Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutaendelea kufuatilia mwenendo wa nyuklia Ukraine na kwingineko: IAEA

Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia huadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Septemba.
© ICAN/Marlena Koenig
Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Silaha za Nyuklia huadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Septemba.

Tutaendelea kufuatilia mwenendo wa nyuklia Ukraine na kwingineko: IAEA

Amani na Usalama

"Hatuendi popote, tutaendelea kufuatilia mwenendo wa nyuklia kila mahali", ni ujumbe kutoka kwa mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la nguvu ya nishati ya atomiki IAEA, Rafael Grossi, kuhusu dhamira ya shirika hilo kuendelea kufuatilia vinu vya nyuklia vya Ukraine wakati huu wa uvamizi unaoendelea wa Urusi lakini pia mwenendo wa nyuklia kwingineko duniani kama vile shughuli za uhakiki wa nyuklia nchini Iran na ufuatiliaji wa mipango ya nyuklia wa DPRK.

Akihutubia ufunguzi wa mkutano mkuu wa IAEA mjini Vienna leo Bwana Grossi amesema kuwa misheni 53 zikiwa na zaidi ya wafanyakazi 100 wa shirika hilo zimetumwa kama sehemu ya kuendeleza kuwepo wao ndani ya vinu vitano vya nyuklia nchini Ukraine.

Vinu hivyo ni pamoja na kinu cha nyuklia cha Zaporizhzhya, au ZNPP, kwenye mto Dnipro kusini mwa Ukraine, ambako Bwana Grossi amesema kwamba hali inasalia kuwa tete sana.

ZNPP inadhibitiwa na vikosi vya Urusi lakini inaendeshwa na wafanyikazi wake wa Ukraine. 

Ni kinu kikubwa zaidi cha nyuklia barani Ulaya na IAEA imekuwa ikifuatilia hali huko tangu siku za mwanzo za mzozo.

Kila nchi inatamani nyuklia

Mkuu huyo wa IAEA amendelea kusema kwamba “Ni wazi kwamba kila nchi au jumuiya lazima iamue yenyewe ikiwa nishati ya nyuklia ni sawa kwao. Lakini pia inazidi kuwa bayana kuwa nchi zaidi na zaidi zinaonyesha nia ya kuwa na nishati ya nyuklia, na kwamba wanachukua hatua kwa nia hii. Hili lilidhihirika mwaka jana huko Washington katika mkutano wetu wa kimataifa wa mawaziri kuhusu nishati ya nyuklia katika karne ya 21. Nchi mpya zilitangaza mipango ya kuanzisha nishati ya nyuklia, wakati mataifa mashuhuri ya nyuklia yalifichua matamanio ya kuanzisha kizazi kipya cha vinu vya hali ya juu vya nyuklia kushughulikia changamoto kuu.”

Na hivyo akasema juhudi mpya za shirika hilo pia zilionyeshwa ili kuisaidia dunia kufikiria upya nishati ya nyuklia kama chanzo safi, cha kutegemewa na endelevu cha nishati kwa karne ya 21. 

Mathalani amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana nan chi wanachama katika kutumia nyuklia kukabiliana na magonjwa kama saratani na zoonotics.

Hadi miaka michache iliyopita, hatukuwa na sauti za kutosha kuhusu faida za nishati ya nyuklia. Lakini sasa ukurasa huo umegeuzwa ameongeza bwana Grossi.

Kwa mujibu wa IAEA hata kama kura za maoni ya umma kote ulimwenguni zinaonyesha mabadiliko katika kupendelea nishati ya nyuklia, nchi bado zinahitaji kushirikisha washikadau wote kwa uwazi na kwa vitendo katika mipango yao ya nishati ya nyuklia. Juhudi za pamoja na hatua zinahitajika katika kiwango cha kimataifa na kwa hivyo msimu ujao wa kuchipua kutakuwa na mkutano wa kilele wa nishati ya nyuklia. Maamuzi ya kijasiri yanahitajika ili kutufanya tuelekee katika mustakabali wa nishati wagharama nafuu, wa haki na endelevu unaogusa chaguzi zote zinazowezekana za teknolojia inayotoa hewa ukaa ndogo sana ikiwa ni pamoja na nishati ya nyuklia.

​ UN itaendelea kusaidia kwa kila hali usalama wa nyuklia Ukraine

Katika ujumbe uliosomwa wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema anapongeza "huduma ya ujasiri ya wafanyakazi wa IAEA waliopo kwenye vinu vya nyuklia nchini Ukraine. “

Ameahidi kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kufanya "kila unaloliweza kuhakikisha mzunguko salama wa wataalam wanaofanya kazi katika vituo vitano vya nyuklia vya Ukraine.”

Leo IAEA inasema duniani kote kuna vinu 410 vya nishati ya nyuklia vinavyofanya kazi katika nchi 31 vikiwa na uwezo wa kuzalisha takriban gigawati 369 za nishati, na kusambaza asilimia 10 ya umeme wa dunia na karibu robo ya umeme wote wa hewa ukaa ya chini. 

Pia kuna mitambo 58 inayojengwa katika nchi 31, na mitambo hiyo inatarajiwa kuzalisha takriban gigawati 60 za uwezo wa ziada wa nishati.