Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akiwa katika ziara ya kushitukiza Guterres aichagiza jumuiya ya kimataifa kuishika mkono Somalia

Katibu Mkuu wa UN António Guterres alipokutana na familia ya wakimbizi wa ndani katika kambi ya Baidoa kusini magharibi mwa Somalia.
UN Photo/Sourav Sarker
Katibu Mkuu wa UN António Guterres alipokutana na familia ya wakimbizi wa ndani katika kambi ya Baidoa kusini magharibi mwa Somalia.

Akiwa katika ziara ya kushitukiza Guterres aichagiza jumuiya ya kimataifa kuishika mkono Somalia

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiendeleza utamaduni wa mshikamano na mataifa ya Kiislam  wakati wa mwezi mtukufu wa mfungo wa Ramadhan leo amewasili Somalia ambako amesisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa kuishika mtono nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na kuipunguzia madhila ya kibinadamu na kusaidia juhudi za serikali za kujijenga upya.

Akiwa mjini Moghadishu bwana Guterres amesema” Pia Niko hapa kutoa tahadhari ya haja ya msaada mkubwa wa kimataifa unaohitajika kwa sababu ya changamoto kubwa za kibinadamu zinazolikabili taifa hili hasa katika kujenga uwezo wa masuala ya usalama Somalia, na msaada wa kibinadamu kwa ajili ya kurejesha utulivu na maendeleo ya nchi.”

Ameongeza kuwa “Ingawa Wasomali hawachangii chochote katika mabadiliko ya tabianchi ,lakini ndio miongoni mwa waathirika wakubwa wa zahma hiyo. Takriban watu milioni 5 wanakabiliwa na viwango vya juu vya kutokuwa na uhakika wa chakula, na bila shaka mfumuko wa bei imefanya mambo kuwa mabaya zaidi. Hivyo natoa wito kwa wahisani na kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada wao.”

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito huo wakati wa mkutano wa Pamoja na Rais Hassan Sheikh Mohamud  kwa waandishi wa habari kwenye ofisi za serikali za Villa Somalia mjini Moghadishu maara baada ya kuwasili.

Mara ya mwisho Guterres alikuwa Somalia miaka sita iliyopita.

Mamilioni ya watu wanahitaji msaada

Baadaye akiambatana na mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa Somalia ambaye pia ni msaidizi wa Katibu Mkuu nchini humo Adam Abdelmoula, Katibu Mkuu amejionea kwa macho baadhi ya Wasomali walioathirika na mgogoro mkubwa wa kibinadamu nchini humo walipozuru kwenye kambi ya wakimbizi wa ndani mjini Baidoa mji ambao ndio mkubwa zaidi kwenye jimbo la Kusini Magharibi la Somalia.

Katika kambo ya ADC Guterres amekutana na familia mbili, ambapo familia ya kwanza ililazimika kusafiri kilometa 105 kwa mguu na kisha kwa punda kusaka usalama Baidoa baada ya mifugo yake yote kufa kutokana na ukame mkali.

Na familia ya pili ilifanya vivyo hivyo baada ya mifugo yake kufa na ilisafiri kilometa 70 kusaka msaada.

Baada ya kukutana na familia hizo Guterres amesema “Ni wakati wa Jumuiya ya kimataifa kukusanya msaada zaidi kwa ajili ya Wasomali , kusaidia Somalia kuhakikisha usalama wa watu wake na kupambana na ugaidi, kuwasaidia Wasomali kutatua changamoto za kibinadamu ambazo tunazishuhudia kama kambini hapa. Pia msaada kwa Somalia katika kujenga mnepo kwa watu wake na kuandaa njia kuelekea maendeleo kwa watu wa taifa hili.”

Ameendelea kusema kwamba” Katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan tunahitaji ukarimu kutoka kwa jumuiya ya kimataifa ambao ni muhimu sana ili kuwanusuru watu hawa ambao nimewashuhudia kambini na wale wanaoishi katika mazingira magumu.”

Makumi ya maelfu ya watu wamekimbia makazi yao nchini Somalia.
UN Photo/Sourav Sarker
Makumi ya maelfu ya watu wamekimbia makazi yao nchini Somalia.

Watu milioni 8.2 wanahitaji msaada

Kwa sasa, karibu nusu ya wakazi wa Somalia anbao ni watu milioni 8.25 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi wa kuokoa maisha kutokana na majanga ya mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na miaka mitano mfululizo ya misimu mbaya ya mvua, na migogoro ya muda mrefu, kulingana na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu  na misaada ya dharura (OCHA).

Kati ya hao, takriban watu milioni 3.8 ni wakimbizi wa ndani, na karibu watu milioni tano wanakabiliwa na viwango vya juu vya uhaba wa chakula.

Poia watoto wapatao milioni 1.8 wana utapiamlo uliokithiri, na watu milioni nane wanakosa maji ya kutosha, mifereji ya maji taka na usafi.

