Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama ungeni mkono kwa dhati hatua za kutokomeza M23- Bi. Pobee 

Askari wa kulinda amani wakisindikiza msafara wa misaada ya kibinadamu kuelekea kijiji cha Pinga huko Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
© UNICEF/Guy Hubbard
Askari wa kulinda amani wakisindikiza msafara wa misaada ya kibinadamu kuelekea kijiji cha Pinga huko Kivu Kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Baraza la Usalama ungeni mkono kwa dhati hatua za kutokomeza M23- Bi. Pobee 

Amani na Usalama

Ongezeko la hivi karibuni la mashambulizi kutoka kikundi cha waasi cha M23 huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC linatishia amani, usalama na  utulivu kwenye ukanda mzima wa Maziwa Makuu barani Afrika na hivyo hatua za dharura za kudhibiti ghasia hizo zinahitajika, amesema Afisa Mwandamizi wa Umoja wa Mataifa hii leo wakati akihutubia Baraza la Usalama la umoja huo jijini New York, Marekani. 

Martha Pobee, ambaye ni Msaidizi wa Katibu Mkuu katika masuala ya siasa na operesheni za ulinzi wa amani amesema, “ni vema Baraza hili likapatia uzito kamilifu kwenye hatua zinazoendelea za kikanda za kutokomeza kabisa mashambulizi yanayofanywa na M23.” 

Wito wa kusalimisha silaha 

Raia ndio wanaolipa gharama za ghasia zinazoendelea huku akinukuu takwimu kutoka Ofisi ya Umoja wa MAtaifa ya kuratibu masuala ya dharura, OCHA

Watu wapatao 75,000 wamefurushwa wiki iliyopita huko jimboni Kivu Kaskazini ilhali wengine 11,577 wamevuka mpaka na kuingia nchini Uganda. 

Walinda amani wawili wanaohudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO, walijeruhiwa katika mashambulizi hayo huku askari 16 wa jeshi la serikali ya DRC, FARDC wakiuawa na wengine 22 walijeruhiwa. 

Kwa kauli moja, Umoja wa Mataifa na wadau wake wametoa wito kwa M23 kuweka silaha chini na kujiunga na mchakato wa kusalimisha silaha na kuvunja makundi. 

Bi. Pobee amewaeleza wajumbe wa Baraza hilo kuwa “natiwa moyo kwamba DRC na Rwanda wameamua kupeleka katika mfumo wa uthibitishaji ulio chini ya Mkutano wa kimataifa wa ukanda wa Maziwa Makuu, ICGLR uitwao EJVM, ili kuchunguza taarifa za uharibifu wa mali na majeruhi dhidi ya binadamu yatokanayo na matumizi ya vilipuzi vilivyorushwa kutoka katika nchi zao tarehe 23 mwezi uliopita wa Mei. 

Mazungumzo hayana mjadala 

Muungano wa Afrika nao umetoa wito kwa viongozi wa DRC na Rwanda kushinikiza kupatikana kwa suluhu ya mzozo huo kwa njia ya amani. 

“Hakika, kila jitihada inapaswa kuchukuliwa ili kuhakikisha pande husika zinatumia kwa ufanisi mifumo iliyoko ya kutatua ikiwemo EJVM, ambao una dhima kubwa katika kusongesha mazingira ya kuaminiana na ushirikiano ambavyo vinasalia kuwa muhimu katika kutatua changamoto zozote za kiusalama zinazokumba DRC na jirani zake,” amesema Bi. Pobee. 

“Kuendelea kwa mazungumzo na mashauriano kati ya serikali husika ni jambo lisilo na mjadala na ni muhimu sana ili kuepusha kuongezeka zaidi kwa ghasia mashariki mwa DRC,” ameeleza Bi. Pobee. 

Kuepusha janga lingine 

Mjumbe Maallum wa Katibu Mkuu katika Ukanda wa Maziwa Makuu, Huang Xia alihutubia wajumbe kwa njia ya video ambapo amesema, “kinachoendelea hii leo ni kidokezo cha kile kilichofanywa na M23 takribani muongo mmoja uliopita wakati kundi hilo lilipoutwaa mji wa Goma, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini.” 

Amesihi wajumbe wa Baraza la Usalama kufanya kila linalowezekana kuepusha kusambaa zaidi kwa mashambulizi sambamba na kuepush ajanga lingine ambalo linaweza kuwa na madhara yasiyopimika ya kisiasa na kibinadamu kwenye ukanda huo. 

Bwana Huang, akihutubia kwa lugha ya kifaransa amesema, kutokomeza vikundi vilivyojihami mashariki mwa DRC kunahitaji mpango wa kina, hususan katika muktadha wa kuibuka ten ana mashambulizi kutoka M23. 

Hata hivyo amesema anashawishika kuwa, nguvu za kijeshe pekee si suluhu na hivyo kupatia  msisitizo hatua zinazoendelea za ofisi yake za ushirkishaji. 

Amesisitiza pia umuhimu wa kuendelea kwa mashauriano ya ngazi ya juu baina ya viongozi wa kinada na umuhimu wa kupatia shime mifumo ya ushirikiano baina ya serikali na pia kikanda kama vile ICGLR na mchakato wa Nairobi au Nairobi Conclave. 

Nairobi Conclave ni mazungumzo yanayofanywa chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Afrika MAshariki, EAC ambayo tayari DRC ni mwanachama. Mkutano wa kwanza ulifanyika Aprili 8 mwaka huu wa 2022 na mkutano wa pili ulifanyika tarehe 21 mwezi Aprili mwaka huu. Mikutano yote ilifanyika Nairobi Kenya na ni ya ngazi ya marais. 

Napeleka  ujumbe mahsusi 

Kuanzia kesho Bwana Huang anatembelea nchi zote husika za ukanda wa Maziwa Mkuu kupeleka ujumbe mahsusi. 

“Ujumbe wangu kwa nchi hizo ni kwamba, ukanda huu hauhitaji janga jipya; hebu na tuendelee kuacha wazi fursa za mawasiliano katika ngazi zote ikiwemo ngazi ya jumuiya, na tusaidie kutunza maendeleo yalifikiwa katika miaka ya karibuni kupitia mifumo mbalimbali ya ushirikiano.”