Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahamiaji ni msingi wa maendeleo toka enzi na enzi, tusiwabague bali tuwasaidie: IOM

Wakuu wa UNHCR, Filippo Grandi (wa pili kulia), na IOM, António Vitorino (wa pili kushoto), wakitembelea kituo cha misaada ya kibinadamu cha UNHCR huko Agadez, katikati mwa Niger.
© UNHCR/Colin Delfosse
Wakuu wa UNHCR, Filippo Grandi (wa pili kulia), na IOM, António Vitorino (wa pili kushoto), wakitembelea kituo cha misaada ya kibinadamu cha UNHCR huko Agadez, katikati mwa Niger.

Wahamiaji ni msingi wa maendeleo toka enzi na enzi, tusiwabague bali tuwasaidie: IOM

Wahamiaji na Wakimbizi

Katika kuelekea siku ya kimataifa ya wahamiaji duniani itakayoadhimishwa tarehe 18 desemba mwaka huu, shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM limemtaka kila mtu atafakari, mhamiaji ni nani? mchango wa wahamiaji na endapo hapa duniani kuna mtu yeyote ambaye hajawahi kufikiria kuondoka aliko na kwenda kusaka mustakhbali bora, kwani  hatua hii itasaidia kutambua sababu ya uhamiaji na mchango wake kwenye jamii ambako wanakwenda.

Kuelekea siku hiyo, IOM imechapisha video mbalimbali za wahamiaji katika chaneli yake ya Yotube ambako katika moja ya video hizo mhamiaj immoja anasema, Mimi ni mhamiaji,  akijinadi kwa ujasiri huku mwingine akieleza kuwa mhamiaji ni mtu kama mtu mwingine yeyote ambaye amejikuta haishi kwenye nchi aliyozaliwa. 

Kwa mujibu wa IOM kuna sababu lukuki zinazowalazimisha watu kufungasha virago na kwenda katika nchi nyingine, sababu kama vile vita, usalama, mabadiliko ya tabianchi, njaa, na hata kusaka mustakbali bora na wengi wanacho cha kuchangia katika jamii wanakokwenda. Hata hivyo mara nyingi kama anavyosema Antonio Vitorino Mkurugenzi Mkuu wa IOM katika ujumbe wake wa siku ya kimataifa ya wahamiaji mchango wao hauonekani wala kuthaminiwa. 

“Ni watu ambao wamekuwa msingi wa maendeleo na hatua zilizopigwa, ambao wametajirisha jamii nacnchi tangu enzi za kale. Lakini ndio watu ambao mara nyingi wanateseka, wanakwama , kunyanyaswa, kudhalilishwa na kubaguliwa.” 

Vitorino ameongeza kuwa uhamiaji haukuanza jana wala leo, umekuwa ni moja ya hulka za kale sana hivyo amesihi kutoruhusu kuingiza siasa , chuki dhidi ya wageni na mambo mengine kama hayo kwenye suala la uhamiaji 

“Watu uhama kwa sababu nyingi na kwa njia mbalimbali, lakini bila kujali kilichowafanya watu kuhama, haki zao, utu wao lazima viheshimiwe na mchango wao utambuliwe.” 

Amehitimisha ujumbe wake kwa kusisitiza kwamba “jambo la msingi kabisa wahamiaji kwanza ni binadamu, watu, ndugu, majirani na viongozi na hivyo dunia inapaswa kuwasaidia na sio kuwabagua.” 

Maudhui ya mwaka huu ya siku ya wahamiaji yanaihimiza dunia kutafakari na kutambua mchango muhimu wa wahamiaji.