Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapigano Sudan yanaweza kuwatumbukiza mamilioni kwenye njaa: WFP

Lishe maalum inayotolewa na WFP imeboresha hatua kwa hatua utapiamlo mkubwa nchini Sudan, na familia pia zimepokea chakula kama vile unga, maharagwe makavu, mafuta na chumvi.
© WFP/Mohammed Awadh
Lishe maalum inayotolewa na WFP imeboresha hatua kwa hatua utapiamlo mkubwa nchini Sudan, na familia pia zimepokea chakula kama vile unga, maharagwe makavu, mafuta na chumvi.

Mapigano Sudan yanaweza kuwatumbukiza mamilioni kwenye njaa: WFP

Msaada wa Kibinadamu

Mlipuko wa ghasia nchini Sudan una uwezekano wa kuwatumbukiza mamilioni zaidi ya watu kwenye njaa. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limelazimika kusimamisha kwa muda shughuli za kutoa msaada wa chakula na pesa zinazookoa maisha katika nchi ambayo theluthi moja ya watu tayari wanatatizika kupata chakula cha kutosha imeeleza taarifa iliyotolewa leo mjini Roma-Italia na Khartoum-Sudan.

Idadi kubwa ya watu tayari walikuwa wakikabiliwa na njaa nchini Sudan kabla ya mzozo huo kuzuka Aprili 15. Mwaka huu 2023, WFP ilipanga kusaidia zaidi ya watu milioni 7.6. Mapigano yanayoendelea yanazuia WFP kutoa chakula muhimu cha dharura, kutoa chakula shuleni kwa watoto, au kuzuia na kutibu utapiamlo. WFP pia haiwezi kufanya kazi yake ya kusaidia wakulima ili kuongeza tija katika kilimo katika mradi unaolenga zaidi ya maradufu ya uzalishaji wa ngano wa kila mwaka wa Sudan, wala kuwasaidia watu kujenga upya maisha yao. 

Kingine kinachosikitisha ni kwamba wafanyakazi watatu wa WFP wamefariki dunia katika mapigano hayo, huku wengine wawili wakipata majeraha makubwa. Wafanyakazi wa WFP, ofisi, magari, vifaa na akiba ya chakula vimekuwa moja kwa moja katika uwanja wa mapigano. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Huduma za Kibinadamu kwa njia ya  Anga (UNHAS), linalosimamiwa na WFP kwa niaba ya jumuiya ya kimataifa, limesimamisha kabisa huduma nchini Sudan. Kwa kawaida UNHAS husafiri kwa ndege hadi katika vituo zaidi ya 30 nchini Sudan ikibeba takriban abiria 26,000 na mizigo midogo ya kibinadamu kila mwaka. Ndege moja imeharibika mno kiasi cha kutowezekana kurekebishika na iko Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Khartoum. Wakati huo huo takriban magari kumi na lori sita za chakula zimeibwa. 

Nyumba za wageni, ofisi, na maghala ya WFP huko Nyala, Darfur Kusini yamezidiwa na kuporwa, na kupoteza hadi tani 4,000 za chakula kwa watu wenye njaa. 

WFP inatoa wito kwa pande zote kwenye mzozo kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wa kibinadamu na kulinda mali na majengo ya kibinadamu nchini Sudan. WFP inazitaka pande zote kukomesha mapigano na kufikia makubaliano ambayo yatawezesha kuendelea kusambaza chakula muhimu na misaada ya kibinadamu.