Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sasa ni wakati wa kulitoa azimio la SDGs kwenye karatasi na kulitekeleza kwa vitendo:UN

Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs
UN SDGs
Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs

Sasa ni wakati wa kulitoa azimio la SDGs kwenye karatasi na kulitekeleza kwa vitendo:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la ngazi ya juu la kisiasa kuhusu malengo ya maendeleo endelevu SDGs limefunga pazia jioni hii kwenye makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York kwa kupititishwa azimio la kisiasa la kusongesha mchakato wa kufikia malengo hayo.

Akizungumza wakati wa kufunga jukwaa hilo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Huu ni wakati wa kutoa maneno ya azimio lililopitishwa kutoka kwenye karatasi, na kuwekeza katika maendeleo kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa.”

Amerejelea kauli yake kwamba sasa ni wakati wa viongozi kurejea katika nchi zao na kuanza kufanyia kazi sera, bajeti na uwekezaji unaohitajika ili kufikia SDGs. Zaidi ya yote, sasa ni wakati wa kudhihirisha uongozi. Hebu tuchukue hatua sasa kwa ajili ya dunia iliyo bora, yenye afya, amani zaidi, endelevu na yenye mafanikio.”

Kauli ya Rais wa Baraza Kuu 

Rais wa Baraza Kuu Dennis Francis ameongeza sauti yake na kusisitiza kuwa  “Tunahitaji kuchukua hatua, tunahitaji kuwa na matamanio, tunahitaji ushirikiano, na tunahitaji kwenda na wakati.”

Pia amesema "Tunahitaji kuhakikisha kuwa mfumo wa kifedha wa kimataifa unahudumia nchi zote, kushughulikia mahitaji ya zama hizo na kubadilika vya kutosha ili kukabili changamoto za kesho. Lazima tuhakikishe kwamba taasisi zetu za umma zinaunga mkono sera madhubuti na kuharakisha maendeleo kuelekea SDGs.”

Mwenyekiti mwenza waziri mkuu wa Canada Justin Trudeau

Waziri Mkuu wa Kanada Justin Trudeau, ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa jopo la Watetezi wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ameongeza sauti yake katika hafla ya kufunga jukwaa hilo.

Amesema, “Tunatakiwa kuhakikisha kuwa sekta binafsi zinapiga hatua kikamilifu kuwekeza kote duniani. Tunahitaji kuhamasisha rasilimali hizo, tunahitaji kufanya kazi bega kwa bega na nchi zinazoibukia kiuchumi ili kuhakikisha kuna uwezekano wa kutabirika badala ya kuwa na utulivu na uthabiti kwa uwekezaji wao.”

Waziri Mkuu wa Kanada amehitimisha ujumbe wake kwa kusema "Wakati umefika, kwa sisi sote kujitokeza na kuelewa mustakbali wetu unatarajia sisi sote kukutana wakati huu. Tunahitaji kuongeza juhudi zetu maradufu, tunahitaji kuendelea kufanya kazi pamoja na tunahitaji kujenga ulimwengu bora ambao SDGs ndio njia yetu.”

Mambo saba yanayohitajika kufanywa

Vipengee saba viko kwenye "orodha ya mambo ya kufanya ya maendeleo," kutoka kwenye Mkutano wa SDG.

Mosi: kubadili msaada wa kuchochea utekelezaji wa SDG kuwa uwekezaji halisi katika nchi zinazoendelea.

Pili: kutafsiri ahadi zilizotolewa katika mkutano huu katika sera madhubuti, bajeti, uwekezaji na hatua.

Tatu: kuimarisha msaada wa utekelezaji katika mabadiliko sita muhimu ya SDGs yaliyoangaziwa hapa ambayo ni chakula, nishati, uwekezaji wa kidijitali, elimu, ulinzi wa hifadhi ya kijamii na ajira na bayoanuwai.

Nnne: Anza mipango sasa kwa ajili ya ongezeko kubwa la uwekezaji katika hifadhi ya jamii.

Tano: Kama tamko la kisiasa linavyoweka bayana ni wakati muafaka kwa nchi zilizoendelea kufikia lengo lao lamsaada rasmi wa maendeleo ya asilimia 0.7 ya pato la taifa.

Sita - Mkutano wa mwezi ujao wa shirika la fecha duniani IMF na Benki ya Dunia haupaswi kuwa kama wa kawaida.

Na saba: Fika kwenye mkutano wa COP28 mwezi ujao na mipango na mapendekezo madhubuti ya kuzuia athari mbaya zaidi za mabadiliko ya tabianchi, kuweka ahadi za kimataifa za kutoa msaada muhimu, na kusaidia nchi zinazoendelea kufikia mabadiliko ya haki na ya usawa kwa nishati mbadala.