Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mradi wa kuboresha makazi duni nchini Kenya waleta nuru katikati ya kiza cha Corona

Vioski vya maji safi na salama katika eneo la Mtwapa kaunti ya Kilifi nchini Kenya vimesaidia kupunguza kusambaa kwa virusi vya Corona COVID-19
© UN-Habitat/Kirsten Milhahn
Vioski vya maji safi na salama katika eneo la Mtwapa kaunti ya Kilifi nchini Kenya vimesaidia kupunguza kusambaa kwa virusi vya Corona COVID-19

Mradi wa kuboresha makazi duni nchini Kenya waleta nuru katikati ya kiza cha Corona

Afya

Nchini Kenya mradi wa kuboresha maeneo ya makazi duni, PSUP, unaotekelezwa kwa ubia kati ya shirika la Umoja wa Mataifa la makazi, UNH-Habitat na shirika la kiraia, SHOFCO umesaidia kuimarisha maisha ya wakazi wa eneo la mabanda la Majengo katika kaunti ya Kilifi,  hasa wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19. 

 

Mradi wa UN-HABITAT nchini Kenya unaosaidia wasio na makazi katika kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona.
UN News/ Jason Nyakundi
Mradi wa UN-HABITAT nchini Kenya unaosaidia wasio na makazi katika kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona.

Mradi huo ulioanzishwa mwezi Machi mwaka 2020, ulihusisha utekelezaji wa hatua za dharura kwa lengo kuzuia maambukizi ya Corona na wakati huo huo kuinua kipato cha wakazi wa eneo hilo

Miongoni mwa wanufaika ni Swalehe Amani Mbarouk mwenye ulemavu wa kutoona lakini hali hiyo haimzuii kuendesha biashara ya kuuza mkaa hapa Majengo ili angalau apate fedha kiasi za kujipatia mlo. 

Kama wakazi wengine wa mji huu wa Pwani, Bwana Mbarouk mwenye umri wa miaka 75 naye anahaha kujipatia kipato hasa wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19. 

Ili kuzuia kusambaa kwa Corona, UN-Habitat kupitia mradi wa kuimarisha makazi duni, PSUP na SHOFCO walianza mpango wa kutengeneza vituo vya kunawa mikono kwa maji na sabuni, ambacho kituo kimoja anakiendesha Bwana  Mbarouk na kujipatia kipato kidogo akisema, 
“nashukuru sana kwa mradi huu  uliokuja wameniletea tanki na hili shirika nalishukuru sana, limenisaidia sana kwa vile mimi ni mlemavu. Nachukua tenki hili kama langu, kusaidia jamii, kusaidia umma.” 

Mahali pa kuonyeshea mikono pametengenezwa na UN-Habitat kwenye makazi duni ya Kibera Nchini Kenya.
© UN-Habitat /Julius Mwelu
Mahali pa kuonyeshea mikono pametengenezwa na UN-Habitat kwenye makazi duni ya Kibera Nchini Kenya.

Kama ilivyo kwa Bwana Mbarouk, wakazi wengi wakiwemo wafanyabiashara na wachuuzi sokoni hapa Majengo wamechukua hatua kukabiliana na changamoto za ukali wa maisha zitokanazo na COVID-19,  
Wananchi nao wamejitokeza kwa kushirikiana na serikali ya kaunti ya Kilifi kupitia mradi huo wa PSUS na SHOFCO kutumia matenki ya maji, sabuni na vitakasa mikono kuhakikisha janga la Corona linadhibitiwa ipasavyo. 

Ingawa hivyo hata kabla ya ujio wa Corona, wako ambao walkuwa wanajitolea kusaidia jamii katikati ya makazi haya duni yaliyogubikwa na changamoto za kiuchumi na kijamii na miongoni mwao ni Mishi Rama Mbete ambaye amekuwa akijitolea kusaidia jamii kukabiliana na masuala ya afya. Wakati huu wa COVID-19 mchango wake umeongezeka thamani. 

Kwa wiki kadhaa amekuwa akielimisha jamii kuhusu virusi vya Corona huku akikusanya takwimu kuhusu hali zao za kiafya huku akisambaza kwa wanawake taulo za kike.  Bi. Mbete anasema, “kila mtu alikuwa anatoka na boksi 6, na kila boksi lilikuwa na sabuni 72, halafu tunabeba na vitakasa mikono 72. Kila mtu tunampatia sabuni moja na kitakasa mikono chupa moja. “ 
Licha ya mwelekeo mzuri, Bi. Mbete anasema haikuwa rahisi mwanzoni kwa kuwa wananchi walikuwa hawaamini uwepo wa Corona. 

Mgao wa maji bure kwa wakazi

Matenki ya kunawa mikono kwa maji na sabuni hayana faida bila maji, hivyo mradi ulisambaza bure maji safi kwa kutumia magari. Kila siku magari yalipeleka maji eneo la Mipingu, kilometa 20 kutoka Majengo ambako kila gari lilikuwa na ujazo wa lita 10,000 za maji. Wengi wa wakazi wa eneo hilo chanzo cha maji ni kisima ambacho maji ni ya chumvi na machafu. Kwa hiyo maji yanayoletwa ndio mkombozi wao. 

Msururu wa madumu ya maji hupokea magari haya kila uchao na ni furaha kwa wanawake na watoto wa kike ambao ndio wanaobeba jukumu la kuteka maji. 

Picha ya maktaba ikionesha wakazi wa mitaa ya mabanda ya Kibera Nairobi Kenya wakipatiwa sabuni na maji kwa ajili ya kunawa mikono ili kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.
© UNICEF
Picha ya maktaba ikionesha wakazi wa mitaa ya mabanda ya Kibera Nairobi Kenya wakipatiwa sabuni na maji kwa ajili ya kunawa mikono ili kusaidia kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Mradi huu ni baraka kwetu

Wanufaika wengine ni wakazi wa kitongoji cha Mzambarauni katika kaunti ya Kilifi ambapo Eunice Kazungu kiongozi wa kijiji anafunguka akisema maji wanayoletewa bure ni baraka kwao kwa kuwa ugonjwa wa Corona umetowesha ajira . Eunice anasema,“hapa ni nyumbani, shughuli zangu nafanya hapa. Lakini Corona ilivyoingia ilituathiri sana. Na kuanzia Corona ilivyoanza ilikuwa shida chakula, shida ya maji, shida ya kila kitu, na hata pesa tulikuwa hatuna. Lakini kuanzia huu msaada wa maji ulivyoingia pia tulikuwa tunapata msaada kwa hayo maji, kwa kuwa maji ilikuwa ni tatizo. Sasa tunapata msaada na zaidi ya hayo yote tunawaomba hata kama kuna msaada mwingine mzidi kutuletea ili tuweze kujikimu kimaisha.” 
Msingi wa mradi wa PSUP ni kituo cha kijamii kilichoko Majengo ambako wanajamii hupatiwa mafunzo ili wajengewe uwezo wa kushiriki vyema kwenye mradi huo hususan wanawake na wasichana.