Janga baya zaidi la njaa laikabili Zimbabwe-WFP

7 Agosti 2019

Zimbabwe inakabiliwa na janga baya zaidi la la njaa kuwahi kuikumba nchi hiyo na hali ya uhakika wa chakula imefikia kiwango kinachohitaji msaada wa haraka ili kunusuru Maisha ya mamailioni ya watu  limesema leo shirika la mpango wa chakula duniani WFP. 

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo msemaji wa shirika hilo Herve Verhoosel amesema tayari jumuiya ya kimataifa ya masuala ya kibinadamu imeanza kuchukua hatua na kutoa ombi la haraka la fedha ili kukabiliana na hali hiyo huku WFP ikiongeza msaada wake hususan katika maeneo yaliyoathirika vibaya na ukame, lakini pia kuzijengea uwezo jamii kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

WFP inasema zaidi ya watu milioni 3.6 katika maeneo ya vijijini Zimbabwe hawatokuwa na uhakika wa chakula ifikapo Oktoba mwaka huu na ifikapo Januari mwakani idadi inatarajiwa kuongezeka hadi watu milioni 5.5.

Wilaya 60 zinatarajiwa kumaliza akiba yake yote ya mahindi ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu na hii ni sawa na asilimia 60 ya watu wote wa vijijini.

Kwa sasa WFP inatoa msaada wa chakula kwa watu 700,000 mwezi huu wa agosti na endapo fedha zitaruhusi inatarajia kuongeza idadi ya watu wanaosaidiwa na kufikia milioni mbili mwezi Januari mwakani.

Ili kufanikisha utoaji msaada huo WFP inahitaji dola milioni 173 kutosheleza huduma kwa miezi tisa ijayo. Na jumuiya ya misaada ya kimataifa inahitaji dola milioni 331 ili kusaidia Zimbabewe.

WFP imeomba jumuiya ya kimataifa na wahisani kuchukua hatua haraka ili fedha hizo zipatikane kuweza kunusuru Maisha ya mamilioni ya wat una kuepusha janga kubwa.

 

Shiriki kwenye Dodoso UN News 2021:  Bofya hapa Utatumia dakika 4 tu kukamilisha dodoso hili.

♦ Na iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter