Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shughuli za uvuvi na ufugaji wa Samaki zinatoa mchango mkubwa kwenye uhakika wa upatikanaji wa chakula :FAO

 Bandari ya uvuvi ya Joal nchini Senegal.
© FAO/Sylvain Cherkaoui
Bandari ya uvuvi ya Joal nchini Senegal.

Shughuli za uvuvi na ufugaji wa Samaki zinatoa mchango mkubwa kwenye uhakika wa upatikanaji wa chakula :FAO

Ukuaji wa Kiuchumi

Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu bahari ukiwa katika siku ya tatu hii leo huko Lisbon nchini Ureno Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO limesema ongezeko kubwa la ufugaji wa samaki sambamba na uvuvi wa kimataifa umesababisha mazao ya vyakula vya majini kuwa kwenye rekodi ya juu katika kuchangia kwa kiasi uhakika wa chakula na lishe katika karne hii ya Ishirini na moja.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ya FAO iliyotolewa leo kwenye miji ya Lisbon Ureno na Roma Italia ikinukuu Ripoti ya mwaka huu wa 2022 kuhusu Hali ya uvuvi na mazao ya majini au SOFIA. 

Akizungumzia ripoti hiyo Mkurugenzi Mkuu wa FAO Qu Dongyu amesema jumla ya uvuvi na ufugaji wa samaki ulifikia kiwango cha juu cha tani milioni 214 mwaka 2020 ikijumuisha tani milioni 178 za wanyama wa majini na tani 36 za mwani. 

Uvuvi na ufugaji wa samaki huchangia katika ajira, biashara na maendeleo ya kiuchumi. Jumla ya mauzo ya kwanza ya thamani ya uvuvi na ufugaji wa samaki na wanyama wa majini kwa mwaka 2020 ilikadiriwa kuwa dola bilioni 406, ambapo dola bilioni 265 zilitokana na uzalishaji wa ufugaji wa samaki. 

 

Wavuvi wenyeji huvua dagaa kwenye ufuo wa Kitaifa wa Nui Chua huko Vietnam.
UNEP/Lisa Murray
Wavuvi wenyeji huvua dagaa kwenye ufuo wa Kitaifa wa Nui Chua huko Vietnam.

Uvuvi endelevu

FAO imesema ukuaji wa uvuvi na ufugaji wa samaki ni muhimu duniani kote katika jitihada za pamoja za kumaliza njaa na utapiamlo lakini kunatakiwa kufanyika mabadiliko ili kukabiliana na changamoto zilizopo. 

 Dongyu amesema wakati sekta hiyo ikizidi kukuwa “kunahitajika mabadiliko ili kuwa na sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki endelevu zaidi, yenye ushirikishaji na usawa kwakuwa biashara ya kutumia vyakula vya majini ni muhimu ikiwa tunataka kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa”. 

“Lazima tubadili mifumo ya chakula kitokanacho na kilimo ili kuhakikisha vyakula vya majini vinavunwa kwa uendelevu, maisha yanalindwa na makazi ya majini na viumbe hai vinalindwa” ameongeza Dongyu

 Na ili kupata suluhisho la changamoto za uzalishaji huo Mkurugenzi Mkuu wa FAO anayehusika na Idara ya Uvuvi na Ufugaji wa samaki Manuel Barange amesema kunahitajika  mabadiliko ya bulu “Ni mchakato unaoendeshwa na malengo ambapo wanachama na washirika wa FAO wanaweza kuongeza mchango wa mifumo ya chakula cha majini ili kuimarisha uhakika wa chakula , lishe bora na lishe kwa gharama nafuu huku ikibaki ndani ya mipaka ya ikolojia” 

 Kusoma zaidi kuhusu ripoti hii bofya hapa