Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC maisha yamesambaratishwa na ghasia, kufurushwa na njaa katika mgogoro uliosahaulika: WFP

Mwanamke akifanyakazi katika ghala la chakula la WFP mjini Katanga DR Congo
© WFP/Vincent Tremeau
Mwanamke akifanyakazi katika ghala la chakula la WFP mjini Katanga DR Congo

DRC maisha yamesambaratishwa na ghasia, kufurushwa na njaa katika mgogoro uliosahaulika: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Jumuiya ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa leo imetoa ombi la dharura kusaidia mamilioni ya watu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ambako ghasia za muda mrefu na watu kuyakimbia makazi yao kunaendelea kuchochea baa la njaa.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, tangu Machi 2022 pekee, watu milioni 5.7 wamekimbia makazi yao katika majimbo ya Mashariki ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.

Idadi kubwa ya waliotawanywa

Kwa mujibu wa WFP ujumla ya watu milioni 6.2 wamekimbia makazi yao kote nchini  ikiwa ni idadi kubwa zaidi barani Afrika.

Msemaji wa WFP kusini mwa Afrika, Tomson Phiri, amewaambia waandishi wa habari huko Geneva Uswisi kwamba "Nchi ina ukubwa wa bara na ekari nyingi za nafasi, lakini mamilioni ya watu hawana chaguo ila kuishi katika kambi zenye msongamano mkubwa na duni au na familia ambazo tayari zimeelemewa.”

Fursa ya ufikishaji misaada ya kibinadamuni finyu

WFP inasema leo hii kutokana na matokeo ya uvunjaji sheria unaohusishwa na vikundi 120 vyenye silaha visivyo vya serikali, shirika hilo limejitahidi kutoa misaada muhimu kwa jamii zilizo hatarini ambapo majadiliano ya fursa za kuwafikia wenye uhitaji ni changamoto inayoendelea.

"Huwa inaichukua WFP siku nne hali inaporuhusu kupeleka msaada wa chakula kutoka Goma, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Mashariki, hadi eneo linaloitwa Beni, ambalo liko umbali wa kilomita 241," amesema Bwana Phiri na kuongeza kuwa "Lakini leo hii inatuchukua kati ya miezi mitatu hadi minne kufanya hivyo kwa sababu ya ukosefu wa usalama."

Ugawaji wa dharura wa chakula unaendelea Mashariki mwa DRC
© WFP/Michael Castofas
Ugawaji wa dharura wa chakula unaendelea Mashariki mwa DRC

Zaidi ya watu milioni 25 wana njaa

Bwana Phiri, ambaye ameshikilia kuwa janga la kibinadamu nchini humo ni mfano wa dharura iliyosahaulika, ameelezea kuwa watu kufurushwa makwaokumechangia uhaba wa chakula huku watu wakifukuzwa katika ardhi yao na kuachwa hawawezi kulima chakula chochote.

“Makadirio ya hivi karibuni yanaonyesha kuwa watu milioni 25.8 nchini DRC watakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula mwaka huu wa 2023 ikiwa ni idadi kubwa zaidi ulimwenguni.”

Msemaji huyo wa WFP ameongeza kuwa “Wengi wa watu wa taifa hili wana njaa licha ya utajiri mkubwa wa asili wa nchi hiyo. Cha kushangaza zaidi DRC inazalisha madini ya thamani ambayo hutoa teknolojia ya juu zaidi duniani.”

Changamoto ya mabadiliko ya tabianchi

Mbali na kuongezeka kwa vurugu mashariki, mgogoro wa  mabadiliko ya tabianchi leo hii unaendelea kukatili maisha na kuathiri riziki. 

Takriban watu 400 walikufa katika mafuriko mabaya huko Kivu Kusini mwezi uliopita,  nyumba 3,000 ziliharibiwa na kusababisha watu wengine kukosa makazi.

Sasa zaidi ya hapo awali, jumuiya zinazowakaribisha wakimbizi pia zinakabiliwa na hatari ya njaa, ameonya Bwana Phiri wakati WFP inaongeza msaada ili kuwafikia watu milioni 3.6 katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Tunahitaji amani

Bwana Phiri amebainisha kwamba hadi sasa mwaka huu, ni asilimia 15 tu ya dola milioni 870 zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na misaada ya kibinadamu nchini humo ndizo zimepatikana, 

Hivyo amesisitiza kuwa "Tunahitaji uwekezaji katika nyanja zote za maisha nchini DRC kuanzia miundombinu, hadi huduma za msingi, lakini muhimu zaidi, tunahitaji amani."