Skip to main content

Dozi moja ya chanjo ya HPV inakinga thabiti dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi : WHO

Msichana mdogo akipokea chanjo yake ya kwanza ya HPV kumkinga na saratani ya shingo ya kizazi  nchini Mauritania
© UNICEF/Raphael Pouget
Msichana mdogo akipokea chanjo yake ya kwanza ya HPV kumkinga na saratani ya shingo ya kizazi nchini Mauritania

Dozi moja ya chanjo ya HPV inakinga thabiti dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi : WHO

Afya

Ukaguzi uliofanywa na kundi maalum la wataalamu wa ushauri wa kimkakati wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO lijulikanalo kwa kifupi SAGE umehitimisha kuwa chanjo ya dozi moja ya Human Papillomavirus (HPV) inatoa ulinzi thabiti dhidi ya virusi vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi, ikilinganishwa na dozi mbili au tatu.

Kundi hilo maalum la SAGE lililo kutana tarehe 4 hadi  tarehe 7 April 2022 lilitathmini ushahidi uliojitokeza kwa miaka iliyopita na kueleza matokeo hayo ni habari njema kwa kuwa sasa dozi hizo za HPV zitaweza kuwafikia wasichana wengi zaidi na kuokoa maisha yao.

Taarifa ya WHO kwa vyombo vya habari imemnukuu Dkt. Alejandro Cravioto, mwenyekiti wa SAGE akieleza kuwa chanjo ya HPV ni nzuri sana kwa kuzuia  kirusi aina ya HPV 16 na 18, ambavyo husababisha asilimia 70 ya saratani ya shingo ya kizazi“SAGE inahimiza nchi zote kuanzisha chanjo ya HPV na kuweka kipaumbele kwa kundi la watu wa umri tofauti tofauti kupata chanjo hiyo pamoja na kundi la wasichana wenye umri mkubwa. Mapendekezo haya yatawezesha wasichana na wanawake wengi zaidi kupata chanjo na hivyo kuwaepusha na saratani ya shingo ya kizazi na changamoto zake katika maisha yao yote.”

Mapendekezo ya utoaji chango ya HPV yaliyotolewa ni

• Dozi moja au mbili kwa kundi la msingi la wasichana wenye umri wa kati ya miaka 9-14

• Dozi moja au mbili kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 15-20

• Dozi mbili katika pindi cha miezi 6 kwa wanawake walio na umri zaidi ya miaka 21.

Wataalamu hao wameeleza kuwa watu walio na upungufu wa kingamwili, ikiwa ni pamoja na wale walio na VVU, wanapaswa kupata dozi tatu kama inawezekana, na kama haiwezekani basi angalau wapate dozi mbili.

Ushauri huu umetolewa kufuatia kuwepo kwa ushahidi mdogo kuhusu ufanisi wa dozi moja pekee katika kundi hili.

Dozi moja ni mkombozi kwa nchi masikini

Chaguo hili la kutumia dozi moja ya chanjo ni ya gharama nafuu, linahitaji rasilimali kidogo na ni rahisi kuwapatia chanjo wananchi.

Linawezesha kutekeleza kampeni za kuwafuatilia watu wa rika mbalimbali, kupunguza changamoto zinazohusishwa na kuwatafuta wasichana ili kuwapatia dozi yao ya pili na kuruhusu rasilimali fedha na watu kuelekezwa kwenye vipaumbele vingine vya afya.

Saratani ya shingo ya kizazi imekuwa ikijulikana kama 'muuaji wa kimyakimya' na anayeweza kabisa kuzuilika.

Zaidi ya asilimia 95 ya saratani ya shingo ya kizazi husababishwa na HPV inayoenezwa kutokana na zinaa, ambayo ni aina ya nne ya saratani kwa wanawake duniani huku asilimia 90 ya wanawake hao wakiishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi
PAHO/WHO
Chanjo ya HPV hupatiwa kwa wasichana ili kuepusha saratani ya kizazi. Pichani ni nchini Brazil msichana akipatiwa chanjo hiyo ambayo hutolewa kwa wanafunzi wa shule za umma na binafsi

Sasa unahitajika utashi wa kisiasa

Saratani ya shingo ya kizazi ni ugonjwa unaoelezwa kutokana na ukosefu wa usawa wa ufikiaji wa chanjo.

Pendekezo jipya la SAGE linaungwa mkono kupunguza wasiwasi uliopo juu ya kuanzishwa polepole kwa chanjo ya HPV katika programu za chanjo na pia katika utoaji chanjo ya jumla kwa watu, haswa katika nchi masikini.

Mkurugenzi mkuu msaidizi wa WHO Dk Princess Nothemba (Nono) Simelela alitoa maoni baada ya kuwasilishwa kwa mapendekezo hayo amesema, “Ninaamini kabisa kutokomezwa kwa saratani ya shingo ya kizazi kunawezekana. Mnamo mwaka 2020 Mpango wa Kuondoa Saratani ya Shingo ya Kizazi ulizinduliwa ili kushughulikia changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usawa katika upatikanaji wa chanjo. Pendekezo hili la dozi moja lina uwezo wa kutufikisha haraka kwenye lengo letu la kuwa na asilimia 90 ya wasichana waliopewa chanjo wakiwa na umri wa miaka 15 ifikapo 2030.”

Dkt Simelela ameendelea kusema kuwa unahitajika utashi wa kisiasa ili kuleta usawa katika upatikanaji wa chanjo ya HPV. “Kushindwa kufanya hivyo ni dhuluma kwa kizazi cha wasichana na wanawake ambao wanaweza kuwa katika hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.”

Mapendekezo haya mapya ya WHO yatafanyiwa mashauriano zaidi na washikadau wengine.