Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Asilimia 60 ya Watoto wachanga hawanyonyeshwi sababu ya sera za kazi-UNICEF

Masita Lemorin mwenye umri wa miaka 26 akimyonyesha mwanae mwenye umri wa miezi 4 huko Port au Prince nchini Haiti
UNICEF/Marco Dormino
Masita Lemorin mwenye umri wa miaka 26 akimyonyesha mwanae mwenye umri wa miezi 4 huko Port au Prince nchini Haiti

Asilimia 60 ya Watoto wachanga hawanyonyeshwi sababu ya sera za kazi-UNICEF

Afya

Sera zilizo rafiki kwa masuala ya familia ni muhimu katika kuhakikisha idadi ya watoto wachanga wanaonyonyeshwa katika miezi sita ya mwanzo ya maisha yao inaongezeka kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF.

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo ikianza wiki ya unyonyeshaji duniani inasema unyonyeshaji una faida kubwa kwa mama na mtoto ikiwemo uimarishaji wa afya ya akili katika maendeleo ya mtoto, kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa, kupunguza hatari za utipwatipwa, kupunguza gharama za huduma kwa mtoto na pia kuwalinda kina mama wanaonyonyesha dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi na ya matiti.

Pamoja na faida zote hizo UNICEF inasema bado sera za kuunga mkono unyonyeshaji kama vile likizo yenye malipo kwa wazazi na mapumziko ya kunyonyesha hazipo kwa kina mama wengi kote duniani.

Akisistiza hilo mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Henrietta Fore amesema “Sehemu nyingi za kazi duniani zinawanyima kina mama msaada wanaohitaji kuweza kunyonyesha, tunahitaji kuwekeza kwa kiasi kikubwa katikalikizo za malipo na msaada utakaowaweesha kina mama kunyonyesha katika maeneo yote ya kazi ili kuongeza kiwango cha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kote duniani.”

Bi. Fore ameongeza kuwa "faida za kiafya, kijamii na kiuchumi za unyonyeshaji zinajulikana na kukubalika kote duniani, lakini bado Karibu asilimia 60 ya Watoto wachanga hawanyonyeshwi katika miezi sita ya mwanzo iliyopendekezwa”.

 Hali halisi

Kwa mwaka 2018 UNICEF inasema ni watoto 4 tu kati ya 10 walionyonyeshwa maziwa ya mama katika miezi sita ya mwanzo ya maisha yao sawa na asilimia 41 ya watoto wote. Nchi zinazoendelea ndio zinaongoza kwa unyonyeshaji huo Rwanda ikishika nafasi ya kwanza kwa asilimia 86.9, ikifuatiwa na Burundi asilimia 82.3, Sri Lanka asilimia 82, Visiwa vya Solomon asilimia 76.2 na Vanuatu asilimia 72.6. Utafiti pia unaonyesha kuwa watoto katika maeneo ya vijijini wana kiwango kikubwa cha kunyonyeshwa kuliko mijini

Nchi za kipato cha juu na cha wastani wana viwango vidogo vya unyonyeshaji

Takwimu za UNICEF zinaonyesha kuwa nchi za kipato cha juu na cha kati viwango wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika miezi sita ya mwanzo ya maisha ya mtoto ndiovya chini Zaidi vikiwa ni asilimia 23.9 hivi sasa vikiwa vimepungua kutoka asilimia 28.7 mwaka 2012.

Mama akimnyonyesha mwanae huko Ukraine wakati wa warsha mahsusi ya unyonyeshaji watoto wakati wa dharura, warsha iliyoandaliwa na UNICEF. (2015)
UNICEF/Zavalnyuk
Mama akimnyonyesha mwanae huko Ukraine wakati wa warsha mahsusi ya unyonyeshaji watoto wakati wa dharura, warsha iliyoandaliwa na UNICEF. (2015)

 

Unyonyeshaji wakati wa kazi unasaidia

Fursa ya mapumziko wakati wa saa za kazi ili kunyonyesha au kukamua maziwa kwa kina mama wanaonyonyesha na mazingira rafiki ya unyonyeshaji kama vile kuwa na sehemu maalum kwa ajili ya wanaonyonyesha vinawasaidia kina mama kuendelea kuwapa Watoto maziwa ya mama pekee katika miei sita ya mwanzo ya maisha yao.

Kina mama wanaofanya kazi hawapati msaada wa kutosha

Duniani kote UNICEF inasema ni ailimia 40 tu ya wanawake wenye Watoto wachanga kote duniani wanaopata hata ile likizo ya msingi ya uzazi wakiwa kazini. Na pengo ni kubwa Zaidi miongoni mwa nchi za Afrika ambako wanawake wanaopata likizo hiyo wakiwa kazini ili waendelee kunyonyesha watoto wao ni asilimia 15 tu.

Nchi chache sana zinazotoa likizo ya malipo kwa wazazi

Sera ya shirika la kazi duniani ILO kuhusu likizo ya uzazi inasema angalau kuwe na likizo ya wiki 14 yenye malipo ya likizo ya uzazi huku nchi zikihimizwa kutoa wiki 18  pamoja na msaada kazini , lakini hadi sasa ni asilimia 12 tu ya nchi zote duniani ndizo zinazotoa likizo hiyo yenye malipo.

Sera mpya ya UNICEF iliyotangazwa mwaka huu kuhusu likizo ya uzazi inapendekeza miezi sita ya likizo yenye malipo kwa wazazi wote kwa jumla na kati ya miezi hiyo wiki 18 zitengwe kwa ajili ya kina mama. Na inapendekeza kwa serikali na makamouni ya biashara kutoa angalau miezi 9 ya jumla likizo kwa wazazi.

Likizo ndefu ya uzazi unyonyeshaji zaidi

Utafiti wa hivi karibuni wa UNICEF umebaini kwamba wanwake wanaopata likizo ya uzazi ya miezi sita au zaidi takribani asilimia 30 wanaendelea na unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee kwa Watoto kwa angalau miezi sita.

Unyonyeshaji nimuhimu kwa mama na mtoto

Kuongeza kiwango cha unyonyeshaji kwa mujibu wa shirika la UNICEF kutazuia vifi 823,000 kila mwaka vya Watoto wa chini ya umri wa miaka mitano na vifo 20,000 kila mwaka vitokanavyo na saratani ya matiti kwa kina mama.

Idadi ndogo ya watoto wananyonyeshwa pinditu wazaliwapo

Kwa mujibu wa takwimu mpya za UNICEF kwa mwaka 2018 chini ya nusu ya watoto wote duniani au asilimia 43 ndio walioweza kunyonyeshwa katika saa ya kwanza ya uhai wao baada ya kuzaliwa hatua ambayo ni muhimu katika kumjengea mtoto kinga ya mwili na kumsaidia mama kujiweka tayari kuendelea kunyonyesha mwanaye kwa muda mrefu. Maziwa ya mama kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO ni zaidi ya chakula kwa mtoto, pia ni dawa ya kumkinda ma magonjwa mbalimbali na kifo.

Unyonyeshaji ni uwekezaji

Endapo kiwango cha juu cha unyonyeshaji kitafikiwa duniani, UNICEF inasema kitapunguza gharama za huduma za afya duniani kwa dola bilioni 300. Wiki ya unyonyeshaji duniani kuadhimishwa kila mwaka kuanzia Agosti 1-7.