Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bado haki za mtoto zinasiginwa, miaka 34 tangu CRC- UNICEF

Watoto wakimbizi wa ndani huko Cabo Delgado, Msumbiji
© UNICEF/Daniel Timme
Watoto wakimbizi wa ndani huko Cabo Delgado, Msumbiji

Bado haki za mtoto zinasiginwa, miaka 34 tangu CRC- UNICEF

Haki za binadamu
  • Mkataba umepitishwa 1989 lakini hali bado tete 
  • Haki zinapondwaponda kuanzia kuishi hadi kulindwa 
  • Ni maombolezo badala ya sherehe

Miaka 34 tangu kupitishwa kwa Mkataba wa Kimataifa wa haki za Mtoto (CRC) bado watoto katika maeneo mbalimbali duniani wanaishi kwenye mazingira yanayosigina haki zao. 

Kauli hiyo ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, (UNICEF) Catherine Russell, aliyoitoa leo New York, Marekani, ambayo ni siku ya mtoto duniani inayoadhimishwa kukumbuka kupitishwa kwa CRC ikiwa na haki kuu nne za msingi wa mtoto ambazo ni kuishi, kuendelezwa, kushirikishwa na kulindwa. 

Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 akiwa amebeba mwanae katika nyumba ya wazazi wake huko Kasese, Magharibi mwa Uganda.
© UNICE/Henry Bongyereirwe
Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 14 akiwa amebeba mwanae katika nyumba ya wazazi wake huko Kasese, Magharibi mwa Uganda.

Mkataba umesainiwa na nchi nyingi zaidi lakini utekelezaji hakuna 

CRC ni Mkataba wa Kimataifa ambao historia inaonesha kuwa ni mkataba wa kimataifa ulioridhiwa na idadi kubwa zaidi ya nchi duniani, na nchi hizo kwa kufanya hivyo zimeahidi kulinda haki hizo za mtoto na zizingatiwe. 

“Hakuna pahala ambako usiginaji wa haki za mtoto uko dhahiri na watoto wana uzoefu wa haki zao kupondwapondwa kama wale walioathirikwa na vita,” anasema Bi. Russell. 

Takwimu za UNICEF zinakadiria kuwa watoto milioni 400 – au mtoto 1 kati ya watoto 5– wanaishi kwenye mizozo au wanakimbia mizozo. Wengi wao wanauawa, wanajeruhiwa au wanakumbwa na ukatili wa kingono. Halikadhalika wanapoteza familia na jamaa zao, marafiki na wengine kutumikishwa vitani na vikundi vilivyojihami. 

“Umoja wa Mataifa umethibitisha zaidi ya matukio 315,000 ya ukiukwaji wa haki za mtoto kwenye maeneo yenye mizozo kati yam waka 2005 hadi 2022,” anasema Mkuu huyo wa UNICEF. 

Mabadiliko ya tabianchi, umaskini navyo vyasigina haki za mtoto 

Kando ya maeneo ya mizozo, haki za mtoto pia zinatishiwa mathalani ongezeko la umaskini, mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la ukosefu wa usawa. 

Haki za mtoto zinakiukwa kwa kiwango kikubwa zaidi hivi sasa, miaka 34 tangu kupitishwa kwa Mkataba huo na hivyo Mkurugenzi Mkuu huyo wa UNICEF anasema “ni wakati wa kuchukua hatua. Natoa wito kwa kila mtu kuanzia hapa UNICEF na wadau wetu wa jamii za haki za mtoto pamoja na serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia kuwa mabingwa na wachechemuzi wa kulinda haki za mtoto kwa kujumuisha vipengele vya CRC kwenye sheria za nchi.” 

Amesema leo Novemba 20 inapaswa kuwa siku ya kusherehekea kuongeshwa kwa haki za mtoto duniani lakini cha ajabu haki zinashambuliwa. 

Familia zinaendelea kupata hifadhi katika kambi ya Khan Younis huko Gaza.
© WHO
Familia zinaendelea kupata hifadhi katika kambi ya Khan Younis huko Gaza.

Badala ya sherehe sasa ni maombolezo 

Kutoka Geneva, Uswisi, Kamati ya Baraza la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu imetoa taarifa yake hii leo ikisema siku hii ya mtoto duniani inaadhimishwa katika mazingira ya majonzi kwani mtoto 1 kati ya 5 anaishi kwenye maeneo ya mizozo, na hivyo inataka sitisho la mapigano ili sheria ya kimataifa ya kiutu iweze kuzingatiwa na kulinda haki za watoto wote. 

“Siku hii badala ya kuwa ya sherehe imekuwa siku ya maombolezo kwa ajili ya watoto wengi waliouawa kwenye mizozo ya hivi karibuni. Zaidi ya watoto 4,600 wameuawa ukanda wa Gaza katika kipindi cha wiki 5” imesema taarifa hiyo kwa kuwa mapigano yalianza Oktoba 7 2023 kati ya Israeli na wanamgambo wa kipalestina wa Hamas walioanza kushambulia Israeli.

Kamati inasema katika siku ya leo pamoja na suala la eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli ndio linagonga vichwa vya watu hivi sasa, ingependa pia kuelezea shaka na shuku zake kuhusu hali ngumu za maelfu ya watoto kwenye mizozo huko Ukraine, Afghanistan, Yemen, Syria, Myanmar, Haiti, Sudan, Mali, Niger, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Somalia. 

Soma habari nzima ya Kamati hapa