Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Katika enzi zilizoghubikwa na ubaguzi, mizozo na migawanyiko, diplomasia ndio suluhu pekee ya ufanisi: India

Waziri wa mambo ya nje wa India, Subramaniam Jaishankar, akihutubia kikao cha 78 cha mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Cia Pak
Waziri wa mambo ya nje wa India, Subramaniam Jaishankar, akihutubia kikao cha 78 cha mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Katika enzi zilizoghubikwa na ubaguzi, mizozo na migawanyiko, diplomasia ndio suluhu pekee ya ufanisi: India

Masuala ya UM

Waziri wa mambo ya nje wa India, Subramaniam Jaishankar, akihutubia kikao cha 78 cha mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa hii leo amesema kuwa katika wakati ambapo dunia inapitia misukosuko isiyo na kifani kuanzia mgawanyiko kati ya ulimwengu wa Mashariki na Magharibi unaoongezeka, na mvutano wa kimataifa baina ya Ulimwengu wa Kaskazini na Kusini kuzidi kuongezeka, diplomasia na mazungumzo ndio suluhisho pekee la ufanisi la kukabiliana na changamoto za sasa.

Namaste, waziri huyo wa mambo ya nje amesema kutokana na tofauti za kimuundo na maendeleo yasiyo sawa, mzigo kwa nchi za Kusini mwa dunia umeongezeka. 

Halii hii imezidishwa na mivutano na migogoro inayotokana na janga la kimataifa la COVID-19 na vita.

Ameongeza kuwa kutokana na hali hiyo hatua zilizopigwa hivi karibunizimerudishwa nyuma, changamoto kubwa zimejitokeza katika kukusanya rasilimali kwa ajili ya maendeleo endelevu, na nchi nyingi zinapata ugumu wa kujikimu kimaisha.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mustakbali wa Dunia huku tukipambana na hali hizi sasa umekuwa mgumu zaidi. Katika wakati huu, kwa hisia kubwa ya uwajibikaji, India inachukua urais wa G20."

Ameendelea kusema kuwa "Maono yetu ya dunia moja, familia moja, mustakbali mmoja yanataka kuzingatia maswala ya msingi ya wengi, sio tu masilahi finyu ya wachache."

Ameweka bayana kwamba Azimio la New Delhi katika hitimisho la G20 lilidhihirisha hisia za kupanda mbegu za ushirikiano ambao unastawisha ulimwengu, kuziba migawanyiko na kuondoa vizuizi.” 

Wakati wa wachache kufanya maamuzi na wengine kutekeleza umepita

Amesema mfumo wa kimataifa ni wa aina mbalimbali na ikiwa ni tofauti basi tofauti hizo zinapaswa kushughulikiwa.

"Siku za nchi chache kuweka ajenda na kisha zingine kufuata zimepita. Kuwasikiliza wengine na kuheshimu maoni yao si udhaifu ni msingi wa ushirikiano. Hapo ndipo juhudi za pamoja katika masuala ya kimataifa zinaweza kufanikiwa.”

Amesisitiza warizi huyo wa mambo ya nje na kuongeza kuwa kwa mpango ulioanzishwa na India, Muungano wa Afrika umepewa uanachama wa kudumu, kwenye G-20 hali ambayo bara zima limepata sauti ambayo ilihitajika kwa muda mrefu.

Jaishankar amesema hatua hii madhubuti kuelekea mageuzi ya G20 inapaswa pia kuhamasisha Umoja wa Mataifa, ambao ni shirika kongwe zaidi, kufanya Baraza la Usalama kuwa la kisasa kwani uwakilishi mpana ni hitaji la msingi la ufanisi na uaminifu.

Si vibaya kutetea maslahi binafsi

Kulingana na Jaishankar, kila nchi inataka kuelekea kwenye masilahi yake ya kitaifa, lakini India haioni juhudi hizi kama ni kinzani kwa ustawi wa ulimwengu.

Ameongeza kuwa India inatamani taifa lenye kuongoza lakini si kwa kuongeza nafasi yake bali kwa kubeba majukumu zaidi.

"India imedhihirisha hilo kupitia mpango wa chacho ya Maitri wakati wa COVID-19. Juhudi zetu kama vile muungano wa kimataifa wa sola na muungano wa miundombinu yenye mnepo dhidi ya mabadiliko ya tabianchi imepata msaada mkubwa.

Katika mlolongo huu, pia ametaja 'Mwaka wa mimataifa wa mtama', ambao umeelezwa kuwa muhimu kwa mtazamo wa kuimarisha uhakika wa chakula duniani.

Pia amesema India imeendeleza ushirikiano wa kimaendeleo na nchi 78 katika maeneo tofauti ya kijiografia, na wahudumu wa misaada wa nchi hiyo wamechukua jukumu la mstari wa mbele katika hali nyingi za maafa, likiwemo tetemeko la ardhi la hivi karibuni nchini Uturuki.

Tumepiga hatua kubwa kutekelza SDGs

Waziri huyo amesema katika upande wa utimizaji wa malengo ya maendeleo endelevuu SDGs waziri Jaishankar amesema India imepiga hatua kubwa ambayo itasaidia kuimarisha kujiamini kwa nchi zingine.

Mathalani amesema kielezo cha kimataifa cha umaskini kinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 41 nchini India wamefanikiwa kutoka katika mzunguko wa umaskini uliokithiri. 

Na hii amesema imechangiwa na hatua kubwa zilizopigwa katika ujumuishwaji katika masuala ya kifedha, chakula na lishe, afya, huduma za maji, nishati na makazi.

Pia amaendeleo ya teknolojia yamesaidia kuleta mabadiliko chanya kwa umma hasa kwa watu wenye uhitaji ukizingatia kwamba lengo la serikali ni kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kila Nyanja.