Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuongezeka kwa ghasia nchini Sudan kunaweka mamilioni ya watoto katika hatari – Mkuu UNICEF

Afaf Briema, afisa lishe wa UNICEF nchini Sudan akiwa na watoto wa kike wakimbizi wa ndani kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abushok nchini Sudan.
© UNICEF/Mustafa Abdalrasol
Afaf Briema, afisa lishe wa UNICEF nchini Sudan akiwa na watoto wa kike wakimbizi wa ndani kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abushok nchini Sudan.

Kuongezeka kwa ghasia nchini Sudan kunaweka mamilioni ya watoto katika hatari – Mkuu UNICEF

Afya

Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) Catherine Russell akieleza hii leo kuhusu hali ya watoto nchini Sudan ameeleza kinagaubaga namna hali iliyo hatarishi nchini humo kiasi cha kuwaweka watoto katika hatari kubwa. 

"Siku tano za uhasama mkali nchini Sudan, na makataa manne ya kusitisha mapigano, tayari yamesababisha madhara makubwa kwa watoto wa nchi hiyo. Ikiwa vurugu hazitakoma, idadi hii itaongezeka tu.” Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo jijini New York Marekani imemnukuu Catherine Russell.  

Mkuu huyo wa UNICEF ameeleza kuwa takriban watoto 9 wameripotiwa kuuawa katika mapigano hayo, na zaidi ya watoto 50 wameripotiwa kujeruhiwa huku uhasama ukiendelea Khartoum, Darfurs na Kordofan Kaskazini. Hali ya hatari ya usalama nchini kote inafanya kuwa vigumu sana kukusanya na kuthibitisha taarifa, “lakini tunajua kwamba wakati mapigano yakiendelea, watoto wataendelea kulipa gharama.” 

Akielezea zaidi hali ilivyo tete Bi. Russell ameeleza kwamba familia nyingi zimenasa katika mapigano makali, wakiwa na umeme mdogo au hawana kabisa, wanahofu kuhusu mapigano na uwezekano wa kukosa chakula, maji na dawa. Maelfu ya familia zimelazimika kutoka makwao kutafuta usalama. 

“Tumepokea taarifa za watoto kuhifadhiwa shuleni na vituo vya kulelea watoto huku wakipambana na ghasia zinazowazunguka, hospitali za watoto kulazimika kuhama huku makombora yakizidi kusogea, na hospitali, vituo vya afya na miundombinu mingine muhimu kuharibiwa, na hivyo kuzuia upatikanaji wa huduma muhimu na za kuokoa maisha na dawa. Mapigano hayo yamevuruga huduma muhimu, ya kuokoa maisha kwa watoto wanaokadiriwa kufikia 50,000 walio na utapiamlo uliokithiri. Watoto hawa walio katika mazingira magumu wanahitaji matunzo endelevu, ya kila saa, ambayo yanawekwa hatarini kutokana na ongezeko la ukatili.” Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF ameeleza.  

Mapigano hayo pia yanaweka hatarini utaratibu mzima wa uhidahi wa chanjo nchini Sudan, ikiwa ni pamoja na chanjo ya zaidi ya dola milioni 40 na insulini, kutokana na kukatika kwa usambazaji wa umeme na kutoweza kuhifadhi jenereta kwa mafuta. 

Hata kabla ya kuongezeka kwa ghasia, mahitaji ya kibinadamu nchini Sudan yalikuwa juu zaidi kuliko hapo awali. Usaidizi wa kibinadamu ni muhimu, “lakini UNICEF, na wadau wetu, hawawezi kutoa msaada huo ikiwa usalama na usalama wa wafanyakazi wetu haujahakikishwa. Mioyo na mawazo yetu iko pamoja na wapendwa wa wenzetu wa WFP waliopoteza maisha au kujeruhiwa. UNICEF, na mashirika mengine ya kibinadamu, yameporwa na watu wenye silaha. Mashambulizi kama haya dhidi ya wafanyakazi wa misaada na mashirika ni mashambulizi kwa watoto na familia tunazohudumia.” Amesema kwa maskitiko Bi. Russell.  

UNICEF inarejea wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa vikosi vinavyopigana kukomesha uhasama mara moja na kutoa wito kwa pande zote kuheshimu wajibu wao wa kimataifa wa kuwalinda watoto dhidi ya madhara, na kuhakikisha kuwa wahusika wa misaada ya kibinadamu wanaweza kuwafikia watoto wanaohitaji msaada kwa usalama na haraka. UNICEF pia inatoa wito kwa wahusika wote kujiepusha na kushambulia miundombinu ya kiraia ambayo watoto wanategemea - kama vile mifumo ya maji na vyoo, vituo vya afya na shule.