Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatutumii tena mkoko kama kuni au kujengea nyumba- Wanufaika mradi wa Vanga Blue Forest

Boti ikiwa imeegeshwa wangwani huko mji wa Vanga, kaunti ya Kwale nchini Kenya.
UN/ Thelma Mwadzaya
Boti ikiwa imeegeshwa wangwani huko mji wa Vanga, kaunti ya Kwale nchini Kenya.

Hatutumii tena mkoko kama kuni au kujengea nyumba- Wanufaika mradi wa Vanga Blue Forest

Tabianchi na mazingira

Wakati mkutano masuala ya bahari ukiendelea mjini Lisbon, nchini Ureno, Kenya ambayo ni mwenyeji mwenza wa mkutano huo inajiweka sawa kuwa na sauti kubwa zaidi kwenye umiliki na matumizi ya mali asili za bahari.

Wakaazi wa maeneo ya pwani ya Kenya wako mstari wa mbele kulinda mazingira ya ufukweni kupitia miradi mbalimbali kwani ndio wa kwanza kuathiriwa na mafuriko pale kina cha bahari kinapoongezeka.

Mradi wa Vanga Blue Forests ambao kwa kiasi fulani unafadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP ulianzishwa takribani miaka miwili iliyopita na kusuasua pale janga la COVID 19 lilipozuka lakini kwa sasa harakati zinaendelea.

Mradi huu unajikita katika juhudi za kuzuia ukataji wa misitu ya mikoko ambayo inahitajika katika mazingira ya ufukweni kama mazalia ya samaki, vyanzo vya mvua na kubwa zaidi katika biashara kufyonza hewa ya ukaa na kuizuza.

Mwandishi wetu wa Kenya Thelma Mwadzaya amezuru eneo hilo kushuhudia juhudi zinazofanyika kulinda mazingira ya bahari na kuinua kipato cha wananchi wa Vanga na maeneo Jirani.

Mikoko katika mji wa Vanga, kaunti ya Kwale nchini Kenya ni mazalia muhimu ya samaki.
UN/ Thelma Mwadzaya
Mikoko katika mji wa Vanga, kaunti ya Kwale nchini Kenya ni mazalia muhimu ya samaki.

 

Mikoko ina uwezo wa kufyonza hewa ya ukaa mara 10 zaidi ikilinganishwa na miti ya nchi kavu.

Mwanaharusi Mwafrika ni mratibu wa mradi wa Vanga blue forest na anasimulia mradi huo unavyowafaidi,”Tumefanikiwa kufyonza tani zaidi ya tano ya hewa ya ukaa mpaka sasa. Hilo limeleta tofauti katika mabadiliko ya tabianchi. Mwanzo wakaazi hawakuelewa umuhimu wa kuhifadhi mikoko lakini sasa kwavile wameona matokeo ya harakati hizo sasa wamebadili mitazamo.”

Mradi wenyewe wa Vanga Forest Mradi wa Vanga blue forest wa kuhifadhi mikoko unazihusisha jamii Kwa karibu na kuwaasa kutoikata. Mizizi ya mikoko ni mirefu na ina uwezo mkubwa wa kuuzuia mchanga na kupunguza mmomonyoko ufukweni .

Hamadi Juma Tsunusi ni naibu mratibu wa mradi wa Vanga blue forest na anafafanua wanakozikita juhudi zao,”Mikoko imekuwako hapa Vanga na wakaazi wamekuwa wanayo miche.Sisi kama Vanga Blue Forests tunawashika mkono wanakijiji kwa kuinunua ili wapate hela kwani tayari inakuwa mikoko ipo.”

Wakazi elfu 9 wanashiriki katika mradi Mradi huu unawashirikisha wanakijiji wa Vanga, Jimbo na Kiwegu. Kiasi cha wakaazi alfu 9 wa eneo Hilo wanahusika moja kwa moja. Vijiji hivyo vitatu vinaunda shirika la VAJIKI la kuhifadhi misitu ya kijamii ya mikoko na bara.

Harith Mohamed ni mwenyekiti wa VAJIKI na anaelezea uhusiano wa mikoko na misitu ya bara,” mikoko ina uwezo mkubwa sana wa kufyonza hewa kaa ikilinganishwa na miti ya bara.Hata hivyo ni muhmu kuhifadhi misitu ya mikoko na ya bara kwani wanakijiji wataweza kupata mbao na bidhaa nyengine kwa haraka zaidi kwasababu inakuwa kwa kasi. Dhamira yetu ni kila mwanakijiji apate manufaa na faida za kuhifadhi miti yote.”

 

Mradi wa kurejesha mikoko huko Vanga, kaunti ya Kwale nchini Kenya umesaidia kuepusha eneo hilo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.
UN/ Thelma Mwadzaya
Mradi wa kurejesha mikoko huko Vanga, kaunti ya Kwale nchini Kenya umesaidia kuepusha eneo hilo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.

Faida za mradi kwa jamii

Baadhi ya faida hizo za mradi ni shule ya sekondari ya Juma Boy ya Vanga ambayo ilipata maabara mpya iliyojengwa na hela za mauzo ya hewa ukaa katika msimu wa mwanzo wa mradi. Kwa wakaazi wa Jimbo na wavuvi walipata boti ya kisasa ukizingatia wengi wanatumia mbinu za kiasili kusafiri. Kadhalika shule ya chekechea ya jimbo iliyokuwa majini sasa imesimama baada ya ukuta wa ufukweni kujengwa kuzuia maji ya bahari yanapojaa. Kijiji cha jimbo hilo sasa kina majaruba ya miche alfu 30.

Mikoko inatumika kama kuni na mbao za ujenzi, dawa, makazi na mazalia ya samaki na viumbe vyengine vya baharini pamoja na kulinda fukwe yanapokuja mawimbi makubwa. Masika Mohamed Ali ni kiongozi wa kijiji cha Jimbo na anakiri kuwa “mradi wa mikoko ni mzuri kwani awali wakaazi walijenga kwa mikoko lakini tangu tupate usaidizi tunajikanya sana tusiikate.

Kwa kwenda mbele watakaojenga naamini watatumia matofali au mawe ili kuinusuru mikoko.Tumefanyia shule ya chekechea ukarabati na pia kuikamilisha nyumba ya mwalimu kwa hela za mradi.Kwahiyo ni mradi mzuri.”

Samaki waliopotea warejea Elimu ya kuhifadhi mikoko imeleta tija kwani wavuvi wanasimulia kuwa wameshaanza kuona mabadiliko. Aina za samaki waliokuwa wame anza kuadimika Sasa wameanza kurejea. Kadhalika idadi ya samaki pia inaripotiwa kuongezeka japo hakuna takwimu kamili.