Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatuwezi kufanyakazi chini ya mtutu wa bunduki Sudan: Mkuu wa OCHA

Watu wanasubiri kupatiwa hifadhi katika kambi ya muda ya wakimbizi iliyoko kilomita 5 kutoka mpaka wa Chad na Sudan. Wengi wa watu hawa tayari walikuwa wakimbizi wa ndani katika eneo la Darfur.
© WFP/Eloge Mbaihondoum
Watu wanasubiri kupatiwa hifadhi katika kambi ya muda ya wakimbizi iliyoko kilomita 5 kutoka mpaka wa Chad na Sudan. Wengi wa watu hawa tayari walikuwa wakimbizi wa ndani katika eneo la Darfur.

Hatuwezi kufanyakazi chini ya mtutu wa bunduki Sudan: Mkuu wa OCHA

Amani na Usalama

Kwa muda wa miezi mitatu sasa, watu wa Sudan wamevumilia mateso yasiyoelezeka huku kukiwa na ghasia zinazosambaratisha nchi yao amesema mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu na mkuu wa ofisi ya kuratibu masuala ya dharura na misaada ya kibinadamu OCHA, Martin Griffiths. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leoi mjini New York Marekani bwana Griffiths amesema “Wakati mzozo huo unapoingia mwezi wake wa nne, safu za vita zinazidi kuwa ngumu, na kufanya kuwa vigumu zaidi kufikia mamilioni ya watu wanaohitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.”

Ameongeza kuwa Sudan sasa ni mojawapo ya maeneo magumu zaidi duniani kwa wafanyakazi wa kibinadamu kufanya kazi. 

“Tukishikana mkono na mashirika ya ndani, tunafanya yote tuwezayo kuwasilisha vifaa vya kuokoa maisha. Lakini hatuwezi kufanya kazi wakati bunduki zikirindima .Hatuwezi kujaza maduka ya chakula, maji na dawa ikiwa uporaji wa kulenga msaada huo utaendelea. Hatuwezi kutoa msaada ikiwa wafanyikazi wetu wamezuiwa kuwafikia watu wenye uhitaji.”

Familia ya Kisudan ikipata hifadhi kwenye kituo cha kupokea wakimbizi karibu na mpaka kati ya Sudan na Chad
© WFP/Eloge Mbaihondoum
Familia ya Kisudan ikipata hifadhi kwenye kituo cha kupokea wakimbizi karibu na mpaka kati ya Sudan na Chad

Madhila yataisha vita itakapokwisha

Mkuu huyo wa misaada ya kibinadamu amesema “Hatimaye, mateso ya Sudan yataisha tu wakati mapigano yatakapoisha. Wakati huo huo, tunahitaji ahadi zinazotabirika kutoka kwa wahusika kwenye mzozo ambazo zitaturuhusu kuwasilisha kwa usalama msaada wa kibinadamu kwa watu wanaohitaji, popote walipo. “

Amezitaka pande zote mbili katika mzozo lazima zifuate tamko la ahadi walilotia saini huko Jeddah la kulinda raia na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu.

Tangu mzozo huo huo uanze, zaidi ya watu milioni 3 nchini Sudan nusu yao wakiwa ni watoto wamefungasha virago na wamekimbia ghasia, ndani na nje ya nchi. 

Nusu ya watoto waliosalia nchini Sudan, ambao ni takriban milioni 13.6, wanahitaji msaada wa kibinadamu haraka.

Wakimbizi wapya waliowasili kutoka Sudan waanzisha makazi ya muda nchini Chad.
© UNHCR/Colin Delfosse
Wakimbizi wapya waliowasili kutoka Sudan waanzisha makazi ya muda nchini Chad.

Kila siku ya vita zahma inaongezeka

Kwa mujibu wa Griffiths kila siku mapigano yanapoendelea, masaibu yanazidi kuwakumba raia wa Sudan. 

“Ugunduzi wa hivi majuzi wa kaburi la halaiki nje ya mji mkuu wa Darfur Magharibi, El Geneina, ni ushahidi wa karibuni kabisa unaoashiria kuzuka upya kwa mauaji ya kikabila katika eneo hilo. Jumuiya ya kimataifa haiwezi kupuuza mwangwi huu mbayá wa historia huko Darfur.”

Amesisitiza kuwa “Ni lazima sote tuongeze juhudi zetu ili kuhakikisha kwamba mzozo wa Sudan hauingii katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya kikatili na visivyoweza kuisha vyenye madhara makubwa kwa eneo hilo. Watu wa Sudan hawawezi kusubiri.”