Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msaada wa IAEA waokoa wagonjwa wa saratani Uganda

Picha na: IAEA
Programu ya IAEA ya kudhibiti saratani kwa kutumia mionzi katika nchi za kipato cha chini na cha wastani

Msaada wa IAEA waokoa wagonjwa wa saratani Uganda

Afya

Shirika la nishati ya atomiki duniani, IAEA limesema saratani imesalia moja ya jukumu kubwa inalohusika nalo katika kazi yake. 

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Yukiya Amano, amesema hayo leo huko Vienna Austria wakati wa kikao cha bodi ya magavana wa shirika hilo akitolea mfano Zambia ambako amesema kumekuwepo na maendeleo makubwa ya matibabu dhidi ya saratani kutokana na usaidizi wa IAEA.

Amesema hospitali  ya saratani mjini Lusaka imekuwa mfano kwa nchi zingine kwenye ukanda huo.

Dkt. Amano ametaja pia Uganda akisema msaada wa IAEA umewezesha Uganda kupata mashine ya tiba ya miozi ambayo ilikosekana kwa miaka miwili baada ya mashine ya zamani kuharibika.

Nchini Malawi nako usaidizi wa kiufundi wa IAEA umewezesha nchi hiyo kupata mkopo wa dola milioni 13.5 na kufungua kituo cha kwanza kabisa cha kutibu saratani.

Na katika kilimo, IAEA imesaidia nchi za Afrika kutumia nyuklia kuzalisha mazao bora zaidi..

(Sauti ya Yukiya Amano)

“Aina mbalimbali za mpunga unaostahimili ukame zimetengenezwa huko Misri, ilhali Namibia imetengeneza mbegu za kunde na mtama ambazo pia zinastahimili ukame. Zimbabwe ilizindua mbegu bora zaidi ya kunde mwaka 2017.”

Amezungumzia pia masuala ya nyuklia ambapo kuhusu Iran, IAEA imekagua maeneo kwa mujibu wa itifaki mpya inayotaka ukaguzi ufanyike maeneo yote na kwamba hatua hiyo itajenga imani kuhusu mpango wa nyuklia wan chi hiyo.

Kuhusu jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Korea, DPRK, Dkt Amano amesema wanaendelea kuonyesha dhima yao muhimu ya kukagua mpango wa nyuklia wa nchi hiyo iwapo makubaliano ya kisiasa yatafikiwa baina ya nchi husika.