Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni hatarini kutokana na milipuko ya magonjwa Sudan: WHO

Akina mama waleta watoto wao kwa uchunguzi wa lishe katika kliniki tembezi ya afya katika jimbo la Kassala, Sudan.
© UNICEF/Osman
Akina mama waleta watoto wao kwa uchunguzi wa lishe katika kliniki tembezi ya afya katika jimbo la Kassala, Sudan.

Mamilioni hatarini kutokana na milipuko ya magonjwa Sudan: WHO

Afya

Sudan, nchi iliyoghubikwa na vita, hivi sasa inakabiliwa na janga lingine la afya ambapo magonjwa ya kipindupindu, surua, homa ya kidingapopo na malaria vinazunguka katika majimbo kadhaa na mchanganyiko wa magonjwa haya yote na utapiamlo vinaweza kuwa na athari mbaya sana kwa mamilioni ya watu limeonya leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO.

Shirika hilo limesema wiki iliyopita idadi ya watu wanaoshikiwa kuwa na kipindupindu iliripotiwa kufikia 1,962 na vifo 72 vinavyohusishwa na ugonjwa huo. 

Na zaidi ya watu milioni 3.1 wanakadiriwa kuwa katika hatari ya ugonjwa huo kufikia mwisho wa mwaka huu limeonya shirika hilo la WHO.

Magonjwa mengine yaliyoenea

Wakati huo huo, WHO imesema nchi hiyo ina zaidi ya watu 4,300 wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa wa surua, zaidi ya watu 4,000 wanaoshukiwa kuwa na homa ya kidingapopo na zaidi ya wagonjwa 813,000 wa malaria, huku watoto milioni 4.6, wajawazito na akina mama wanaonyonyesha wakiwa na utapiamlo.

Mfumo wa afya nchini humo "umefikia hatua mbaya” WHO imesema, huku hadi vituo 4 kati ya 5 vya afya vilivyo katika maeneo yenye migogoro havifanyi kazi na kuna upatikanaji mdogo wa huduma za afya nchini kote kutokana na ghasia, kuhama kwa watu wengi na uhaba wa dawa na vifaa tiba. 

Pia shirika hilo la afya limesema wahudumu wa afya ambao wamefanya kadiri wawezavyo kuhakikisha vituo vikiendelea kufanyakazi licha ya hatari binafsi hawajalipwa kwa takriban miezi saba sasa.

Mfumo wa afya umelemewa 

Dkt. Ni’ma Saeed Abid ambaye ni Mwakilishi wa WHO nchini Sudan, leo ameripoti kuwa “Mfumo wa afya nchini humo umezidiwa kiasi cha kufikia hatua mbaya huku mahitaji yakiongezeka kutokana na milipuko hiyo ya magonjwa, utapiamlo, na kuongezeka kwa wagonjwa wenye magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambao hawajatibiwa mathalani wenye kisukari, shinikizo la damu, saratani, magonjwa sugu ya kupumua na figo.”

Hata hivyo amesema WHO Sudan inajiandaa kupokea chanjo ya matone dhidi ya kipindupindu kutoka kwa ICG ambalo ni kundi la kimataifa la kuratibu usambazaji wa chanjo nyakati za dharura linaloundwa na WHO shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na wadau wengine. 

WHO imekuwa ikiunga mkono hatua za mamlaka za afya Sudan kupambana na changamoto hizo za kiafya kwa kutoa vifaa, wafanyakazi na mafunzo kwa vituo vya matibabu ya kipindupindu, kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na kusaidia kuendesha kampeni za chanjo ya surua.