Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mfumo wa chakula Gaza umesambaratika kabisa: WFP

Palestina. Usambazaji wa mkate wa WFP katika shule ya UNRWA ambayo ni makazi maalum wakati wa dharura
© WFP/Ali Jadallah
Palestina. Usambazaji wa mkate wa WFP katika shule ya UNRWA ambayo ni makazi maalum wakati wa dharura

Mfumo wa chakula Gaza umesambaratika kabisa: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati umesambaratisha kabisa mfumo wa chakula Gaza limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, likisisitiza wakati huu ambapo ni asilimia 10 tu ya bidhaa muhimu za chakula ndizo zinazoingia Gaza tangu kuanza kwa mzozo huo Oktoba 7. Hali ni mbaya na imesababisha njaa kwa karibu wate wote wa eneo hilo na tegemeo lao pekee lililobaki ni msaada wa chakula kutoka WFP.

Watoto wakicheza nje ya majengo ya shule ya umma ya GV  katika eneo la Deir El Balah Gaza, kana kwamba hakuna kinachoendelea, wakifurahia utoto wao na kidogo kusahau vita iliyowalazimu kuwa wakimbizi wa ndani katika shule hii iliyogeuzwa makazi ya muda.

Inakadiriwa kwamba watu takriban 6,000 wanapata hifadhi katika kila shule kama hii.

Hapa mlo ni changamoto 

Wanawake kwa wanaume wanapika na kujaribu kuoka mikate ambayo ndio chakula kikuu Gaza kwenye majiko ya kuni na mkaa kwani hawana gesi wala umeme. Shifa Al Masri ni mama na mmoja wa wakimbizi wa ndani hapa anasema “Watoto wananjaa na kiu na wote wanaharisha kutapika na kukohoa, hakuna chakula wala matibabu”

Kabla ya machafuko ya sasa watu hawa walikuwa walila wawzavyo na kujipatia mahitaji katika maduka ya chakula yanayoendeshwa na WFP lakini sasa maduka haya yamesalia matupu bila chochote.

Ni asilimia 25 tu ya maduka yote ya WFP Gaza ndio yaliyosalia wazi na mengine yote yamefunga mlango kwa kuishiwa chakula na yaliyowazi chakula kidogo kilichopo gharama haishikiki hali ambayo imewalazimu watu kula mlo mmoja tu kwa siku.

Alaa Younis Mohamed Al-Helw hakuwa na jinsi bali kukimbia na familia yake hadi kwenye makazi haya ambapo sasa analala chini katika nyumba iliyofurika watu 30. Kaja dukani kuangalia mahitaji , lahaula kambulia patupu anatoa wito,

“Kama unavyoona tumekuja katika duka hili hakuna chochote tangu asubuhi tumezunguka maduka yote hakuna kitu. Wajuzeni watu ili dunia isikie tuna njaa, tuna njaa tunataka kula, Kuna watoto na mke wangu ana ugonjwa wa moyo anahitaji kula na hakuna hata kipande cha mkate cha kumpa.”

Mkate chakula kikuu cha Wapalestina sasa umeadimika kupita kiasi, matumaini yao yote yako kwa WFP. Samer Abdeljaber ni mkurugenzi wa WFP eneo la Palestina, “Watu wanalala njaa. Gaza, watu wanaishi kwa mlo mmoja tu kwa siku ikiwa wana bahati. Uhaba wa mafuta na kutokuwa na mawasiliano kunalemaza operesheni zetu huko Gaza. Ukosefu wa mafuta umekilazimu kiwanda cha mwisho cha kuoka mikate cha WFP kufungwa na pia kinu cha mwisho cha kusagisha unga wa ngano. Hata mkate ambao ni msingi wa kila mlo wa Wapalestina, sasa umeadimika.”

Pamoja na changamoto zote hizo WFP imeendelea kuwahakikisha mlo hata kama ni mmoja tu watu hawa, inagawa tende na samaki wa makopo kila siku kwa watu karibu 800,000 wanaohifadhiwa katika shule za shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA na jamii zinazowazunguka.