Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kilichojiri kwenye mkutano maalum kuhusu Sudan kando ya UNGA78

Hali ya afya nchini Sudan inazidi kuzorota kutokana na mzozo nchini humo
© UNHCR
Hali ya afya nchini Sudan inazidi kuzorota kutokana na mzozo nchini humo

Kilichojiri kwenye mkutano maalum kuhusu Sudan kando ya UNGA78

Amani na Usalama

Tangu kuanza kwa mgogoro mpya nchini Sudan, sasa ni miezi sita, hali ya kibinadamu inaendelea kuwa mbaya na kutishia kuleta msukosuko katika Ukanda mzima.

Leo kandoni mwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA78 kumefanyika mkutano maalum ukiwaleta pamoja serikali na mashirika ya kimataifa ili kuanisha gharama ya kibinadamu kwa kutochukua hatua na kutoa wito wa suluhu ya mzozo huo lakini pia kusaidia janga la kibinadamu na hatua kwa wakimbizi.

Haya ndio yaliyosemwa katika mkutano huo na wadau mbalimbali walioshiriki.

Wafadhili wa msaada wa kibinadamuwanajitahidi kutoa msaada wakati wowote na popote inapohitajika, #NoMatterWhat..
OCHA/Giles Clarke
Wafadhili wa msaada wa kibinadamuwanajitahidi kutoa msaada wakati wowote na popote inapohitajika, #NoMatterWhat..

Kuwafikia waathirika ni mtihani mkubwa

Msaidizi wa Katibu Mkuu na mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura Martin Griffiths amesema "Mgogoro nchini Sudan unazidi kuwa hatari siku hadi siku, na mahitaji yanaongezeka. Jitihada zisizochoka zinafanywa kufikisha misafara ya misaada kuvuka mipaka hadi Darfur na kuvuka maeneo ya migogoro ndani ya nchi, lakini mchakato huo ni wa kuchosha, wa ukiritimba na wa hatari. kilio chetu ni fursa ya ufikiaji usio na vikwazo na salama kwa watu ambao tunapaswa kuwafikia. Tunafanya kazi kwa bidii kupanua wigo wa ufikiaji wa msaada wa kibinadamu, lakini tunahitaji mchakato wa kisiasa kumaliza mapigano na kuanza kujenga Sudan mpya.”

Mamilioni wamelazimika kufungasha virago

Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR, Filippo Grandi, amesema “Mamilioni ya watu tayari wamelazimika kuhama makwao kutokana na vita nchini Sudan, na kila siku zaidi na zaidi wanalazimika kukimbia kwenda kutafuta usalama. Wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu ili kuwaweka hai, lakini pia misaada ya dharura ya maendeleo ili kuweka mazingira na fursa za kuweza kuishi kwa heshima pale walipo hadi waweze kurejea nyumbani. Na zaidi ya yote, wanahitaji mtutu nwa bunduki kunyamaza na vita hivi visivyo na maana kukoma.”

Jumuiya ya kimataifa lazima iongeze msaada kwa Sudan

Waziri wa nchi wa ushirikiano wa kimataifa wa Qatar, Mheshimiwa Bi. Lolwah Rashid Al-Khater, amesema “Tuna wasiwasi mkubwa kuhusu hali mbaya zaidi ya kibinadamu nchini Sudan. Uharaka wa kutatua hali hii ni mkubwa sana. Ni muhimu kwamba jumuiya ya kimataifa iongeze juhudi zake mara moja ili kutoa msaada muhimu wa kibinadamu kwa watu wa Sudan, ikiwa ni pamoja na waliokimbia makazi yao na kuwa wakimbizi wa ndani na wakimbizi katika nchi jirani. Tunatoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano, na kwa nguvu zote za kisiasa kushiriki katika mazungumzo na njia za amani kutatua mzozo huo. Taifa la Qatar linaunga mkono juhudi zinazoendelea za kikanda na kimataifa zenye lengo la kumaliza mzozo na kuleta utulivu kwa Sudan.”

Wakimbizi wanaokimbia mzozo nchini Sudan wawasili Renk, Sudan Kusini.
© UNOCHA/Iramaku Vundru Wilfred
Wakimbizi wanaokimbia mzozo nchini Sudan wawasili Renk, Sudan Kusini.

Kusaka suluhu kujumuishe usalama wa watoa misaada 

Msimamizi mkuu wa kituo cha misaada ya kibinadamu cha Mfalme Salman wa Saudi Arabia, Dkt. Abdullah Al Rabeeah amesisitiza haja ya kuhakikisha usalama kwa wapokea misaada na watoa misaada akisema  katika "Kutafuta suluhu za mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan ni pamoja na kupata fursa ya ufikiaji kamili na salama wa misaada na wafanyakazi, kuongeza ufadhili wa kimataifa, na kusaidia amani endelevu. Mamilioni ya wakimbizi na wakimbizi wa ndani au IDPs wanahitaji msaada wa dharura nchini Sudan na katika nchi jirani, na nchi zinazowahifadhi pia zinahitaji msaada wetu ili kushughulikia wimbi la wale wanaokimbia ghasia. Kila siku inayopita, watu zaidi na zaidi wako hatarini, lakini tukishirikiana, tunaweza kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu walio hatarini zaidi nchini Sudan. Ni jukumu letu la pamoja kufanya kila tuwezalo ili kupunguza mateso na kufanya kazi kuelekea amani na utulivu nchini Sudan."

Majirani wa Sudan hawapaswi kubeba mzigo peke yao

Waziri wa mambo ya nje wa Misri nchi ambayo inapokea mzigo mkubwa wa wakimbizi kutoka Sudan, muheshimiwa Bwana Sameh Shoukry, amesema "Nchi jirani za Sudan hazipaswi kubeba mzigo wa mgogoro huo peke yake. Kuzibebesha mzigo nchi hizo na uwezo wao wa kutoa huduma za umma kunachochea uhamiaji haramu. Tunahitaji kuzingatia kanuni ya kugawana mizigo na majukumu kwa usawa kama suluhu pekee ya kupunguza mzigo wa kibinadamu na kukabiliana na mzozo wa watu kuhama makwao kwa njia ifaayo na endelevu."

EU itaendelea kuwa mdau wamsaada Sudan

Kamishna wa Muungamo wa Ulaya EU, kwa ajili ya kusimamia migogoro, Janez Lenarčič, anesisitiza kuwa, "EU inasalia kuendelea kujitolea kutoa msaada wa kibinadamu na ulinzi kwa wale walioathiriwa na mzozo nchini Sudan na wale ambao wamekimbilia nchi jirani. Hata hivyo, ili usaidizi wetu ufanikiwe, tunahitaji fursa salama za ufikiaji wenye uhitaji, kwa wakati unaofaa na usiozuiliwa na shughuli za kibinadamu. Hili linapaswa kuhakikishwa na pande zote kwenye mzozo wakati wote, kwa mujibu wa kanuni za kibinadamu. Tukio la ngazi ya juu lililofanyika leo limeangazia masuala haya muhimu ya ufikiaji, na pia kuwakumbusha wapiganaji wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu na haki za binadamu."

Mkutano wa leo wa ngazi ya juu umeitishwa na Umoja wa Mataifa pamoja na Serikali za Misri, Qatar na Saudi Arabia, Muungano wa Ulaya na Muungano wa Afrika AU.