Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yanavyohaha kuwasaidia waathirika wa mizozo na ukame Baidoa Somalia

Wafanyakazi wa IOM wanaosimamia kambi wanafanya kazi katika baadhi ya kambi kubwa za watu waliokimbia makazi yao nchini Somalia.
IOM/Claudia Rosel
Wafanyakazi wa IOM wanaosimamia kambi wanafanya kazi katika baadhi ya kambi kubwa za watu waliokimbia makazi yao nchini Somalia.

Mashirika ya UN yanavyohaha kuwasaidia waathirika wa mizozo na ukame Baidoa Somalia

Tabianchi na mazingira

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani, WHO inasema idadi ya milipuko ya magonjwa iliyoripotiwa na dharura za kiafya zinazohusiana na tabianchi katika Ukanda wa Pembe ya Afrika zimefikia kiwango cha juu zaidi kuwahi kutokea karne hii, na hivyo kuzidisha janga la kiafya katika eneo ambalo watu milioni 47 tayari wanakabiliwa na njaa kali. 

Ni katika viunga vya mji wa Baidoa ambao ni mkubwa zaidi katika jimbo la Kusini Magharibi la Somalia, vimetapakaa vijumba vidogo vidogo vya msonge vilivyofunikwa na maturubai, karatasi za nailoni na vipande vya sandarusi, vyote chakavu. Kila mahali ni mchanga mkavu na miti iliyomea hapa, kwa muonekano tu, ni dhahiri miti hii ina kiu ya muda mrefu.

Wafanyakazi wa WHO na IOM wanapita huku na kule katika kambi hii ya wakimbizi wa ndani wakiandaa kila namna ya kuwasaidia watu. Na wakati maafisa hao wa Umoja wa Mataifa wakizungumza na viongozi wa kambi, wananchi walioko hapa wanasubiri kwa hamu angalau kusikia neno moja litakalowatia moyo kwa siku hiyo.

James Ndithia ni Mratibu wa WHO katika kushughulikia madhara ya ukame kwenye eneo hili la Baidoa anasema, "Baidoa ni mojawapo ya wilaya mbili katika jimbo la Kusini Magharibi ambazo zimekuwa katika hali ya tahadhari ya uwezekano wa kutumbukia kwenye njaa kali. Kwa sababu ya migogoro ya muda mrefu, tuna idadi kubwa ya watu waliohama makazi yao. Na tunapozungumza juu ya ukame huu wa mara kwa mara, jambo ambalo ulimwengu hauwezi kuelewa ni kwamba tunashughulikia hali hii hii kila mwaka. Kwa hivyo mfululizo wanapoteza mali zao za uzalishaji, kupoteza maisha yao na kuwa maskini zaidi na zaidi kila tukio la ukame.”

Bundobo Hassan, aliyewasili kambini hivi karibuni, anaandaa mlo pekee wa siku kwa ajili yake na watoto wake anasema…Wamekuwa katika hali ya ukame kwa miaka mitatu, walipoteza mifugo yao yote; wengine wamekufa njaa; “hatukuweza kupata usafiri, tuliwabeba watoto hawa vichwani; na wale walioweza kutembea walitembea”, anaeleza huku watoto wake wakisubiri ugali wa muhogo na kisamvu.

"Tunaishi tu kwa kile ambacho watu wanatupatia.” Anaendelea kueleza mama huyu anayeonekana kukata tamaa. 

Mirura Abdirizak ni Mhudumu wa Afya ya Jamii  wa WHO, "Tunatoa chanjo, maji ya dawa, zinki, Albendazole, na vitamini A. Watu wanapata chakula lakini hakitoshi kukidhi mahitaji yao. Watu wengi katika kambi hizi za wakimbizi wa ndani ni wale ambao wamefurushwa kutoka vijiji vyao, na wana uhitaji mkubwa wa chanjo. Kulikuwa na mlipuko wa surua wa mara kwa mara Baidoa, na watu walifurahi kupokea chanjo.”

Mratibu wa WHO katika kushughulikia madhara ya ukame kwenye eneo hili la Baidoa anarejea kwa masikitiko akieleza wanavyoitizama hali hii ya Somalia kwa ujumla wake. Anasema, “Kwa maoni yetu, ni sehemu ya tatizo kubwa la mabadiliko ya tabianchi na ongezeko la joto duniani. Na kwa bahati mbaya kwetu katika sehemu hii ya dunia, tunaonekana kuwa tunalipa gharama kubwa zaidi katika masuala ya athari kwa mwanadamu, kwa maana ya uwezo wetu wa kupambana na njaa na umaskini. Na kwa njia hii basi, tuko katika hatari ya kukosa kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.”

Video iliyoandaliwa na WHO na ambayo pia unaweza kuitazama kupitia channel yetu ya Youtube ya Habar iza UN, inahitimisha makala hii ikihama kutoka Baidoa hadi eneo jingine, wilaya ya Dolow katika mkoa wa Gedo. Huko nako hali ni tete. Ni uwanda mpana mkavu bila nyasi wala miti, anayeonekana ni ndege mmoja aking’ang’ana kidonoa kilichosalia katika mzoga wa mnyama uliokauka.