za kitaifa, zikiwemo nchini Uganda, Senegal na Ghana, na oparesheni mbili za ulinzi wa amani kama vile operesheni ya Umoja wa Mataifa ya kuimarisha utulivu wa mipaka mingi nchini Mali.

Maafisa wa UNPOL wa Senegal na Nigeria wakihudhuria mafunzo ya kudhibiti umati pamoja na Maafisa wa Polisi wa Mali katika chuo cha polisi huko Bamako, Mali.
MINUSMA/Marco Dormino
Maafisa wa UNPOL wa Senegal na Nigeria wakihudhuria mafunzo ya kudhibiti umati pamoja na Maafisa wa Polisi wa Mali katika chuo cha polisi huko Bamako, Mali.

“Sasa ni wakati wa kutekeleza ahadi hizo na kugeuza mazungumzo kuwa vitendo. Tunahitaji kuleta sauti za wanawake kwenye meza ya mazungumzo katika michakato ya kisiasa na amani. Ni lazima tuwawezeshe kwa kuwajengea uwezo na kuwapa usaidizi wanaohitaji ili kusikilizwa. Hili ni jambo la lazima katika kudumisha amani,” anasema Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Afrika Martha Ama Akyaa Pobee.

Kimsingi, kazi ya lazima ya walinda amani wanawake inaendelea kuleta athari chanya kubwa hasa katika maisha ya wanawake na wasichana wa eneo hilo. Jackline Urujeni, ambaye aliongoza kikosi cha maafisa wa polisi 160 wa Rwanda, nusu yao wakiwa wanawake, katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS, anakabiliwa na maswali mengi kuhusu kazi yake katika muundo wa jadi wa usalama wa mfumo dume.

"Wanawake wa hapa Sudan Kusini wameniuliza maswali mengi, haswa wanapoelewa kuwa mimi ni afisa mkuu wa kundi kubwa la maafisa wa polisi. Wananiuliza: Unawezaje kuwa kamanda? Huna wanaume katika nchi yako?" anasema Urujeni, ambaye anaamini kwamba walinda amani wanawake “wana mchango mkubwa katika kuwatia moyo wasichana na wanawake.”

"Niligundua kuwa wasichana na wanawake hapa polepole wanakuwa na ufahamu wa haki zao za kuwa vile wanavyotaka kuwa. Wanaelewa kuwa wasichana hawapo ili kuolewa na kupata watoto. Tunafungua macho yao kwa uwezekano mpya, kwa chaguzi mpya ambazo wanapaswa kuruhusiwa kuzifanya.