Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa dunia na wadau washikamana kutaka fursa sawa ya huduma za afya kwa wote: UNITAID

Phiona anafanya kazi katika kituo cha afya nchini Uganda kama mwanaharaki wa rika ya akina mama, anasaidia kutoa mafunzo na kusaidia akina mama kujifungua watoto wasio na VVU.
© UNICEF/Karin Schermbrucker
Phiona anafanya kazi katika kituo cha afya nchini Uganda kama mwanaharaki wa rika ya akina mama, anasaidia kutoa mafunzo na kusaidia akina mama kujifungua watoto wasio na VVU.

Viongozi wa dunia na wadau washikamana kutaka fursa sawa ya huduma za afya kwa wote: UNITAID

Afya

Wakati wa mkutano mkuu wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa wa mwaka huu, viongozi wa dunia, wadau wa afya na wawakilishi wa jamii wanaungana na shirika la kufanikisha upatikanaji wa dawa na tiba kwa gharama nafuu UNITAID, kutoa wito wa upatikanaji wa haraka na usawa zaidi wa bidhaa za afya zinazookoa maisha ili kuendeleza mchakato wa kupambana na changamoto kubwa zaidi za leo za afya, ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi ya mama na mtoto, kuzuia majanga, kujiandaa na hatyua za kukabiliana na majanga, na virusi vya ukimwi VVU, kifua kikuu na malaria.

UNITAID inasema mamilioni ya watu katika nchi za kipato cha chini na cha kati wanakufa kila mwaka kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika na yanayoweza kutibika kwa sababu hawawezi kupata bidhaa za kuokoa maisha wanazohitaji. 

Kama ulimwengu ulivyoshuhudia wakati wa janga la COVID-19, vipimo, matibabu na zana mara nyingi hazipatikani, hazinunuliki au hufika polepole sana kwa watu wanaozihitaji zaidi. 

Unitaid iliundwa ili kushughulikia ukosefu huu wa usawa, ikifanya kazi na washirika kufanya bidhaa za afya zinazookoa maisha zipatikane haraka, ziwe na usawa na za gharama nafuu.

Lazima tuchukue hatua haraka kukabili changamoto

"Ili kushinda changamoto za leo za kiafya, lazima tusonge mbele haraka, na tuwe wabunifu zaidi kuliko hapo awali limesema shirika hilo.”

Ni lazima tubadilike ikiwa tunataka kuzuia wajawazito na watoto wachanga kufa kwa kukosa matibabu rahisi kama vile oksijeni ya kimatibabu, na hatimaye kukomesha milipuko ya VVU, kifua kikuu na malaria. 

“UNITAID inaongoza kwa kutafuta bidhaa bora zaidi za afya na suluhisho za kushughulikia changamoto zinazoturudisha nyuma. 

Hii ndiyo sababu Ufaransa inajivunia kuwa mmoja wa wafuasi waanzilishi wa UNITAID, "Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema.

Tangu UNITAID ilipoundwa mwaka wa 2006, imesaidia maendeleo ya haraka na kuidhinishwa kwa zaidi ya bidhaa 100 za afya ambazo sasa zinachukuliwa kuwa ni kiwango cha juu cha kupambana na VVU, kifua kikuu na malaria, kuboresha afya ya kina mama na watoto, na kuimarisha maandalizi na kukabiliana na mjanga. Pamoja na washirika wame UNITAID, imesaidia kupunguza bei za vipimo vya kuokoa maisha, matibabu na zana na kuongeza ufikiaji kwa watu wanaohitaji zaidi.

Ili kusaidia kukabiliana na changamoto hizo wakfu wa Bill na Melinda Gates leo umetangaza utaongeza mara mbili msaada wake kwa UNITAID na kufikia dola milioni 100 katika miaka 5 ijayo.

Rais wa Ufanrasa ameupongeza wakfu huo wa Bill na Melinda Gates kwa uamuzi wao wa kuongeza mara mbili msaada wa kifedha kwa UNITAID.

Pia wiki hii serikali za Ureno na Hispania nazo zimetangaza msaada mpya kwa UNITAID.