Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 2.5 wametawanywa Sudan tangu Aprili 15: UNHCR

Mama na binti zake wanne wanawasili Chad kutoka Sudan.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Mama na binti zake wanne wanawasili Chad kutoka Sudan.

Zaidi ya watu milioni 2.5 wametawanywa Sudan tangu Aprili 15: UNHCR

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema inatiwa hofu kubwa na ongezeko la mahitaji ya kibinadamu miongoni mwa watu walioathirika na machafuko yanayoendelea nchini Sudan wakati idadi ya wati waliotawanywa na mgogoro huo ikiendelea kuongezeka na huku ufikishaji wa misaada ya kibinadamu ukiendelea kukabiliwa na vikwazoi vya kiusalama, kutokuwa na fursa ya kuwafikia wenye uhitaji na ukosefu wa fedha za ufadhili.

Kamishna mkuu msaidizi wa uendeshaji wa UNHCR, Raouf Mazou akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo amesema “Zaidi ya watu milioni mbili na nusu wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo huo tangu Aprili 15, huku zaidi ya watu 560,000 wakitafuta usalama katika nchi jirani ambapo Misri ndio iliyopokea idadi kubwa zaidi ya wakimbizi, ikifuatiwa na Chad, Sudan Kusini, Ethiopia na Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na karibu watu milioni mbili wamekuwa wakimbizi wa ndani ya nchi yao.”

Mahema yamejengwa katika kambi ya wakimbizi ya Gorom nchini Sudan Kusini ili kuwahifadhi wakimbizi wapya kutoka Sudan.
© UNHCR/Charlotte Hallqvist
Mahema yamejengwa katika kambi ya wakimbizi ya Gorom nchini Sudan Kusini ili kuwahifadhi wakimbizi wapya kutoka Sudan.

Maelfu wako njiapanda bila msaada

Bwana Mazou ameongeza kuwa nchini Sudan, mapigano yanayoendelea katika mji mkuu, Khartoum, na katika majimbo ya Darfur na Kordofan, yamewaacha wengi wakiwa wamekwama na bila misaada ya msingi ya kibinadamu.

UNHCR imepokea ripoti za kutisha za raia waliokimbia makazi yao wakiwemo wakimbizi wanaokabiliwa na vikwazo vya kutishia maisha wakati wakijaribu kutafuta usalama ndani ya nchi na kuvuka mipaka. 

Shirika hilo la wakimbizi linasema “Kutokana na kukithiri kwa mzozo huo, watu walio katika mazingira magumu wanaokimbia hawana chaguo isipokuwa kukimbia katika mazingira hatarishi na magumu, na kujiweka katika hatari ya unyanyasaji wa kingono, wizi na ujambazi, na katika baadhi ya matukio, kunyimwa fursa ya kuondoka katika maeneo yenye migogoro na kulazimishwa kurudi kwenye njia za hatari”.

Raouf Mazou  amesisitiza kuwa “Timu zetu zinaongeza juhudi za kusaidia wale wanaofika katika maeneo salama kupitia usajili, kutoa msaada wa dharura na kupanua wigo wa huduma katika maeneo yaliyopo. Hata hivyo, kutokuwa na fursa ya kuyafikia maeneo yaliyoathirika kunazuia utoaji wa rasilimali za msingi na huduma muhimu kwa raia walio katika mazingira magumu”.