Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kisima kinachotumia nishati ya jua chawa mkombozi wa elimu kijijini Daley, Garissa, Kenya

Tarehe 26 Oktoba 2022, katika kijiji cha Daley katika Kaunti ya Garissa, Kenya - (kutoka kushoto kwenda kulia) Osman (11), Abdullahi (15) na Abdi (12) wa shule ya msingi ya Daley wakinywa maji safi na salama yanayotoka katika kisima kinachoendeshwa kwa n…
©UNICEF/James Ekwam
Tarehe 26 Oktoba 2022, katika kijiji cha Daley katika Kaunti ya Garissa, Kenya - (kutoka kushoto kwenda kulia) Osman (11), Abdullahi (15) na Abdi (12) wa shule ya msingi ya Daley wakinywa maji safi na salama yanayotoka katika kisima kinachoendeshwa kwa nishati ya jua, mradi uliofadhiliwa na UNICEF katika kijiji hicho.

Kisima kinachotumia nishati ya jua chawa mkombozi wa elimu kijijini Daley, Garissa, Kenya

Tabianchi na mazingira

Msaada wa kisima cha maji uliofanikishwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF katika shule ya Msingi ya Daley kwenye Kijiji cha Daley, Kaunti ya Garissa nchini Kenya, umesaidia sana jamii hasa katika suala la elimu katika eneo hilo la nchi ambayo imekosa mvua ya kutosha kwa misimu mitano mfululizo.

Ni wanafunzi wakiwa darasani, kwa uchangamfu wakijadiliana na mwalimu wao kuhusu umuhimu wa maji katika maisha ya kila siku. Nje ya darasa lao kunaonesha wazi hali ya ukame ilivyo ya kutisha. Ardhi imekauka na ni miti michache tu imebaki na ukijani. Kabla ya UNICEF kwa kushirikiana na jamii na serikali kuigilia kati, hali ya kukosekana kwa mvua imesumbua maisha ya wakazi wa hapa ikiwemo upatikanaji wa elimu kwa watoto wa jamii hii ya wafugaji kama asemavyo Mwalimu Mkuu Msaidizi, Wasula Samson Saiya anasema "Tuna takribani wasichana 146 na wavulana 200 jumla wanafunzi 346. Unagundua kwamba wengi wa wanafunzi wanachunga mifugo. Kwa hiyo, wakati wa ukame kama hivi unakuta pia wanahama na wanyama hao kule walikokwenda kulishia ili wawachunge. Kwa hivyo, tunajikuta tuna wanafunzi wachache darasani.” 

Ili kuitatua hali hiyo, UNICEF ilitoa msaada wa kifedha na kiufundi kuchimba kisima cha chini ya ardhi na kuweka mfumo wa kupaadisha maji kwa kutumia nguvu ya nishati ya jua na pia ujenzi wa upanuzi mpya wa bomba ili kuunganishwa na miundombinu iliyopo ya usambazaji wa maji. Takriban watu 6200 wakiwemo wanafunzi kutoka Shule ya Msingi ya Daley na Kituo cha Maendeleo ya Awali ya Watoto (ECDC) wanapata huduma ya maji salama. Aidha, zahanati moja ya afya ina huduma ya maji salama. 

Osman Aden Abdi, Naibu Mkurugenzi, Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Idara ya Maji ya Kaunti ya Garissa anasema "Faida ni nyingi. Wakati tulipopata kisima, hali ya hatari katika suala la wanyama pori imepungua. Unyanyasaji wa kijinsia pia umepungua kwa sababu kioski hiki cha maji kiko mahali pa wazi sana. Tuna bahati sana kwa sababu umbali ni kama mita 50 tu hadi mahali pa maji. Inaokoa muda linapokuja suala la masomo ... unajua, katika maeneo yetu ni kukavu sana na joto sana. Kwa hivyo, tunawaruhusu wanafunzi kupata maji kila baada ya dakika 30...badala ya kurudi nyumbani. Kuna maeneo kadhaa ambako UNICEF, kwa usaidizi wa serikali ya kaunti imeweka mitambo ya nishati ya jua. Baada ya kisima hiki kilichimbwa na kuwekewa nishati ya jua, hakuhitajiki gharama zaidi, ili kwa muda mrefu jamii ziweze kujikimu zenyewe.” 

Kufikia Novemba 2022, katika Kaunti ya Garissa, UNICEF tayari imesaidia ukarabati wa mifumo 21 ya usambazaji wa maji na kufikia jumla ya watu 92,279 wanaopata maji salama.