Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tusipoilinda bahari tunaathiri kizazi cha sasa na vijavyo: Wananchi wa Vanga Kenya 

Wavuvi pwani ya Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Wavuvi pwani ya Kenya.

Tusipoilinda bahari tunaathiri kizazi cha sasa na vijavyo: Wananchi wa Vanga Kenya 

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni siku ya bahari duniani Umoja wa Mataifa imeichagiza dunia kuchukua hatua Madhubuti ili kuhakikishwa inalindwa kwa ajili ya maslhai ya kizazi cha sasa na kijacho kwani bahari sio tu inahakikisha uhakika wa chakula kwa mamilioni ya watu , bali pia ni moja wa muajiri mkubwa na inachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la dunia la kila mwaka.  

Mwandishi wetu wa Kenya Thelma Mwadzaya amekwenda Vanga Pwani ya Kenya kushuhudia kinachofanywa na jamii ya wavuvi katika kuhakikisha bahari na rasilimali zake zinalindwa. 

Asilimia 70% ya dunia ni bahari na inahifadhi viumbe vya aina na mifumo tofauti ya uhai. 

Bahari ina uwezo mkubwa wa kusawazisha hali ya hewa kadhalika kuziwezesha jamii za pwani kuhimili athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. 

Kauli mbiu ya siku ya bahari kwa mwaka 2022 ni kuishajiisha jamii kuwa na juhudi za pamoja za kuihifadhi. 

Misitu ya mikoko ina uwezo mkubwa wa kufyonza hewa kaa na kusafisha mazingira.Mkoko mmoja unaweza kusafisha hewa mithili ya miti 10 ya nchi kavu na pia kuzuwia nguvu na kasi ya mawimbi ya bahari.  

Wadi ya Vanga iko mwisho wa mpaka wa Kenya na Tanzania kwenye bahari ya Hindi, Omar Rico ni mkaazi wa eneo la pwani la Vanga na anaelezea umuhimu wa mikoko ufukweni na anaelezea kuwa ,”mikoko iliwanusuru wakaazi wa Vanga wakati janga la Tsunami lililopoyaponda maeneo ya pwani miaka michache iliyopita.Mikoko inaipunguza kasi ya mawimbi na dhoruba zake na tsunami ilipokuja tulisamilika kwasababu ya hilo.” 

Uchafuzi wa maeneo ya  bahari wa taka za plastiki, Vanga Kilifi Kenya.
UN News/ Thelma Mwadzaya
Uchafuzi wa maeneo ya bahari wa taka za plastiki, Vanga Kilifi Kenya.

Samaki na taka za plastiki 

Kitisho kikubwa ni uchafuzi wa bahari hasa taka ngumu zisizooza.Taka za plastiki zinaweza kuwasakama samaki na viumbe vya bahari au hata maambukizi.  

Ili kupata ufahamu wa mfumo wa utegemeano wa mazingira ya bahari ni muhimu kupata elimu mwafaka. Mbali ya kufyonza hewa kaa, mikoko ina mizizi mirefu inayoishika na kuizuwia michanga kumomonyoka. 

Maeneo hayo ndio mazalia ya samaki na viumbe vya bahari.Goodluck Mbaga ni mlinzi wa mazingira na mkaazi wa pwani huko Kilifi na anaelezea hatari ya kuchafua mazingira ya baharini.”Taka za plastiki ni hatari kwani samaki wanaweza kudhania kuwa ni chakula.Mfano mipira ya condom ikielea majini inaweza kuonekana kama aina fulani ya viumbe vya bahari.Endapo unamvua samaki yule na unapompasua unakuta ana mipira ya condom inakuwa ni taswira ya kutamausha kwa kweli.Lazma tuhifadhi mazingira yetu ya baharini na tuyaache nadhifu wakati wote.” 

Boti Vanga kaunti ya Kilifi, pwani ya Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya.
Boti Vanga kaunti ya Kilifi, pwani ya Kenya.

Mikoko na Matumbawe 

Mikoko ina mchango mkubwa katika kuziwezesha jamii kuhimili athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. Maji ya bahari yanafyonza gesi nyingi zaidi ya hewa ukaa ikilinganishwa na inayotolewa na viumbe viishivyo ndani yake. 

Mikoko inazilinda fukwe kwa kuzuwia mmonyoko wa ardhi, kuzuwia athari za mafuriko baharini, ongezeko la kina cha bahari na kuikinga miamba ya matumbawe ambayo ni mazalio na mapango ya samaki. 

Katana Charo Hinzano ni mlinzi wa mazingira na anausisitizia umuhimu wa kukifunza kizazi kijacho kuhusu uhifadhi wa bahari na anasisitiza kuwa, “Kila siku ya bahari tunatenga muda wa kuwafundisha watoto hasa wa shuleni na wavuvi pia kuhusu umuhimu wa kuhifadhi matumbawe.Baadhi ya wavuvi wanadhani kwamba matumbawe ni kitu tu cha baharini na hakina uhai.Lau matumbawe yakivunjika na kuharibiwa, mazalio ya samaki yanakuwa yamevurugwa na hapo basi ukiingia majini hutaona samaki wowote,”. 

Siku ya bahari hii leo inaangazia juhudi za pamoja za kuihifadhi bahari. Uhifadhi wa mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi za baharini vyote vinachangia kubadili athari za mabadiliko ya tabia ya nchi.