Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwasaidie wananchi waliathirika na ukame wana hali mbaya: FAO

Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.
UNDP/Ngele Ali
Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.

Tuwasaidie wananchi waliathirika na ukame wana hali mbaya: FAO

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO katika Ukanda wa Afrika Mashariki limetoa wito kwa wananchi, taasisi binafsi na mashirika ya dini kuchangia wananchi walioathirika na Ukame pamoja na mazao yao kuharibiwa na nzige katika nchini za Kenya, Ethiopia na Somalia. 

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa Dokta. Paul Mutungi Afisa wa mashinani wa Shirika hilo la FAO anayehusika na wafugaji katika Ukanda wa Afrika Mashariki amesema “Hali ya Afrika Mashariki na Pembe wa Afrika sio nzuri sana kwasababu katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwa na baa la njaa alafu likafuatiwa na janga la nzige na kisha janga la COVID-19 ambalo hata kabla ya kuisha kumekuja na ukame mkali ambao umesababishwa na hali ya Ya- Nina  na umeweka watu wengi sana hatarini kwasababu kumekuwa na ukosefu wa chakula na kumekuwa na njaa na sasa maisha yao yapo hatarini”. 

Akitolea mfano ya maeneo yaliyoathirika na hali hiyo Dkt. Mutungi amesema “Kenya katika eneo la Mosobeti lililopo kusini mwa Kenya pale ni wafugaji na wanyama wengi sana wamekufa kwasababu ya ukosefu wa lishe ya nyasi na hata maji watoto nao wamekuwa na utapiamlo. Maeneo mengine ni Turkana mpaka kule Mandera kumeathirika kabisa."

Soundcloud

 

Akigusia nchini Ethiopia amesema “Ukiangalia jimbo la Somali, Afar na Oromia wamethirika pia kwasababu majimbo yote haya yanatumainia kilimo cha wanyama. Na nchini Somalia karibu 90% imepatwa na baa la njaa.” 

Wanawake na watoto wakipulizwa na vumbi la mchanga katika eneo la Somalia, Ethiopia.
© UNICEF/Mulugeta Ayene
Wanawake na watoto wakipulizwa na vumbi la mchanga katika eneo la Somalia, Ethiopia.

FAO walichofanya 

Dkt. Mutungi anasema wakati FAO ilipoona hali inazidi kuwa ya hatari na maisha yanakuwa magumu kwa wananchi walichukua fedha za miradi mingine ili kuweza kusaidia wananchi wasife njaa na mifugo yao isizidi kuangamia. “Tulipeleka chakula cha ng’ombe, dawa za kutibu mifugo na maeneo machache ambapo wanalima tuliwapatia mbegu kidogo.” 

Msaada zaidi unahitajika 

Kwa mujibu wa FAO katika nchi tatu za Kenya, Ethiopia na Somalia jumla ya watu milioni 25.3 wanauhitaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu. “Watu hawa wapo hatarini, mambo yao yasipoangaliwa kufikia katikati ya mwaka huu ( 2022) maisha yao yatakuwa katika hatari kubwa sana na ndio maana tumeomba msaada wa fedha dola milioni 138 ili iweze kusaidia katika mambo haya yanayowakabiliwa wananchi. “Amesisitiza Dkt Mutungi. 

Amesema wamekuwa wakipokea misaada kutoka kwa nchi zenyewe kama Kenya, na taasisi za kidini pamoja na wananchi binafsi lakini bado mahiyaji ni makubwa na hivyo kila mtu mwenye uwezo wa kuchangia kwa namna yoyote kuokoa maisha ya wananchi hawa anahimizwa kufanya hivyo na wengine wenye uwezo wakuchangia moja kwa moja katika shirika hilo la Umoja wa Mataifa wanaombwa kuwasilisha michango yao.

Nzige wa Jangwani ambao kwa muda wamevamia maeneo ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, sasa wamevamia nchi za kusini mwa Afrika.
© FAO/Haji Dirir
Nzige wa Jangwani ambao kwa muda wamevamia maeneo ya Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika, sasa wamevamia nchi za kusini mwa Afrika.

 Wito wa FAO kwa wananchi wa Afrika

1.    Hali ya anga imeanza kuwa mbaya hivyo watu watunze mazingira ili ukame unapokuja waweze kuwa hata na maji.

2.    Wafugaji wakiona ukame umeanza wauze mifugo yao wasingonje mpaka afya ya mifugo imeathirika ndio wauze, hawatapata fedha nzuri. 

3.    Wakulima warudi kwenye kutumia mbegu za asili ambazo zinastahimili ukame.