Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia Gaza wanahaha kuishi huku eneo la Kaskazini litenganishwa na dunia: UN

Uharibifu mkubwa unaonekana katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 10 Oktoba 2023.
WHO
Uharibifu mkubwa unaonekana katika ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya Israel tarehe 10 Oktoba 2023.

Raia Gaza wanahaha kuishi huku eneo la Kaskazini litenganishwa na dunia: UN

Msaada wa Kibinadamu

Mamia kwa maelfu ya Wapalestina waliosalia kaskazini mwa Gaza wanaendelea kustahimili matatizo ambayo hayajawahi kushuhudiwa baada ya operesheni za jeshi la Israel kulikatilia mbali na sehemu nyingine za eneo hilo, huku msafara wa msaada wa matibabu uliotumwa na Umoja wa Mataifa na washirika wake ukishambuliwa katika mji wa Gaza yamesema leo mashirika ya misaada ya kibinadamu.

Haya yanajiri wakati mawaziri wa mambo ya nje wa kundi la nchi 7 tajiri duniani za G7 wakijiunga na wito wa kimataifa wa kusitisha uhasama kwa minajili ya kibinadamu ili kuwalinda raia, kusaidia kufikisha misaada na kuunga mkono kuachiliwa kwa mateka zaidi ya 240 wanaoshikiliwa huko Gaza na Hamas tangu tarehe 7 Oktoba. .

Hakuna duka la mikate linalofanya kazi kaskazini mwa Gaza kwa sababu ya ukosefu wa mafuta, maji na unga wa ngano na hakuna chakula au maji ya chupa ambayo yamesambazwa huko kwa muda wa wiki moja, kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ta dharura OCHA.

Msafara wa misaada washambuliwa

Kwa sababu ya ukosefu wa vifaa vya matibabu, hospitali za kaskazini sasa zinafanya upasuaji bila ganzi, shirika la afya la Umoja wa Mataifa la afya duniani WHO lilisema. 

Ikitanabaisha hali mbaya ya afya, OCHA imeripoti kuwa msafara wa malori matano kutoka WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kmsaada kwa wakimbizi wa Palestina (UNRWA), ukisindikizwa na magari mawili ya Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ulikabiliwa na mashambukizi ukiwa njiani. kupeleka vifaa vya matibabu vya kuokoa maisha katika hospitali za Shifa na Al Quds katika mji wa Gaza jana Jumanne.

Malori mawili yaliharibika na dereva mmoja alijeruhiwa, lakini msafara huo hatimaye ulifika hospitali ya Shifa na kujifungua, OCHA imesema.

Moja ya familia iliyotawanywa kutoka Al Ganoub Oktoba 2023.
OCHA/Manal Massalha
Moja ya familia iliyotawanywa kutoka Al Ganoub Oktoba 2023.

Watu waamriwa kuondoka Gaza Kaskazini

Wakati huo huo, mashambulizi ya Israel yanaendelea katika Ukanda wa Gaza huku makundi ya Wapalestina yenye silaha yakiendelea pia kurusha makombora kuelekea Israel. 

Wanajeshi wa Israel wameripotiwa kuwa ndani ya Mji wa Gaza kuwasaka wapiganaji wa Hamas waliohusika na shambulio baya la Oktoba 7 kusini mwa Israel.

OCHA imesema kuwa jeshi la Israel lilirejelea maagizo yake ya kuwahamisha wakaazi wa kaskazini na jana , kwa siku ya nne mfululizo, lilifungua upenyo kwenye eneo la pilika nyingi, na kuwapa wakazi fursa ya saa nne kuondoka kuelekea kusini.

Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kuwa hadi watu 15,000 wanaweza kuwa wametumia njia hiyo. 

OCHA imesisitiza kuwa "wengi, wakiwemo watoto, wazee na watu wenye ulemavu, walifika kwa miguu wakiwa na vitu kidogo walivyoweza kubeba".

Watoto walio kwenye machine za kupumua wako hatarini

Jana Jumanne jeshi la Israel pia lilitoa upya maagizo yake ya kuhamishwa kwa hospitali ya Rantisi katika mji wa Gaza, kituo pekee cha watoto kaskazini mwa Gaza, "likidai kwamba makundi yenye silaha yalikuwa yanatumia majengo na mazingira yake", limesema shirika la OCHA.

