Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nigeria kutoa chanjo ya HPV kwa wasichana milioni 7.7

Msichana mdogo nchini Nigeria apewa chanjo.
© UNICEF Nigeria
Msichana mdogo nchini Nigeria apewa chanjo.

Nigeria kutoa chanjo ya HPV kwa wasichana milioni 7.7

Afya

Nigeria hii leo imetangaza kuanzisha chanjo ya virusi vya human papilloma (HPV) katika mfumo wake wa kawaida wa chanjo, ikilenga kuwafikia wasichana milioni 7.7 hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi katika awamu moja ya chanjo ya HPV barani Afrika.

Taarifa iliyotolewa leo na Shiria la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO kutoka Abuja Nigeria imeeleza kuwa nchini humo saratani ya shingo ya kizazi ni saratani ya tatu kwa wingi na ya pili kwa vifo vya saratani miongoni mwa wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 na 44. 

Virusi vya HPV vinaelezwa kusababisha karibu wagonjwa wote wa Saratani ya shingo ya kizazi.

Ufadhili 

Chanjo hiyo inatolewa bure kwa Wizara ya Afya ya Nigeria kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo ya Afya ya Msingi kwa msaada wa Ubia wa chanjo duniani, GAVI, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) na wadau wengine.

Ofisi ya WHO nchini Nigeria na washirika wake imetoa mafunzo kwa wafanyakazi wa afya 35,000 katika maandalizi ya kampeni hiyo ya utoaji chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi, mojawapo ya saratani chache ambazo zinaweza kuondolewa kwa chanjo. 

“Tumejitolea kusaidia serikali kuongeza ufikiaji wa chanjo ya HPV ili kulinda afya na ustawi wa kizazi kijacho cha wanawake." Amesema Dkt. Walter Kazadi Mulombo, Mwakilishi wa WHO nchini Nigeria.

Wito wa Serikali ya Nigeria kwa wazazi

Takwimu za hivi karibuni zilizokusanywa mwaka 2020 zinaonesha nchi hiyo imerekodi wagonjwa wapya 12,000 na vifo 8000 kutokana na saratani ya shingo ya kizazi.

Pate Muhammad Ali ni Waziri anayehusika na Uratibu wa Afya na Ustawi wa Jamii nchini Nigeria na amesema “Kupoteza takriban wanawake wa kinigeria 8000 kila mwaka kutokana na ugonjwa ambao unaweza kuzuilika haikubaliki kabisa.”

Wasichana wenye umri wa miaka 9 mpaka 14 watapata dozi moja ya chanjo hiyo, ambayo ina ufanisi mkubwa katika kuzuia maambukizi ya HPV aina ya 16 na 18 ambayo inajulikana kusababisha takriban asilimia 70 ya saratani ya shingo ya kizazi.

Waziri Ali amesema “Saratani ya shingo ya kizazi husababishwa zaidi na HPV, na wazazi wanaweza kuepuka maumivu ya kimwili na ya kifedha kwa kuwalinda watoto wao kwa dozi moja ya chanjo. Kuokoa maisha, na kutoa matokeo bora ya afya na kulinda ustawi wa Wanigeria ni msingi wa Ajenda Mpya ya Afya ya Rais Bola Ahmed Tinubu.” 

Amesisitiza kuwa kuanza kwa kampeni ya chanjo hiyo ni fursa ya kuwalinda wasichana dhidi ya janga la saratani ya shingo ya kizazi miaka mingi ijayo. 

“Ningependa kuwasihi wazazi wenzangu kuhakikisha kwamba kizazi hiki cha wasichana wetu kinavuruga upotezaji wa maisha unaoweza kuzuilika kutokana na saratani ya shingo ya kizazi pamoja na taabu, hasara na maumivu mengine yasiyoelezeka.”

Waziri huyo wa Afya wa Nigeria amesema Kampeni ya siku tano ya chanjo kubwa mashuleni na katika jumuiya itatekelezwa wakati wa uzinduzi utakaohusisha majimbo 16 na Mji Mkuu wa Nigeria.

Kisha chanjo hiyo ya HPV itajumuishwa katika ratiba za kawaida za utoaji chanjo katika vituo vya afya. 

Awamu ya pili ya utoaji chanjo hiyo inatarajiwa kuanza Mei 2024 katika majimbo 21.