Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi moja ya sababu za ongezeko la Idadi ya wagonjwa wa malaria duniani - WHO

Katika maeneo ya mashini nchini Uganda, mama anamlaza mtoto wake wa mwaka mmoja ndani ya chandarua.
© UNICEF/Maria Wamala
Katika maeneo ya mashini nchini Uganda, mama anamlaza mtoto wake wa mwaka mmoja ndani ya chandarua.

Mabadiliko ya tabianchi moja ya sababu za ongezeko la Idadi ya wagonjwa wa malaria duniani - WHO

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO limesema katikia ripoti yake mpya iliyotolewa leo kwamba licha ya hatua kubwa zilizopigwa katika kupanua wigo wa kupata vyandarua vya mbu vyenye dawa pamoja dawa za kusaidia kuzuia malaria kwa watoto na kina mama wajawazito, watu wengi wamekuwa wakiugua malaria. 

Kwa mujibu wa shirika hilo mwaka 2022 kulikuwa na wagonjwa wa malaria milioni 249 duniani kote ikiwa ni wagonja milioni 16 zaidi ya ilivyokuwa kabla ya janga la coronavirus">COVID-19 ambapo wagonja mwaka 2019 walikuwa ni milioni 233.

WHO inasema mbali na usumbufu uliosababishwa na janga la COVID-19, hatua za kupambana na malaria duniani zimekabiliwa na vitisho vinavyoongezeka, kama vile usugu dhidi ya dawa na wadudu, migogoro ya kibinadamu, vikwazo vya rasilimali, athari za mabadiliko ya tabianchi na ucheleweshaji wa utekelezaji wa programu haswa katika nchi zenye kiwango kikubwa cha mzigo wa ugonjwa huo.

Malaria na magonjwa mengine yanaongezeka baada ya mafuriko katika jimbo la Sindh, Pakistan.
© UNICEF/Saiyna Bashir
Malaria na magonjwa mengine yanaongezeka baada ya mafuriko katika jimbo la Sindh, Pakistan.

Kuhusu ripoti ya Malaria 2023

Kwa mujibu wa WHO ripoti ya dunia ya malaria ya mwaka 2023 inaangazia uhusiano kati ya mabadiliko ya tabianchi na malaria. 

Inasema mabadiliko ya halijoto, unyevunyevu na mvua yanaweza kuathiri tabia na uhai wa mbu aina ya Anopheles anayeambukiza malaria. 

Matukio mabaya ya hali ya hewa kama vile mawimbi ya joto na mafuriko, yanaweza pia kuathiri moja kwa moja maambukizi na mzigo wa magonjwa. Mafuriko makubwa nchini Pakistan mwaka 2022, kwa mfano, yamesababisha ongezeko la mara tano la visa vya malaria nchini humo.

Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus  amesema "Kubadilika kwa hali ya hewa kunaleta hatari kubwa kwa mapambano dhidi ya malaria, haswa katika maeneo hatarishi. Makabiliano endelevu na sugu ya malaria yanahitajika sasa kuliko wakati mwingine wowote, pamoja na hatua za haraka za kupunguza kasi ya ongezeko la joto duniani na kupunguza madhara yake,” 

Ameongeza kuwa takwimu kuhusu athari za muda mrefu za mabadiliko ya tabianchi katika maambukizi ya malaria ni chache. 

Hata hivyo, mwelekeo na ukubwa wa athari zozote zinaweza kutofautiana katika mifumo ya kijamii na kiikolojia, ndani na miongoni mwa nchi.

Mtoto akichunguzwa kama ana malaria jimbo la Adamawa, Nigeria
© UNICEF/Andrew Esiebo
Mtoto akichunguzwa kama ana malaria jimbo la Adamawa, Nigeria

Mzigo wa malaria na hatua zinazochukuliwa duniani

WHO inasema janga la COVID-19 lilitatiza huduma za malaria kwa kiasi kikubwa, na kusababisha kuongezeka kwa matukio na viwango vya vifo, na kuzidisha changamoto ambazo tayari zimekwama dhidi ya ugonjwa huo.

Sirika hilo limeainisha kwamba “Ulimwenguni kote kulikuwa na wagonjwa zaidi ya milioni tano wa malaria mwaka 2022 na nchi tano zilibeba mzigo mkubwa wa ongezeko hili. Pakistani ilipata ongezeko kubwa zaidi, ikiwa na takriban kesi milioni 2.6 mwaka wa 2022 ikilinganishwa na 500 000 mwaka wa 2021. Ongezeko kubwa lilijitokeza pia Ethiopia, Nigeria, Papua New Guinea na Uganda.”

Wakati huo huo, limesema katika nchi 11 zinazobeba mzigo mkubwa zaidi wa ugonjwa wa malaria, viwango vya maambukizi mapya na vifo vimepungua kufuatia ongezeko la awali katika mwaka wa kwanza wa janga hilo. 

Nchi hizi, zikiungwa mkono na WHO "Mzigo mkubwa wa athari zilishuhudia visa vya malaria milioni 167 na vifo 426,000 mwaka wa 2022.”

Kwa kuzingatia mwelekeo wa sasa, hatua za kuelekea malengo ya 2025 za mkakati wa kimataifa wa malaria wa WHO zinakwenda kombo kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi mkuu wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema "Ni muhimu kutambua wingi wa vitisho vinavyozuia jitihada zetu za kukabiliana na malaria”

Amesema “kubadilika kwa hali ya hewa kunaleta hatari kubwa, lakini lazima pia tukabiliane na changamoto kama vile upatikanaji mdogo wa huduma za afya, migogoro inayoendelea na dharura, athari zinazoendelea za COVID-19 katika utoaji wa huduma, ufadhili usiofaa na kutotekelezwa kwa usawa kwa misaada yetu mikubwa ya malaria. Ili kusonga mbele kuelekea mustakabali usio na malaria, tunahitaji juhudi za pamoja ili kukabiliana na vitishio hivi mbalimbali hatua ambazo zinakuza uvumbuzi, uhamasishaji wa rasilimali na mikakati shirikishi.”

Mhudumu wa afya nchini Kenya akiwa ameshikilia chupa za chanjo ya malaria itakayotolewa katika kampeni ya chanjo.
© UNICEF/Washington Sigu
Mhudumu wa afya nchini Kenya akiwa ameshikilia chupa za chanjo ya malaria itakayotolewa katika kampeni ya chanjo.

Nini kinahitajika sasa

Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mradi wa majaribio wa kwanza kabisa wa chanjo ya malaria katika nchi tatu za Afrika WHO inasema ni umuhimu mkubwa katika mapambano dhidi ya malaria unahitajika, pamoja na kuongezeka kwa rasilimali, kuimarishwa kwa utashi wa kisiasa, mikakati inayotokana na takwimu na zana za ubunifu. 

Pia ubunifu unapaswa kuzingatia maendeleo ya bidhaa bora zaidi, naza gharama nafuu.

Kwa mujibu wa WHO Tishio lililoongezwa la mabadiliko ya tabianchi linataka hatua endelevu kwa sugu ya malaria ambazo zinaendana na juhudi za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Pia limesisitiza kuwa “Ushirikiano wa jamii nzima ni muhimu ili kujenga mbinu jumuishi.”