Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ufugaji samaki haujatuepusha tu na janga la tabianchi, bali umebadili maisha yetu: Christine Mbura

Christine, mfugaji wa samaki amabye ni mnufaika wa mradi wa Umoja Self-Help Group na Mradi wa Maendeleo ya Pwani ya Kenya (KCDP).
UNIS Nairobi
Christine, mfugaji wa samaki amabye ni mnufaika wa mradi wa Umoja Self-Help Group na Mradi wa Maendeleo ya Pwani ya Kenya (KCDP).

Ufugaji samaki haujatuepusha tu na janga la tabianchi, bali umebadili maisha yetu: Christine Mbura

Tabianchi na mazingira

Janga la mabadiliko ya tabianchi katika eneo la Kibokoni, Kaunti ya Kilifi nchini Kenya lilipindua maisha ya mamia ya wavuzi ambao hakuna kazi nyingine waliyoifanya kwa miaka nenda miaka rudi isipokuwa uvuvi. 

Janga hilo liliwaaathiriki kiuchumi na kimaisha na pia kuwakatisha tamaa hadi pale mradi wa ufugaji samaki kwa kutumia mabwa ulipowasili katika kaunti hiyo na kubadili kabisa maisha ya wavuvi.

Mradi huo wa ufugaji samaki ulio chini ya mwamvuli wa Umoja Self-Help Group unapigwa jeki na Mradi wa Maendeleo ya Pwani ya Kenya (KCDP) ambao ni mradi wa maendeleo wa sekta mbalimbali unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF).

Hivi sasa  jamii hiyo ina mabwawa 17 ya samaki yanayozalisha samaki aina ya milkfish, kamba, kaa, sandfish, rabbitfish na perege au tilapia.

Mradi una zaidi ya wanachama 40 na umekuwa ukifanya kazi kwa zaidi ya muongo mmoja. 

Naibu Mkurugenzi wa kitengo cha habari cha Umoja wa Umoja wa Mataifa jijini Nairobi Kenya UNIS, alifunga safari hadi Kibokoni na kuzungumza na mmoja wa wavuvi waliofaidika na mradi huo Bi. Christine Sori Mbura ambaye anasema kabla ya mradi maisha yalikuwa magumu sana lakini sasa” Maisha yamebadilika kabisa, na jamii imefaidika sana na huu mradi, mwenzangu wameweza kusomesha watoto na wengine wamepata kazi na hata mimi nimeweza kusomesha wanangu na nilikuwa nadunduliza kidogokidogo nitachopata kwenye mradi sasa nimeweza kununua mbuzi na ng’ombe na shamba. »

Christine na wafugaji wenzake wa samaki ambao ni waufaika wa mradi wa Umoja Self-Help Group na Mradi wa Maendeleo ya Pwani ya Kenya (KCDP).
UNIS Nairobi
Christine na wafugaji wenzake wa samaki ambao ni waufaika wa mradi wa Umoja Self-Help Group na Mradi wa Maendeleo ya Pwani ya Kenya (KCDP).

Kilichowasukuma kuingia katika mradi

Mradi huu ulianza miaka 11 iliyopita na Christine anasema haukuwa kwa kupenda kwao bali mazingira yaliwalazimisha » Ilifika wakati samaki walitoweka baharini, creek ilikuwa haina tena samaki. Wakati wa mvua tunapata samaki wengi lakini mvua ikikata basi na samaki wanakata,hali hiyo ilikuwa ngumu sana kwetu kama wavuvi. »

Hivyo wazo la kuanzisha mabwawa ya samaki kukabiliana na changamoto hiyo ya mabadiliko ya tabianchi ilikuwa muziki masikioni mwa wavuvi hao, wakaukumbatia mradi na kujiunga katika kikundi kwani waliamini Umoja ni nguvu kwao.

Walianza kidogokidogo na kisha serikali ya kaunti ikawapiga jeki kupitia KCDP na kuwaanzishia mabwa mengine ambayo ni makubwa na yenayozalisha samaki wengi zaidi.

Faida na umuhimu wa mradi huo

Kwa mujibu wa Christine wana kikundi cha Umoja self Help wameufurahia mradi huo kwa kuwa unawapatia kipato endelevu, kwani tofauti nailivyokuwa awali kwa samaki wa kuvua baharini ambao ni wa msimu, lakini mabwa ya samaki ni biashaya ya mzunguko wa mwaka mzima.

"Tunavuna samaki mara tatu kwa mwaka, mwezi wa kwanza, wa pili na wa tatu na baada ya hapo tunaweza tena samaki wadogo kisha wanakuwa hivyo tanaweza kuvuna na kuuza samaki hao kama tilapia na milk fish mara tatu kwa mwaka na tilapia wanatupa faida kubwa kwani wanazaliana sana."

Ukiacha kipato ambacho kinawasaidia kiuchumi pia katika kikundi hicho cha Umoja self- Help wana utaratibu wa kukopeshana fedha ambao huwasaidia wanachama kufanya masuala mengine binafsi ya maendeleo kama kujenga, kununua mashamba na hata kusomesha watoto.

Fursa ya kuanzisha biashara nyingine

Kama walivyo wavuvi wengine Christine na wenzake baada ya kupata faida kubwa katika kikundi  wanawaza kupanua wigo wa biashara yao ambapo mbali ya kufuga samaki sasa wanataka kuanzisha mgahawa ambao sio tu utatoa ajira kwa jamii ya wavuvi hao lakini utawaletea watu wengi zaidi katika jamii yao watakaokuja kuchuuza samaki na kula chakula 

"Mgahawa huo utakuwa nafasi ya watu kufuata samaki Kilifi na si samaki kuwafuata waliko. Na kwa maoni yangu endapo tutapata ufadhili zaidi basi tunaweza kujenga na kuanzisha hata shule ambayo watu wataweza kutoka sehemu mbalimbali na kuja hata kujifunza ufugaji wa samaki."