Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Athari za COVID-19 kwa huduma za saratani hazielezeki:WHO

Muuguzi akitoa matibabu kwa wagonjwa wanaougua saratani katika hospitali ya wilaya ya Burera, Rwanda.
© UNICEF/Karel Prinsloo
Muuguzi akitoa matibabu kwa wagonjwa wanaougua saratani katika hospitali ya wilaya ya Burera, Rwanda.

Athari za COVID-19 kwa huduma za saratani hazielezeki:WHO

Afya

Leo ikiwa ni siku ya saratani duniani shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO limeonya kwamba athari za janga la corona au COVID-19 kwa vipimo na matibabu ya saratani kote duniani ni kubwa mno na zinaendelea kuongezeka kama inavyofafanua taarifa ya Flora Nducha. 

Kwa mujibu wa shirika hilo ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 athari zake ni za kupindukia hasa kwa kuwa katika serikali nyingi huduma za saratani zimelazimika kupunguzwa kwa asilimia 50, kupatikana kidogo au kusambaratika kabisa.

Dkt. Andre Ilbawi kutoka idara ya WHO ya magonjwa yasiyo ya kuambukizwa amesema kufuatia janga la COVID-19 uchelewashwaji wa vipimo imekuwa kawaida na kuvurugwa kwa huduma kama za mionzi au kuachwa kabisa kumeongezeka kwa kiasi kikubwa , hali ambayo amesema huenda ikawa na athari katika idadi ya vifo vitokanavyo na saratani katika miaka ijayo kote duniani. 

WHO inasisitiza kuwa vipimo ni muhimu sana katika kubaini saratani na matibabau yake kama anavyofafanua Dkt. Adriana Velazquez mhandisi na afisa mkuu mshauri wa vifaa tiba kwenye shirika hilo “Vipimo ni muhimu sana kwa mgonjwa kabla hajaanza matibabu yoyote, hivyo jinsi watakavyofahamu mapema ni ugonjwa gani ndivyo watakavyoweza kupata matibabu bora zaidi. Ni muhimu kwa nchi kuwa na vipimo hivyo, kwenye ngazi ya jamii hadi kwenye hospitali maalum na maabara , na kuwe na mtazamo wa ngazi kama vile ngazi ya jamii, kwenye hospitali za kawaida na kisha kwenye hospitali maalum za saratani.” 

WHO imeongeza kuwa nchi zote za kipato cha juu na cha chini zimepata pigo la COVID-19 katika huduma zake za saratani ingawa kwa nchi tajiri kama Uholanzi zimeweza kupambana na athari hizo ikilinganishwa na nchi masikini. 

Takwimu za shirika hilo zinaonyesha kwamba mzigo wa kiuchumi wa saratani katika jamii unaendelea kuongezeka kwani mwaka 2010 gharama zilikadiriwa kuwa dola trilioni 1.16 na “Mwaka 2020 idadi ya wagonjwa wa saratani kote duniani ilifikia milioni 19.3 huku idadi ya wanaokufa ikiongezeka hadi milioni 10.” 

 Na kwa mara ya kwanza WHO inasema saratani ya matiti ndio inaathairi watu wengi zaidi duniani hivi sasa huku mwaka 2020 kukibainika wagonjwa wapya milioni 2.3 sawa na asilimia 12 ya wagonjwa wote wa saratani na hivyo kuongoza pia kwa idadi ya vifo vya saratani kwa wanawake, ikifuatiwa na saratani ya mapafu ambayo awali ndiyo iliyokuwa ikiongoza na inayoshika nafasi ya tatu ni saratani ya utumbo. 

Shirika hilo limeonya kwamba mzigo wa saratani unatarajiwa kuendelea kuongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ongezeko la watu duniani huku idadi ya wagonjwa wapya kote duniani ikitazamiwa kuongezeka kwa asilimia 47 ifikapo mwaka 2040 ukilinganisha na idadi iliyokuwa 2020. 

Na ili kurejea katika msitari wa kutokomeza saratani ya  shingo ya kizazi, WHO imesisitiza kwamba ni lazima kutimiza malengo matatu ifikapo mwaka 2030 ambayo ni “Mosi asilimia 90 ya wasichana wenye umri wa miaka 15 kupatiwa chanjo ya HPV, pili asilimia 70 ya wanawake waliofikisha umri wa miaka 35 kufanyiwa uchunguzi wa kina kwa kutumia vipimo vya hali ya juu na uchunguzi kurejewa wakiwa na umrim wa miaka 45 na tatu asilimia 90 ya wanawake waliobainika kuwa na saratani ya shingo ya uzazi kutibiwa.” 

Malengo haya yakitimia kwa mujibu wa  WHO yatapunguza idadi ya wagonjwa kwa zaidi ya asilimia 70 ifikapo mwaka 2050 na kuepusha vifo milioni 4.5 vya saratani ya shingo ya kizazi.