Ripoti: Zinahitajika $ Bil 360 kwa mwaka ili kufikia usawa wa kijinsia 2030

Takwimu mpya zilizokusanywa na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa zimeonesha kuwa kuna haja ya uwekezaji wa ziada wa dola bilioni 360 kwa mwaka ili kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake ifikapo 2030.
Tarehe 07 Seotember 2023 jijini New York Marekani shirika la Umoja wa Mataifa la UN WOMEN linalohusika na masuala ya wanawake na UNDESA ambayo ni Idara ya Umoja wa Mataifa ya uchumi na kijamii, walizindua ripoti yao ya kila mwaka ya Maendeleo kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu: Muhtasari wa jinsia 2023 inayotathimini namna malengo 17 ya maendeleo endelevu SDGs yanavyotekelezwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Utafiti wa mwaka huu ulihusisha nchi 116 pamoja na mambo mengine uliweka mkazo kwa wanawake wazee ambapo ripoti ilionesha kuwa kundi hilo ndani ya jamii linakabiliwa na viwango vikubwa si tu vya umasikini na kutokuwa na pensheni, bali pia ukatili, ikilinganishwa na wanaume wazee.
Wakati huu ambapo utelekezaji wa SDGs umefika nusu ya muda uliopangwa kabla ya kufikia kilele hapo mwaka 2030, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women Bi. Sarah Hendriks anasema ripoti ya mwaka huu ni wito mkubwa wa kuchukua hatua.
Bi. Hendriks aliongeza kuwa “ni lazima kwa pamoja na kwa dhamira ya dhati tuchukue hatua sasa kusahihisha changamoto zilizopo ili tuwe na ulimwengu ambao mwanamke na msichana wana haki sawa, fursa na uwakilishi. Ili kufikia hili, tunahitaji dhamira isiyoyumba, suluhu bunifu, na ushirikiano katika sekta zote na wadau.”
Ripoti hii imesisitiza hitaji la dharura la juhudi madhubuti za kuharakisha maendeleo kuelekea usawa wa Kijinsi ifikapo mwaka 2030 na kueleza kwamba zaidi ya dola bilioni 360 kwa mwaka zinahitajika ili kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika malengo muhimu ya kimataifa.
Pamoja kupigiwa chepuo kila kwenye majukwaa makubwa hususani ya wafanya maamuzi, pengo la kijinsia katika madaraka na nyadhifa za uongozi bado limekita mizizi, na, kwa kasi ya sasa ya maendeleo, ripoti imeeelza kizazi kijacho cha wanawake bado kitatumia wastani wa saa 2.3 zaidi kwa kila siku bila ujira wakati wakifanya kazi za nyumbani kuliko wanaume.
Ripoti ya mwaka huu pia iliangazia suala la mabadiliko ya tabianchi na takwimu zilizokusanywa zimeonesha kuwa mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusukuma hadi wanawake na wasichana milioni 158.3 katika umasikini. Idadi hiyo zaidi ya milioni 16 ikilinganishwa na wanaume na wavulana.
Ripoti hiyo pia inajumuisha wito wa kuwa na mtazamo jumuishi na wa kiujumla, ushirikiano mkubwa kati ya wadau, ufadhili endelevu, na hatua za kisera kushughulikia tofauti za kijinsia na kuwawezesha wanawake na wasichana duniani kote, ikihitimisha kwamba kushindwa kuweka kipaumbele kwa usawa wa kijinsia sasa kunaweza kuhatarisha Ajenda nzima ya 2030 ya SDGs.