Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wapatao 400,000 wakabiliwa na utapiamlo kasai DRC: UNICEF

UNICEF kukabiliana na changamoto ya utapiamlo kwa kinamama na watoto nchini DRC. Picha: UNICEF

Watoto wapatao 400,000 wakabiliwa na utapiamlo kasai DRC: UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF,  limesema zaidi ya watoto 400,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano huko  eneo la Kasai nchini jamhuri ya kidemokrasia la Congo, DRC,  wanakabiliwa na utapiamlo  uliokithiri .

Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC,  Dkt. Tajudeen Oyewale amesema matatizo ya lishe kwa  watoto hao yamesababishwa na migogoro nchini humo, hivyo kufanya familia nyingi kukimbilia maeneo ambayo ni vigumu kwa mashirika ya kibinadamu kufikishia huduma ya lishe bora na matibabu kwa   watoto.

Aidha, Dkt. Tajudeen amesema hali ni  hatarishi iwapo misaada ya dharura haitowafikia  familia hizo haraka iwezakano.

Ijulikane kwamba migogoro ya kikabila , na kisiasa katika mikoa iliyopo eneo la Kasai nchini DRC, imesababisha ukimbizi wa ndani kwa   watu wapatao milioni 1.4 ambao waathirika wakubwa ni wanawake, watoto na wazee wasiojiweza.

Tangu Januari 2017, UNICEF na washirika wake wametoa huduma ya lishe na  matibabu kwa watoto  wapatao 50,700 wenye utapiamlo mkali, wenye umri kati ya miezi 6 na 59, katika mkoa wa Kasai.