Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Urithi wa DRC ni wa watu wa DRC, tuhakikishe ni chanzo cha maendeleo na sio migogoro:Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 11 wa mfumo wa ufuatiliaji wa kikanda kwa ajili ya amani, usalama na ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ulioanza leo mjini Bujumbura Burundi
UN / BURUNDI
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 11 wa mfumo wa ufuatiliaji wa kikanda kwa ajili ya amani, usalama na ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ulioanza leo mjini Bujumbura Burundi

Urithi wa DRC ni wa watu wa DRC, tuhakikishe ni chanzo cha maendeleo na sio migogoro:Guterres

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema utajiri na urithi wa rasilimali zilizosheheni nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ni wa watu wa Congo na si vinginevyo n ani jukumu la kanda nzima na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha unakuwa chanzo cha maendeleo na mafanikio na sio vita.

Guterres ameyasema hayo katika ufunguzi wa mkutano wa 11 wa mfumo wa ufuatiliaji wa kikanda kwa ajili ya amani, usalama na ushirikiano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC ulioanza leo mjini Bujumbura Burundi na kuongeza kuwa eneo la Maziwa Makuu lina utajiri mkubwa ambao ni utajiri wa asili shukrani kwa rasilimali zake nyingi na utajiri wa kitamaduni unaotoka kwa watu wake.

Lakini amesema “mwaka baada ya mwaka, utajiri huu wa kipekee unadhoofishwa na wizi, migogoro na vita. Kwa miongo kadhaa, watu wa eneo hilo wamekuwa waathiriwa na uporaji na vurugu.”

Makubaliano yalileta matumaini

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kutiwa saini miaka kumi iliyopita kwa mkataba wa mfumo kuliibua matumaini mengi.

Kliashiria hatua ya mabadiliko, ambapo nchi za eneo hilo zilijitolea kwa dhati kukomesha mzunguko wa mara kwa mara wa ghasia  hasa mashariki mwa DRC  na kujenga amani na usalama wa kudumu.

“Nazipongeza nchi zilizotia saini pamoja na taasisi zilizotoa dhamana kwa kazi iliyofanyika hadi sasa ya kutekeleza mkataba huu wa mfumo.Lakini kwa bahati mbaya mgogoro wa sasa unadhihirisha kibarua ambacho bado tunacho kutimila lengo hilo.”

Ameendelea kutanabaisha kwamba “Licha ya juhudi zetu za pamoja, zaidi ya vikundi mia moja vyenye silaha vya Congo na vya nje bado vinafanya kazi hadi leo na hivyo kutishia uthabiti wa eneo lote la Maziwa Makuu.”

Amesema kuwepo kwa makundi haya yenye silaha ya M23, ADF, FDLR, CODECO, RED-Tabara na wengine kusababisha majanga ya kibinadamu na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia.

Pia yanachochea kutoaminiana na mivutano ya hivi karibuni kati ya nchi katika eneo hilo.

Familia iliyotengana wakikimbia ghasia mashariki mwa DRC imeunganishwa tena mjini Goma. (Maktaba))
© UNICEF/Jospin Benekire
Familia iliyotengana wakikimbia ghasia mashariki mwa DRC imeunganishwa tena mjini Goma. (Maktaba))

Zahma ya wakimbizi

Bwana Guterres amesema nchini DRC, tangu kuibuka upya kwa kundi la M23 mwezi Novemba 2021, ‘Zaidi ya watu 500,000 wamelazimika kukimbia makazi yao.

Hali katika jimbo la Ituri pia bado inatia wasiwasi sana. Ni wakati wa vurugu kukomesha. Narudia ombi langu kwa makundi yote yenye silaha, wekeni silaha zenu chini mara moja na mjiujiunge na uondoaji, upokonyaji silaha na mchakato wa kuunganishwa tena katika jamii.”

Pia ametia wito kwa viongozi wa kisiasa na jamii kukomesha kauli za chuki na uchochezi wa ghasia.

Amesisitiza kuwa “Pande zote lazima zitekeleze maamuzi yaliyochukuliwa chini ya mchakato wa Luanda na Nairobi bila kuchelewa na bila ubaguzi. Mazungumzo pekee ya mara kwa mara na ya dhati yatawezesha kupata maelewano ya kudumu. Nakaribisha juhudi za hivi karibuni za viongozi katika Ukanda huo za kuepuka kuongezeka kwa mivutano.”

UN na MONUSCO wako bega kwa bega nanyi

Katibu Mkuu ameuhakikishia mkutano huo kwamba Umoja wa Mataifa na mpango wake wa kulinda Amani nchini DRC ujulikanao kama MONUSCO wataendelea kuunga mkono juhudi za kikanda ikiwemo za jeshi la Jumuiya ya Afrika Mashariki na ametoa wito kwa wadau wote wa kimataifa kufanya hivyo.

Amekaribisha maelewano ya wahusika katika kanda kuhusu hatua zisizo za kijeshi zinazolenga kupokonya silaha, kurejesha na kuunganishwa tena kwa vikundi vya kigeni vyenye silaha katika nchi yao ya asili.

Pia amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukwepaji sheria ni hatua nyingine muhimu akitaka “Wahusika wa uhalifu wa kuvuka mpaka na kimataifa lazima wafikishwe mbele ya sheria.”

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini. (MAKTABA)
MONUSCO
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wakisindikiza wapiganaji wa M23 waliojisalimisha Kivu Kaskazini. (MAKTABA)

Utajiri wa DRC na kanda nzima

Guterres amesema Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na ukanda mzima lina utajiri mkubwa wa maliasili.

Mathalani bonde la Congo ni makazi ya msitu wa pili kwa ukubwa duniani  unaochangia asilimia 10 ya viumbe hai duniani.

Una wingi wa viumbe vya kipekee vya wanyama na mimea na madini mengi ya thamani.

Urithi wa DRC ni wa watu wa Congo. Ni lazima tuhakikishe kuwa unakuwa chanzo cha ustawi na maendeleo si migogoro, mashindano na unyonyaji usio endelevu-Antonio Guterres.

Amekumbusha kuwa amani na maendeleo lazima viende pamoja, na ili amani iwe endelevu, sauti za wanawake, vijana na watu waliokimbia makazi yao lazima zisikike kikamilifu katika michakato yote ya kisiasa, usalama na mahakama. Ametaka watu hao wasisahaulike.

Amehitimisha hotuba yake kwa kuzichagiza nchi zilizotia saini, Muungano wa Afrika, mkutano wa kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika kuongeza juhudi zao maradufu.

“Katika muktadha huu, ninakaribisha hatua iliyochukuliwa na Baraza la Amani na Usalama la Muungano wa Afrika mwezi Februari kuhuisha mfumo huo. Umoja wa Mataifa bado unashiriki kikamilifu, na uko upande wenu. Kwa pamoja tu tunaweza kufikia malengo ya pamoja ya amani, usalama na ushirikiano wa Mfumo wa Addis Ababa.Watu wa ukanda huu wanatutegemea.”