Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO: Bahari ni sehemu ya suluhisho la matatizo lukuki katika jamii

Mvuvi katika ziwa Tanganyika, Tanzania
UN News
Mvuvi katika ziwa Tanganyika, Tanzania

FAO: Bahari ni sehemu ya suluhisho la matatizo lukuki katika jamii

Tabianchi na mazingira

Wakati dunia ikijiandaa kuadhimisha siku ya bahari duniani hapo kesho Juni nane shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limesema ni vyema jamii kuzingatia afya ya baharí kwani umuhimu wake kamwe hauwezi kupuuzwa. 

Bahari, ni makazi ya asilimia 80 ya majani ya wanyama, ambayo yanatumika kama chanzo muhimu cha wananchi kujipatia riziki na pia lishe kwa mamilioni ya watu ulimwenguni.

Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Rasilimali za Uvuvi na Ufugaji wa samaki kutoka FAO Manuel Barange, anasema kwa utajiri uliopo baharini, “Hakuna tatizo hata moja ambalo tunalo ulimwenguni iwe kwenye mabadiliko ya tabianchi, umasikini au uhakika wa chakula ambalo linaweza kutatuliwa bila kuzingatia baharí kama sehemu ya suluhisho”

Manuel anasema kwa sasa zaidi ya watu milioni 800 wameathiriwa na njaa kote ulimwenguni, vyakula vya baharini vilivyo sheheni lishe ya hali ya juu ni suluhisho la kushughulikia njaa na utapiamlo, “Ufugaji wa samaki umekuwa mfumo wa uzalishaji wa chakula unaokua kwa kasi zaidi katika kipindi cha  miongo mitano iliyopita. Ulaji pia wa vyakula vya majini umekuwa ukiongezeka maradufu ya kiwango cha ongezeko la watu katika miongo ya hivi karibuni.”

Katika kuhakikisha kila nchi inajitosheleza na kuweza kuhimili ongezeko la uhitaji wa vyakula vya majini FAO inahamasisha utekelezaji wa mkakati wa Mabadiliko ya Buluu Blue Transformation unaolenga kuimarisha mifumo ya vyakula vya majini katika kulisha idadi ya watu inayoongezeka duniani kwa kutoa mifumo ya kisheria, sera na usaidizi wa kiufundi inayohitajika ili kuendeleza ukuaji na uvumbuzi, “Mpango wa Mabadiliko ya Bluu ni dira kutoka FAO ambayo imeanza na kanuni mbili kubwa. Kwanza ni kukubali kwamba vyakula vya majini ni sehemu ya suluhisho la njaa na utapiamlo. Pili ni utambuzi kwamba mabadiliko yanafanyika hata bila sisi kufanya lolote.”

Mpango wa Mabadiliko ya Buluu umependekeza msururu wa hatua zilizoundwa kusaidia ustahimilivu katika mifumo ya chakula cha majini na kuhakikisha uvuvi na ufugaji wa samaki unakuwa kwa njia endelevu huku hakuna mtu anayeachwa nyuma, hususan jamii zinazotegemea sekta hiyo.

Masuala mengine yanayoangaziwa na mabadiliko hayo ni pamoja na sera na desturi zinazofaa kwa mabadiliko ya tabianchi na mazingira, pamoja na ubunifu wa kiteknolojia.