Doreen Malambo wa UNMISS ndiye mshindi wa tuzo ya UN ya polisi wa mwaka 2020
Doreen Malambo wa UNMISS ndiye mshindi wa tuzo ya UN ya polisi wa mwaka 2020
Inspekta mkuu Doreen Malambo ambaye ni mshauri wa masuala ya kijinsia kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) ameshinda tuzo ya mwaka ya Umoja wa Mataifa ya afisa wa pilisi kwamwaka huu 2020 kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kusaidia vikundi vilivyo hatarini kama wanawake, wasichana , Watoto na watu wenye ulemavu.
Bi Malambo ambaye ni raia wa Zambia ambaye alitumia miaka 24 kutoa huduma katika jeshi la polisi la nchi yake , alipelekwa kwenye mpango wa Umoja wa Mataifa wa UNMISS tangu mwaka 2019 ambapo jukumu lake linajumuisha kushiriki katika mashauriano ya kijamii na uhamasishaji kuhusu kuzuia na kupunguza uhalifu.
Athari ya haraka ya kazi yake
Katika majukumu ya awali na Umoja wa Mataifa inspekta mkuu Malambo alifanyakazi katika mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Liberia (UNMIL) kuanzia mwaka 2008 hadi 2009 ambapo aliisaidia polisi ya kitaifa ya Liberia katika kuzuia na kuchunguza masuala ya ukatili wa kingono na kijinsia na unyanyasaji majumbani.
Muda mfupi baada ya kuwasili Sudan Kusini Bi. Malambo haraka alileta athari chanya akisaka mshikamano na mashirika ya Umoja wa Mataifa na kuzaa ushirika bunifu na wanaume katika ngazi ya mashinani ambao unalenga kuboresha haki za wanawake na wasichana.
Akifanyakazi na shirika la idadi ya watu duniani la Umoja wa Mataifa (UNFPA) alihusika katika kuanzisha mpango wa “Simamia haki za wanawake na wasichana” ambao umesaidia kupunguza na kuzuia uhalifu wa ukatili wa kingono na kijinsia nchini Sudan Kusini.
Kama sehemu ya mradi huu Bi. Malambo aliunde mtandao wa vikundi vinavyoongozwa na maafisa wa polisi wa kiume ili kushirikisha wanaume wengine katika jamii kusambaza taarifa na kuchagiza ulinzi na maendeleo ya haki za wanawake na wasichana. Pia amewaunga mkono polisi wenzake katika kuanzisha mitandao ya wanawake.
“Kujua kwamba ninaleta mabadiliko kwa kufanya kazi kuwawezesha wanawake na kukuza ujumuishwaji wao na ushiriki katika jamii kunanihamasisha” amesema inspekta mkuu Malambo na kuongeza kuwa “Uwezeshaji wa wanawake ni ufunguo wa kuongeza mwonekano wa maslahi yao, hofu zao, mahitaji na michango yao.”
Polisi bora wa UN
Tuzo hiyo itatolewa na Jean-Pierre Lacroix mkuu wa operesheni za ulinzi wa mani za Umoja wa Mataifa , katika hafla itakayofanyika tarehe 3 Novemba mwaka huu.
Katika taarifa iliyotolewa leo Bwana. Lacroix amesema “Bi. Malambo ni mfano bora wa polisi wa Umoja wa Mataifa kupitia mawazo yake na vitendo vyake. Ushiriki mkubwa wa wanawake katika ulinzi wa amani unatuma ujumbe mzito kwa watu tunaowahudumia. Ujumbe huu unakuwa wakati maafisa wa polisi wanawake kama inspekta mkuu Malambo wanapoongoza kuwawezesha na kuwalinda wengine n ahata zaidi katika mazingira ya majanga”