Ukame wasababisha wanakijiji kula dungusi kakati nchini Madagascar

Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha kuenea kwa jangwa katika sehemu za kusini mwa Madagascar
UN Madagascar
Mabadiliko ya tabianchi yamesababisha kuenea kwa jangwa katika sehemu za kusini mwa Madagascar

Ukame wasababisha wanakijiji kula dungusi kakati nchini Madagascar

Tabianchi na mazingira

Wakati mkutano wa mabadiliko ya tabianchi ungali ukiendelea huko Glasgow, Scotland, ukame unazidi kushika kasi kusini mwa Madagascar na watu wakiingia mwaka wa tano bila ya mvua hali inayowalazimu wananchi kula dungusi kakati kwa kuwa ndio mmea pekee unaoota kwenye maeneo yao.  

Mito! Ardhi Kame! Vumbi na watu wakisaka maji kwenye eneo kavu! ni taswira kutoka angani kupitia video ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP ya kijiji cha Marofanony kilichoko kusini mwa Madagascar!

Ardhini timu ya WFP inalakiwa na upepo mkali ukipeperusha mchanga na mmea ulioshamiri zaidi ni Dungusi kakati. Hivi ndivyo tunavyokula, anasema Masy Celestinea ambaye amekutwa akikusanya majani ya mmea wa dungusi kakati, ambayo bado hata hayajatoa matunda.

Licha ya mjukuu wake aliyekuwa na miezi 8 kufariki kutokana na kula mbegu nyingi za tunda hili Masy anasema bado hawezi kuacha kula.“Watu wote wa hapa kijijini tunakula haya majani. Kwa sababu ni miaka mitano imepita tangu mvua inyeshe. Wale waliokuwa na mifugo sasa hawana tena, kwa sababu wameuza ng'ombe zote. Angalia mazao yetu, hakuna majani yanayokua, hata moja. Unapopita kwenye barabara, unaweza kuona, ni kavu. Kuna upepo wa mchanga tu.”

Huu ndio mmea wa dungusi kakati
FAO/Filippo Brasesco
Huu ndio mmea wa dungusi kakati

Ziara ya WFP katika kijiji hiki imekuja na faraja ambapo watoto wanapimwa kiwango cha utapiamlo huku wazazi nao wakipata msaada wa mahindi, mafuta, chumvi na vyakula vyenye virutubisho kwa ajili ya akina mama na watoto walioathirika na ukame.

Naibu Mkurugenzi Mkazi wa WFP nchini Magadascar Arduino Mangoni anasema aliyoyaona yanahuzunisha
"Kwa sababu ya ukame, kwa sababu ya dhoruba za mchanga, hili ni jambo jipya ambalo limejidhihirisha katika miaka michache iliyopita, bei ya vyakula imepanda kwa sababu ya uzalishaji duni wa kilimo na watu hawana chakula cha kutosha ... hawana. Sina pesa za kuwapatia chakula na viwango vya utapiamlo vinaongezeka. Watu hawa hawajachangia mabadiliko ya tabianchi lakini wao ndio wanalipa gharama ya  juu zaidi.”

Masy anahitimisha kwa kuwaeleza viongozi walioko kwenye mkutano wa COP26 huko Glasgow kuwa “Unajua msitu una uhai wake, binadamu ana uhai wake, msitu una damu yake, na sisi wanadamu pia. Nina huzuni kwa sababu mvua hainyeshi tena, na Madagascar ni mwathirika wake. Nina huzuni kwa sababu mvua hainyeshi. Hakuna hata umande, lakini upepo mkali tu unavuma, kwa hivyo nina moyo wa huzuni. inanivunja moyo.”