Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maendeleo hayawezi kuwa endelevu kama sio jumuishi na yenye usawa:UN 

 Maendeleo endelevu SDGs
UN Photo/Manuel Elías
Maendeleo endelevu SDGs

Maendeleo hayawezi kuwa endelevu kama sio jumuishi na yenye usawa:UN 

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Umoja wa Mataifa umesema kuna ushahidi ulio bayana kwamba asilani maendeleo hayawezi kuwa endelevu kama sio jumuishi na hakuna usawa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa jukwaa la ngazi ya juu la kisisa ngazi ya mawaziri (HLPF) linalotathimini hatua zilizopigwa na nchi wanachama katika utekelezaji wa malengo sita ya maendeleo enedelu SDGs hii leo mjini New York Marekani, Katibnu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita jukwaa hili limekuwa kama taa ya kutoa dira ya utekelezaji wa malengo hayo na mwaka huu nchi 50 zimejitoa kimasomaso kufanyiwa tathimini ya utekelezaji wake katika malengo hayo. Guterres ametaja baadhi ya mambo yanayoonekana kuwa kikwazo cha nchi nyingi kutekeleza malengo hayo ambayo ni pamoja na“ongezeko la kutokuwepo usawa kunazuia ukuaji endelevu, sanjari na athari za utandawazi na mabadiliko ya teknolojia. Tunashuhudia leo hii jinsi gani pengo la usawa linavyochochea changamoto za kiuchumi, kuondoa imani ya umma na kuathiri mshikamano wa kijamii, haki za binadamu na mafanikio.”

Ameongeza kuwa ikiwa ni miaka minne sasa tangu kupitisha ajenda ya maendeleo ya 2030, bado juhudi haziridhishi na hatuko kwenye msitari unaotakiwa hivyo juhudi zaidi zinahitajika,amesema kwa mfano umasikini unapungua lakini sio kwa kiwango cha kutosha kutimiza lengo la kuutokomeza ifikapo 2030.

Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs
UN SDGs
Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs

Amesema pengo la usawa baina ya nchi na nchi ni kubwa na ingawa kiwango cha ukosefu wa ajira kimepungua lakini kiwango cha mishahara kimedumaa huku asilimia 30 ya wasichana na 13 ya wavulana hawana elimu, ajira au ujuzi wowote na watu bilioni 4 kote duniani hawana hifadhi ya jamii na kwamba, “hakuna nchi yoyote duniani iliyo katika mtari unaotakiwa kufikia usawa wa kijinsia ifikapo 2030, na wanawake wanaendelea kuathirika na sheria za kibaguzi, pengo la usawa wa fursa na ulinzi, viwango vikubwa vya ukatili na hulka na mila potofu.”

Na hatimaye amesema mabadiliko ya tabianchi yanakimbia kuliko kasi ya nchi wanachama kuyakimbiza na kutaja mambo manne yanayodhihirisha hilo, “mosi gesi ya viwandani hewani ni ya kiwango cha juu kabisa kushuhudiwa katika miaka milioni 3-5, pili dunia yetu itaweka rekoni ya miaka mitano ya joto la kupindukia duniani ambayo ni 2015-2019, tatu kina cha bahari sio tu kinaongezeka bali ni katika kasi ya hali ya juu na mwisho bila shaka sote twajua katika hili watu masikini, wasiojiweza na nchi ndio watakaoathirika zaidi. "

Hata hivyo amesema kuna mengi ya kufanya kugeuza hali hii, kwanza ni lazima kuongeza uwekezaji wa umma na sekta binafsi kwa ajili ya SDGs, pili kushirikiana na kuongeza msaada wa nchi zilizoendelea kwa masikini, tatu tunahitaji mfumo wa ufadhili wa afya ya kimataifa. Pia amesema kuwe na mazingira bora kwas ekta binafsi kuendelea na kuwekeza, kuhamia kwenye uchumi wa kijani kushughulikia suala n la uhamiaji, ahadi ya kimataifa katika kutokomeza vita na migogoro na kuhakikisha kila mtu anajumuishwa.