Theluthi mbili ya watu wote katika maeneo yaliyoathiriwa na ukame hawana huduma muhimu za afya.

Mpango wa hatua za misaada ya kibinadamu kwa 2023 ili kukidhi mahitaji ya Somalia unahitaji dola bilioni 2.6 kuweza kusaidia watu milioni 7.6 lakini ufadhili wake umekwami kwa karibu asilimia 15, hadi sasa.

Katika mkutano wa awali na waandishi wa habari mjini Mogadishu, mkuu wa Umoja wa Mataifa alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufadhili haraka mpango huo.

Alisema "Watu wa Somalia wanastahili mshikamano wa jumuiya ya kimataifa, na wanastahili kuzuia utapiamlo na kulazimika kuhama makazi yao, kuokoa maisha, na kuepusha baa la njaa.”

Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akikutana na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia mjini Mogadishu, Somalia.
UN Photo/Sourav Sarker
Katibu Mkuu António Guterres (kushoto) akikutana na Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia mjini Mogadishu, Somalia.

Msaada kwa ajili ya ujenzi wa taifa

Kabla ya mkutano huo na waandishi wa habari, Katibu Mkuu alikutana na Rais na baadhi ya wajumbe wa baraza lake la mawaziri na washauri kujadili mambo mengine, yakiwemo malengo mapana ya ujenzi wa serikali, pamoja na naibu mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa Somalia, Anita Kiki Gbeho ambaye pia anahudumu kama mkuu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia (UNSOM).

"Rais na mimi tumejadili juhudi muhimu za serikali za kukabiliana na ugaidi na kuendeleza amani na usalama kwa kila mtu, na tumesisitiza umuhimu wa ushirikiano wenye nguvu zaidi kati ya serikali ya shirikisho na nchi wanachama wa Shirikisho" amesema Guterres alisema.

"Mamlaka ya serikali ya Shirikisho na wanachama wa shirikisho wanaweza kutegemea msaada wetu kwa ajili ya ujenzi wa hali ya juu zaidi na tunatiwa moyo hasa na makubaliano ya hivi karibuni ambayo yalianzishwa kuhusiana na masuala tofauti ya kugawana mamlaka."

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuongeza msaada zaidi ya nyanja ya kibinadamu, kusaidia Wasomali "kuweza kuanzisha mchakato mpya wa utulivu na maendeleo katika nchi na kujenga uwezo wake wa kupambana na Al-Shabaab na hata kwa ufanisi zaidi kuliko ilivyokuwa hivi karibuni.”

Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya usalama vya Somalia, vikiimarishwa na wanamgambo wa ndani, vimefanya operesheni za kijeshi dhidi ya Al-Shabaab katika nchi wanachama wa shirikisho wa Hirshabelle na Galmudug, na operesheni zinatarajiwa kuhamia hatua kwa hatua katika maeneo mengine ya Somalia.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia waandishi wa habari katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Baidoa kusini magharibi mwa Somalia.
UN Photo/Sourav Sarker
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akihutubia waandishi wa habari katika kambi ya wakimbizi wa ndani huko Baidoa kusini magharibi mwa Somalia.

Mkutano na asasi za kiraia

Leo pia, mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amekutana na wawakilishi wa mashirika ya asasi za kiraia ya Somalia yanayofanya kazi katika nyanja kama vile masuala ya wanawake na uwezeshaji, mabadiliko ya tabianchi, watu wenye ulemavu, vijana na makundi yaliyotengwa ili kusikia moja kwa moja kuhusu kazi zao na jinsi chombo hicho cha dunia kinavyoweza kuwaunga mkono.

Baadaye jioni hiyo hiyo akiwa na wajumbe wa serikali ya shirikisho na wawakilishi wa jumuiya ya kimataifa, Guterres amehudhuria futari, chakula kilichoandaliwa kwa ajili ya machweo ili kuvunja mfungo wa kila siku unaozingatiwa na Waislamu wakati wa Ramadhani.

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa alianza utamaduni wake wa kufanya ziara za mshikamano ambazo ni pamoja na yeye kufunga pia wakati wa Ramadhani alipokuwa kamishna mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa wakimbizi, kabla ya kuchukua kazi ya juu kabisa ya Umoja wa Mataifa mwaka wa 2017.

Hapo awali alisema kuwa kuungana na Waislamu kufunga wakati wa Ramadhani. kwa miaka mingi, imemuonyesha “taswira ya kweli wa Uislamu.”

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Mogadishu leo, alibainisha kuwa Somalia inakumbatia "ujumbe muafaka wa wakati wa Ramadhani ambao ni wa kuzaliwa upya na matumaini."

"Katika nyakati hizi zenye changamoto, nataka kupongeza nguvu na uthabiti wenu na kusisitiza uungwaji mkono usioyumba wa Umoja wa Mataifa," amesema Guterres na kuongeza kuwa "Tunasimama kwa mshikamano na watu wa Somalia na serikali ya Somalia kwa amani, usalama na maendeleo endelevu."