Ubinadamu lazima ushinde vita dhidi ya vita - Zambia
Ubinadamu lazima ushinde vita dhidi ya vita - Zambia
Wakati ulimwengu kwa sasa unakabiliana na changamoto lukuki zikiwemo vita, athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa chakula, Waziri wa Mambo ya nje na uhusiano wa kimataifa wa Zambia Stanley Kakubo amesema gharama ya vita kwa ubinadamu ni kubwa.
Akihutubia katika Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA78 jijini New York Marekani Kakuba amesema “Gharama za vita kuanzia nchini DRC, huko Sudan mpaka Ukraine imepelekea wanawake na watoto wengi kuyakimbia makazi yao na kitu kibaya zaidi wanawake kwa wanaume wengi kupoteza maisha yao.”
Na ili kutoka katika hali hiyo “Ubinadamu lazima ushinde vita dhidi ya vita.” Amesema Waziri huyo wa Zambia na kuongeza kuwa kamwe “hatupaswi kupoteza mbio za kuikomboa sayari yetu kwani kuharibu sayari yetu ni kuharibu uwepo wetu.”
Matumizi ya AI
Kuhusu maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na matumizi ya akili mnemba Zambia imesema dunia inapaswa kukumbatia maendeleo hayo na nchi zisaidiane kupeana taaluma zaidi ili kuboresha hali za wananchi.
“Embu fikiria kutumia AI kupelekea dawa za kuokoa Uhai wa bibi ambaye anaonekana amesahaulika huko vijijini barani Afrika, au mabadiliko makubwa tunayoweza kuyafikia katika utunzaji wa udongo wenye rutuba nchini Zambia kwa kutumia teknolojia sahihi ya umwagiliaji.”
Akiendelea na hotuba yake Waziri huyu wa mambo ya nje wa Zambia amesema kadri sekta ya teknolojia ya mawasiliano inavyozidi kukuwa anaona mwanga mpya kwa siku zijazo katika ushirikiano wa kidijiyali.
“Sasa inawezekana kwa Profesa wa chuo kikuu cha Harvard (Marekani) kuwafundisha wanafunzi walioko Kenya, Malawi au Chuo Kikuu cha Lusaka.”
Baraza la Usalama la UN
Masuala mengine mbalimbali yamezungumzwa katika hotuba ikiwa ni pamoja na marekebisho ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo Zambia imetaka kuwepo na uwakilishi wa kudumu wa Afrika.
“Marekebisho hayo si tu yataongeza uhalali wa Baraza la Usalama bali pia yatakomesha dhulma ya kihistoria.”
Kutazama video ya hotuba ya Zambia katika UNGA78 bofya hapa.