Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tukiadhimisha siku ya Malaria, hebu tushikamane kuelekea ulimwengu usio na janga hilo:WHO 

Wasichana wakiwa wameketi chini ya neti kwa ajili ya kuzuia mbu, Bienythian, Sudan Kusini.
© UNICEF/Mark Naftalin
Wasichana wakiwa wameketi chini ya neti kwa ajili ya kuzuia mbu, Bienythian, Sudan Kusini.

Tukiadhimisha siku ya Malaria, hebu tushikamane kuelekea ulimwengu usio na janga hilo:WHO 

Afya

Katika kuadhimisha siku ya malaria duniani, hii leo afisa wa shirika la afya duniani WHO amesema kwamba licha ya janga la COVID-19, mwaka uliopita umeshuhudia "mafanikio muhimu katika kuzuia na kudhibiti malaria." 

Dkt. Matshidiso Moeti, ambaye ni mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika ameyasema hayo akizungumzia chanjo ya malaria  na kuongeza kuwa "Mwishoni mwa mwaka jana, shirika la afya Ulimwenguni lilitoa mapendekezo ya kihistoria kuhusu matumizi ya chanjo ya kwanza ya malaria ya RTS,S dhidi ya ugonjwa huo." 

Ameongeza kuwa chanjo hii "itatumika kuzuia malaria miongoni mwa watoto wenye umri wa miezi sita hadi miaka mitano, ambao wanaishi katika hali ya wastani hadi ya juu ya maambukizi ya ugonjwa huo." 

Tuchukue hatua kwa busara 

Siku ya Malaria duniani inayoadhimishwa 25 Aprili kila mwaka imejitolea kuelekeza umakini wa kimataifa juu ya magonjwa ya kuambukiza yanayoenezwa na mbu na athari zake mbaya, haswa katika ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.  

Dkt.Moeti anasema mwaka huu unaambatana na wito wake wa kuongeza kasi ya uvumbuzi na kupeleka zana mpya za kupambana na malaria, huku akitetea upatikanaji sawa wa kinga na matibabu katika muktadha wa kujenga mnepo wa mifumo ya afya. 

"Wakati huu ni muhimu kwa maendeleo ya msingi katika kutengeneza zana mpya za kukabiliana na ugonjwa wa malaria, na uwezo wa kuokoa mamilioni ya maisha ya watu, kwani vifaa kwa sasa ni vichache," amesema. 

Kwa hivyo, ni muhimu kuhakikisha kuwa dozi zinazopatikana hutumiwa kuwafikia walio athirika zaidi na wale walio hatarini zaidi. 

Tishio kubwa 

Kwa mujibu wa WHO malaria inasalia kuwa changamoto kubwa ya afya ya umma na maendeleo, kwa mujibu wa WHO. 

Mwaka jana, takriban asilimia 95 ya visa vinavyokadiriwa kufikia milioni 228 vya malaria vilitokea katika kanda ya WHO ya Afrika, huku vifo 602,020 vikiripotiwa. 

Inaelezwa kuwa, sita kati ya nchi zilizoathiriwa zaidi zinachangia hadi asilimia 55 ya visa vyote vya malaria ulimwenguni na asilimia 50 ya vifo vyote vya ugonjwa huo. 

"Pamoja na kudorora kwa maendeleo katika kupunguza visa na vifo vya malaria, na kukatika kwa huduma za afya kutokana na janga la COVID-19, bado tuko mbele sana kuliko tulivyokuwa mwaka 2000. Tunahitaji kuamsha kasi hii na kuendeleza mchakato," amesema afisa huyo wa Umoja wa Mataifa. 

Mkakati wa kutokomeza janga hilo 

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la kufanikisha upatikanaji wa dawa za tiba kwa gharama nafuu UNITAID linaojikita katika kutafuta suluhu za kibunifu za kuzuia, kutambua na kutibu magonjwa kwa haraka zaidi katika nchi za kipato cha kati na cha chini, limesema kuwa zaidi ya theluthi mbili ya vifo vinavyotokana na malaria hutokea miongoni mwa watoto wa umri wa chini ya miaka mitano hususan barani Afrika. 

Ikifadhiliwa kwa pamoja na UNITAID, mfuko wa kimataifa na muungano wa chanjo GAVI, chanjo ya kwanza ya malaria duniani inatolewa kwa watoto kama sehemu ya mkakati wa kina wa kuhakikisha kinga dhidi ya ugonjwa huo. 

WHO inasema udhibiti wa wadudu, ambao unalenga mbu wanaoeneza magonjwa, ni sehemu muhimu na yenye ufanisi mkubwa katika mikakati ya kutokomeza malaria. 

Kupitia uwekezaji katika vyandarua vyenye dawa ambavyo vinapambana na ongezeko la mbu na dawa za kufukuza wadudu, na kwa kutibu watu na mifugo kwa dawa zinazoua mbu wanaowauma, UNITAID inasukuma mchakato wa kuelekea kutengeneza zana mpya na madhubuti. 

Malengo yamewekwa 

Katika kufanya kazi ili kuboresha uchunguzi na matibabu ya malaria ya Plasmodium vivax aina ya malaria inayojulikana zaidi nje ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, UNITAID inasaidia kuboresha huduma kwa watu katika nchi za Asia Pacific na Amerika Kusini. 

Mkakati wa kimataifa wa malaria wa WHO unatoa wito wa kupunguzwa kwa asilimia 90 kwa visa na vifo duniani kote ifikapo mwaka 2030, lengo ambalo linahitaji uwekezaji wa haraka ili kubaini na kupeleka ubunifu muhimu wa kupambana na janga hilo kwa lengo la kulinda watu kila mahali dhidi ya malaria. 

Hii inahitaji kuzingatia utafiti, uthibitishaji wa matumizi bora ya rasilimali na matokeo yanayoweza kupimika, Kupambana na usugu wa dawa na wadudu, Kuzingatia shida mpya zinazoonekana katika eneo hilo, ambazo ni ngumu kugundua na kutibu. 

Dhamira ya kutokomeza malaria 

Dkt. Moeti amesema siku ya malaria duniani ni siku ya "kufufua upya dhamira ya kisiasa na kuhimiza kuendelea kwa uwekezaji katika kuzuia na kudhibiti malaria." 

Ametoa wito kwa nchi na jamii zilizoathirika na ugonjwa wa malaria kushirikiana kwa karibu na wadau wa maendeleo ili kutokomeza ugonjwa huo sambamba na kuchangia katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu SDG’s. 

"Mimi mwenyewe, na ofisi ya WHO ya Kanda ya Afrika, tunaendelea kujitolea kikamilifu katika mapambano dhidi ya malaria," amesema. 

Amesisitiza kuwa "tunaweza kuondokana na changamoto hii ikiwa tutashirikiana kwa karibu na serikali, washirika na jumuiya mbalimbali ili kufikia Afrika huru isiyo na malaria."