Kulingana na mamlaka ya afya ya Gaza, uhamishaji kama huo unaweza kuhatarisha maisha ya watoto kadhaa ambao wako kwenye machine za usaidizi wa kupumua ili kuokoa Maisha yao, kusafishwa kwa figo au kwa wale wanaotegemea vifaa vya kuwasaidia kupumua.

Familia nyingi zimehamia kwenye makambi ya wakimbizi ya Khan Younis Kusini mwa Gaza
© WHO
Familia nyingi zimehamia kwenye makambi ya wakimbizi ya Khan Younis Kusini mwa Gaza

Onyo juu ya uharibifu wa makazi

Takriban thuluthi moja ya majengo yote kaskazini mwa Gaza yameripotiwa kuharibiwa au kusambaratishwa, na mtaalam wa haki za binadamu aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa ameonya leo kwamba mashambulizi ya mabomu kwa nyumba ya kimfumo, vifaa vya kiraia na miundombinu ni marufuku kabisa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu, za jinai na sheria za haki za binadamu.

Balakrishnan Rajagopal, Mtaalamu Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki ya makazi ya kutosha, amesema kuwa kufanya uhasama "kwa kujua kwamba utasambaratisha na kuharibu makazi na miundombinu ya raia, na kufanya mji mzima kama vile mji wa Gaza kutoweza kuishi kwa raia ni uhalifu wa kivita”.

Wataalam Maalum wa Umoja wa Mataifa ni wataalam huru walioteuliwa na Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa. Sio wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa na hawapati mshahara kutoka kwa Umoja wa Mataifa kwa kazi zao.

Asilimia 4 tu mahitaji ya maji yanashughulikiwa

Kusini mwa Gaza, kutafuta chakula na maji bado ni changamoto, OCHA inasema. Viwanda 11 vya mikate vimeshambuliwa na kuharibiwa tangu tarehe 7 Oktoba na "kinu pekee kinachofanya kazi huko Gaza kimesimama kutokana na ukosefu wa umeme na mafuta.”

OCHA imesema kuwa mikate hutolewa kwenye viwanda vya kuoka mikate mara kwa mara na watu hupanga foleni kwa saa nyingi mbele ya viwanda vinavyofanya kazi vya kuoka mikate, ambapo wana hatari ya kukumbwa na mashambulizi ya anga.

Maji yanayoingia kutoka Misri katika chupa na mikebe “yanashughulikia asilimia nne tu ya mahitaji ya maji ya wakazi kwa siku", limeonya shirika la OCHA kulingana na mgao wa lita tatu kwa kila mtu kwa siku kwa madhumuni yote, ikiwa ni pamoja na kupikia na usafi.

Misaada ikiwasilishwa katika kambi ya wakimbizi ya Khan Younis Ukanda wa Gaza
WHO
Misaada ikiwasilishwa katika kambi ya wakimbizi ya Khan Younis Ukanda wa Gaza

Msaada unaopatikana ni kama tone baharini

Jana Jumanne, malori 81 yaliyokuwa yamebeba chakula, dawa, vifaa vya afya, maji ya chupa na bidhaa za usafi yaliingia Gaza kutoka Misri kupitia kivuko cha Rafah. 

Kwa jumla, malori 650 ya misaada yameingia Gaza tangu kuruhusiwa tena kuingia tarehe 21 Oktoba.

OCHA imesema kwamba kabla ya kuanza kwa uhasama, wastani wa malori 500 yaliingia Gaza kila siku za kazi.

WHO imetaja kiasi cha msaada ambacho imeweza kutoa hadi sasa ni sawa na "tone tu la maji katika bahar ikilinganishwa na mahitaji makubwa yaliyopo.”

Umoja wa Mataifa mara kwa mara umetoa wito wa upatikanaji wa misaada zaidi katika eneo hilo. 

Alhamisi wiki hii, mkuu wa Umoja wa Mataifa wa misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura Martin Griffiths atamwakilisha Katibu Mkuu António Guterres katika mkutano wa kimataifa kuhusu misaada ya kibinadamu kwa raia wa Gaza unaoandaliwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Paris.