Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na wadau wake wabuni mbinu za kukabiliana na janga la tabianchi na changamoto katika jamii nchini Kenya

UNICEF na Equal Access International, wabuni mbinu za kukabiliana na changamoto katika jamii nchini Kenya. Vijana wahamasishwa kupitia programu za redio.
UNICEF
UNICEF na Equal Access International, wabuni mbinu za kukabiliana na changamoto katika jamii nchini Kenya. Vijana wahamasishwa kupitia programu za redio.

UNICEF na wadau wake wabuni mbinu za kukabiliana na janga la tabianchi na changamoto katika jamii nchini Kenya

Tabianchi na mazingira

Janga la tabianchi limesababisha kupotea kwa upatikanaji wa elimu, huduma muhimu, na ajira kwa vijana nchini Kenya, hata hivyo Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini humo kwa kushirikiana na shirika la Equal Access International wanawawezesha vijana kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko tabianchi na kutoa ufahamu kuhusu suluhisho la kukabiliana na tatizo hilo. 

Halikadhalika janga hilo limesababisha ukame mkali zaidi katika taifa hilo la Afrika Mashariki na kuathiri maeneo ya Garissa, Wajir, na Mandera, na mvua zinapoanza kunyesha hali hurejea taratibu, vijana wameathiriwa na hali hiyo, wengi wanakosa elimu, huduma za kimsingi na wanahangaika kutafuta ajira. 

Ummulkheir Ahmed Shale ni msanii anayejihusisha na Sanaa ya uchoraji na pia ni mwanasheria anayeishi Garissa kaskazini mwa Kenya, anasema mabadiliko ya tabianchi yamewaathiri kwa kiasi kikubwa, 

“Mabadiliko ya tabianchi yametuathiri duniani kote, lakini kaskazini mwa Kenya huko Garissa, yametuathiri sana, sisi ni wafugaji wa kuhamahama, ukame unapokuja, hatari ni kupoteza maisha, watoto wanaacha shule, ndoa za mapema, mimba za utotoni, kuna changamoto nyingi”.

UNICEF na Equal Access International wanashirikiana katika mradi wa mawasiliano ya kijamii na mabadiliko ya tabia ili kupunguza athari za ukame na kuwawezesha vijana, kujadili masuala mbalimbali kama vile ndoa za mapema, vurugu shuleni, chanjo, na mazoea salama ya usafi, miradi hii inatoa nafasi salama kwa vikundi vya jamii kusikiliza, kujadili, na kuchukua hatua katika jamii zao (LDAG). 

"Nimehudhuria vikao vya LDAG kwa wiki 10 na imekuwa na athari chanya kwangu binafsi na kwa jamii, ni nafasi salama ambapo vijana wanaweza kukutana na kujadili masuala yanayoathiri jamii yetu”. 

UNICEF na Equal Access International, wabuni mbinu za kukabiliana na changamoto katika jamii nchini Kenya. Vijana wahamasishwa kupitia programu za redio.
UNICEF
UNICEF na Equal Access International, wabuni mbinu za kukabiliana na changamoto katika jamii nchini Kenya. Vijana wahamasishwa kupitia programu za redio.

Kila wiki, kipindi kipya cha redio huzalishwa kwa kuzingatia masuala ya kijamii yanayoathiri katika maeneo yao na kisha hupeperushwa kwenye vituo vya redio huko Garissa, Wajir, na Mandera, ambapo vikundi 18 na wazazi hukutana kila wiki kusikiliza na kujadili yaliyomo kwenye vipindi hivyo. 

Jane Maru ni Meneja wa Mradi wa Equal Access International na Petur Thorkelsson, Afisa wa Mabadiliko ya Tabia za Kijamii wa UNICEF nchini Kenya, wanasema,  

“Redio haitapotea kamwe au kuwa nje ya mtindo mtindo kwa sababu mtu yeyote katika eneo la vijijini hatahitaji data (Internet) kutumia redio, kwa mradi huu unaofadhiliwa na UNICEF tulikuwa na vipindi 20 vya redio, 10 zikiwalenga vijana na 10 zikiwalenga wazazi”. 

Na Petur Thorkelsson anaongeza, 

"Kwa kutumia nyenzo katika vipindi vya redio, kimsingi wanakwenda katika jamii zao na kuchukua hatua juu yake, na hii ndiyo lengo kuu la mradi, kujenga mabadiliko endelevu ambapo watu wanaweza kuwa na masuala ya kusema katika jamii zao”. 

Takriban watu 5,400 wameshiriki katika vikao vya LDAG ndani ya wiki 10 tangu kuanzishwa kwa mradi na kuleta matokeo chanya, lakini matarajiyo ni yapi? 

“Kwa siku zijazo, tunataka kushirikiana zaidi na wenyeji wote hapa Garissa, lakini pia Wajir na Mandera, ili kweli sauti zao ziweze kujenga programu, matumaini yangu kwa program hii ni kwamba tuendelee nayo kwa sababu tayari tumekuwa na jina lenye kukubalika ndani ya jamii."